SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya, huku katika sura ya pili taifa rafiki la China, likiendeleza uwekezaji kitaaluma na vifaa.
Lengo ni kufanyika uwekezaji mkubwa katika fani hiyo, kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya, ikithibitishwa na waziri mwenye dhamana, Jenista Mhagama.
Anasema, serikali kupitia Wizara ya Afya, imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Afya, kukabiliana na vifo vitokanavyo na magonjwa ya moyo.
Waziri Mhagama anasema kuwa, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2019, zinaonyesha kuwa takribani watu milioni 17.9 hupoteza maisha kila mwaka, kutokana na magonjwa ya moyo, ikiwa sawa na asilimia 32 ya vifo vyote.
Ni tamko lake Waziri Mhagama, kwenye uzinduzi wa Kliniki ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), iliyopo Oyster Bay, Dar es Salaam.
"Kati ya vifo hivi, asilimia 85 husababishwa na mshtuko wa moyo pamoja na kiharusi. Takwimu hizi zinaonyesha ukubwa wa tatizo la magonjwa haya duniani na Tanzania ikiwamo," anaeleza.
Waziri anasema, kutokana na changamoto hiyo kubwa duniani, serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ikafanya uwekezaji mkubwa kwa kiwango cha kimataifa, kwenye vifaa tiba pamoja na mitambo, zikiwamo mashine za uchunguzi wa magonjwa kama; MRI, CT- Scan na Ultrasound.
"Katika taasisi hii ya JKCI, Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amewezesha usimikwaji wa mashine tatu za ‘Cathlab carto’ kwa ajili ya upasuaji kwa njia ya tundu dogo.
“Upasuaji huu umepunguza kwa kiwango kikubwa muda wa mgonjwa kukaa hospitali," anasema Waziri Mhagama.
Anafafanua kuwa, serikali inaendelea kuhakikisha hospitali zinakuwa na uwezo wa kutoa huduma za matibabu kwa wananchi katika namna mbalimbali, ikiwamo programu ya tiba mkoba (Outreach Programme) ijulikanayo kwa jina la ‘Dk. Samia Suluhu Hassan Outreach Programme.’
"Upanuzi wa huduma za kibingwa za matibabu ya magonjwa ya moyo katika hospitali zetu za kanda; Chato, Hospitali ya Benjamin Mkapa, Hospitali ya Kanda Mtwara na nyinginezo, umeonyesha dhamira ya dhati na kutafsiri kwa vitendo dhana ya Utalii Tiba, watu kutoka mataifa mengine kuja kutibiwa nchini," anasema.
Pia, Waziri Mhagama anaeleza mkakati wa ‘Bima ya Afya Kwa Wote’ unaendelea, akiahidi utakuwa mworobaini wa changamoto nyingi za upatikanaji huduma za afya nchini.
Hapo anahimiza: “Kwa pamoja tuungane katika kuwaelimisha wananchi umuhimu wa ‘Bima ya Afya kwa Wote’ kuwa ndio mkombozi wa huduma za matibabu kwa Watanzania," anasema Waziri Mhagama.
MKUU JKCI
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk. Peter Kisenge, anasema taasisi hiyo kwa sasa inaweza kuwaona wagonjwa hadi 300 wa upasuaji wa tundu na wagonjwa 800 wa upasuaji wa kifua kwa siku.
Anaeleza kwamba wamejiwekea malengo ya kuwaona wagonjwa 3,500 wa upasuaji wa tundu kwa mwaka, pia wagonjwa 900 wa upasuaji wa kifua kwa mwaka.
MSAADA SH. MILIONI 125
Serikali ya China katika kuiunga mkono Tanzania, imeipatia vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 125 vilivyokabidhiwa kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam.
"Msaada huu ni mchango muhimu sana katika kukabiliana na mahitaji ya huduma za afya kwa wananchi, pia katika kuimarisha ushirikiano na urafiki kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China,” anasema.
Waziri Mhagama anautaka uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, kuvitunza vifaa hivyo na kuvihudumia kwa wakati inapobidi, vitumike muda mrefu, kuimarisha utoaji huduma wenye matokeo chanya kwa umma.
Waziri Mhagama anasema, serikali ya China imeendelea kutuma timu ya wataalamu wa afya nchini kila baada ya miaka miwili.
Anataja kwamba imekuwa mkubwa kwa hospitali nchini, kupitia mafunzo wanayotoa kwa wataalamu wa ndani zikiwa za ngazi za ubingwa na ubobezi.
Balozi wa China nchini, Chen Ming Jian, anasema nchi yao itaendelea kushirikiana na Tanzania kuboresha huduma za afya kwa wananchi, ikiwamo katika vifaa tiba, akitaja ushirikiano huo una zaidi ya miaka 60.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi, anