Wenye Shinyanga yao wafunguka kulikoni wanakuwamo ‘nne bora ya malaria’ kitaifa

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 09:00 AM Feb 06 2025
Watoto wamelel ndani ya chandarua
Picha: WHO
Watoto wamelel ndani ya chandarua

UGONJWA wa malaria umekuwa tatizo kubwa katika maisha ya jamii, ukiambatana na madhara hadi hatua mbaya ya kifo.

Kitaaluma una kinga kadhaa, ikiwamo matumizi ya chandarua. Ni bahati mbaya kuna uelewa mdogo kwa wanajamii kuhusu kinga hiyo, umma ukiwa na mitazamo tofauti. 

Wapo ambao wamekuwa wakituhumiwa na matumizi potofu ya vyandarua, katika ufugaji vifaranga vya kuku wasiweze kuliwa na kunguru na wanyama wengine.

Aidha, hiyo inatajwa kushamiri zaidi katika ukanda na mikoa yenye maziwa na mabwawa makubwa, nako kukitumika kuvulia samaki wadogo na hasa dagaa, sababu ikitajwa ni ukosefu wa elimu sahihi ya matumizi yake.

Baadhi yao hasa wanaoishi vijijini, pia wanatajwa kuhusisha malaria na imani za kishirikiana, wakielekeza tiba zao kwa waganga wa jadi.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka jana, inakadiriwa watu milioni 263 wameugua malaria duniani, huku 597,000 walifariki katika nchi 83.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya WHO iliyotolewa Desemba mwaka jana, idadi hiyo ya maambukizi, inatajwa kuwa juu zaidi kwa maambukizi ya watu milioni 11 kulingana na mwaka 2022 na wastani wa vifo takriban vikifanana kwa miaka hiyo inayofuatana.

Hata hivyo, WHO inaonyesha tahadhari kwamba asilimia 95 ya vifo hivyo (wastani 567,150) vimetokea katika nchi za Kiafrika na idadi iliyobaki (wastani 29,850) ndio vinatokea katika mabara mengine duniani.

Pia, katika namna inayoonyesha malaria kuongezeka duniani, takwimu ya vifo duniani mwaka 2019 ilikuwa na maambukizi milioni 229 na vifo 409,000.

HALI ILIVYO NCHINI

Takwimu za Kitaifa za Viashiria vya Malaria kwa Mwaka 2022 (Malaria Indicator Survey-2022), kiwango cha maambukizi ya malaria kitaifa ni asilimia 8.1%, mkoa Tabora ukiongoza kwa asilimia 23.4, ukifuatiwa na Mtwara (20%), Kagera (18%), kisha Shinyanga (16%), ambayo ni sawa ana asilimia 197.5 ya iliyopo kitaifa.

Kukabiliana nayo nchini, Wizara ya Afya imeibua mbinu mpya ya kugawa vyandarau bure kila kaya, kuhakikisha kasi yake inazuliwa kuwa tishio kwa umma.

Serikali pia, inaendelea kukabiliana na malaria kwa kunyunyizia dawa za kuua viluwiluwi vinavyosababisha ugonjwa huo kwenye makazi ya watu.

Vilevile kuna mwendelezo wa ugawaji vyandarua vyenye dawa na hasa kwa wajawazito kliniki, huku ikiendana na utoaji   elimu kwa wananchi, namna ya kujikinga na kuua mazalia ya malaria. 

WIZARA AFYA/TAMISHEMI

Ofisa Mradi Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kutoka Wizara ya Afya, Wilfred Mwafungo, anasema serikali kwa kushirikiana na wadau wake wa afya wanaendesha mbinu kadhaa.

Anataja kugawa chandarua bure kwa kila kaya, vikitolewa kupitia maofisa watendaji wa kata, vijiji na vitongoji na wale watakaobainika kuwauzia wafanyabiashara, wanachukulia hatua za kiutumishi, kwani inatajwa ni kuihujumu serikali katika mapambano yake.

Mwafungo anasema, utafiti uliofanyika umebaini, endapo mwananchi atatumia vema chandarua chenye dawa kulala ndani yake, ana nafasi ya kujikinga na ugonjwa kwa asilimia 63.

 Anahimiza, kinachotakiwa kufanyika ni kuendeleza utoaji elimu kwa wananchi, kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya chandarua, usafi wa mazingira na kuzuia maji kutuama, ili kuua mazalia ya mbu.

Vilevile ana angalizo akitaka kuhakikisha havitumiki kwa uvuaji samaki, kufuga kuku na bata au kuuzwa kwa wafanyabiashara.

Mdhibiti wa Wadudu Dhurufu kutoka Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Best Yoram, anasema, kuna vyandarua 1,542,836 vimetolewa mkoani Shinyanga na katika yake 841,503 (asilimia 54.54%) vitatolewa wilayani Kahama.

Hapo Yoram anatoa mchanganuo kwa halmashauri: Msalala itapata vyandarua 260,350; Ushetu 268,872; na Manispaa Kahama 312,836.

Anaeleza kitaifa, viashiria vya malaria mwaka 2022, kiwango cha maambukizi kilikuwa asilimia 8.1.

Yoram anawakumbusha wananchi kuacha kutumia dawa pasipo kupima na kujua anachoumwa, baadhi yao wamekuwa wakiumwa kichwa na kuhusisha na moja ya dalili ya ugonjwa wa malaria, huku wengine na hasa wanaoishi vijijini wakizama na mazoea kukimbilia tiba kwa waganga wa jadi, hali iliyo kinyume na kanuni za afya. 

KULIVYO KAHAMA

Mboni Mhita, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, anaeleza serikali imekuwa ikibuni mbinu za kukabiliana na ugonjwa huo, lakini inakwamishwa na wananchi kutozingatia maelekezo wanayopewa.

Hapo anawanyooshea vidole maofisa watendaji wa kata na vijiji, wanaotuhumiwa kuuza chandarua kwa wafanyabiashara.

Mkuu wa Wilaya – Mhita, anatamka kashfa zao, kwamba awali waliwadanganya wananchi kwamba vyandarua vimeisha, hata wakakwamisha mapambano hayo ya malaria. 

Kidole chake cha ukali akakifikisha pia kwa wafanyabiashara wanunuzi wa vyandarua vya wizi, akinena hatua za kisheria, ikiwamo kufikishwa mahakamani kwa dai la kuhujumu serikali, akitaja wilayani kwake vimetengewa vyandarua 841,503.

VIONGOZI WA DINI

Alhaji Omari Damka, Shekhe wa Wilaya ya Kahama, anasema, elimu inahitajika kuendelea kutolewa kwa wananchi, kuhusu matumizi sahihi ya vyandarua na uuaji wa mazalia ya mbu.

Anasema, katika msimu uliopo wa kilimo, pia mjumuiko wa wakulima kupitia vyama vyao, itumike kuwafikishia elimu na mgawo wa vyandarua, huku yeye akitumia kuwasilisha hilo muda wa ibada.

Mchungaji wa Kanisa la Anglikana, Emmanuel Maziku, anamuuga mkono akisema elimu ya matumizi ya chandarua kutibu malaria kwa wananchi hasa wa vijijini, imesahaulika kulinganisha na maradhi mengine.

Anashauri umma vijijini watembelewe, wakipatiwa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo unaozuilika, kupitia chandarua chenye dawa.

Maziku kama alivyo mtangulizi wake mdhamini wa kiimani, anaahidi kutumia     nafasi yake kufikisha darasa la malaria na umuhimu wa chandarua katika ibada zake.

Mchungaji Maziku ana maelezo: “Kipindi cha ugonjwa wa Uviko-19, tulishirikiana na wataalamu wa afya kila kona na tukahamasishana namna ya kujikinga kwa kuvaa barakoa na kunawa mikono wakati wote na tulifanikiwa.

Anaendelea: “Na hili suala la ugonjwa wa malaria, tunaweza kulidhibiti kama tutakuwa na ushirikiano wa kutoa elimu juu ya matumizi ya chandarua…nawaahidi somo hili litakuwa moja ya mada zangu kila siku kanisani.”

SAUTI YA WAKAZI

Mkazi wa Mtaa wa Masaki, Kata ya Malunga, Manispaa ya Kahama Shukrathi Juma, anasema wengi wao hawana elimu sahihi ya utumiaji chandarua na wamekuwa wakitumia kipindi cha ujauzito wao kwa maelekezo ya kiliniki.

Anakiri kuwapo wenzao kinamama, wanapopewa vyandarua kliniki, huishia kuwekewa uvunguni mwa vitanda majumbani, akiainisha sababu ni dunia na wapo wanaotumia kufugia kuku na bata.

Greyson Dotto, anayeishi Kata ya Nyasubi, Kahama, anasema mikoa yenye shughuli za uvuvi ameshuhudia wavuvi wakitumia vyandarua kuvua dagaa, akitaka nao wakaelimishwe undani wa mapambano ya malaria.

Anasema, hata yeye awali hakuona umuhimu wa chandarua, mpaka pale alipougua na kulazwa hospitalini kwa wiki mbili, vilevile mkewe akapata darasa kama hilo kliiniki, alipokuwa mjamzito.

“Kwa sasa, nikiumwa malaria sio kwa sababu ya kutotumia chandarua (neti) bali nitakuwa nimeipata wakati wa kutizama televisheni na familia yangu.

“Muda wa kulala nahakikisha wote wako kwenye chandarau na wanaolala bila chandarua huwa nawapatia adhabu…” anasema Dotto.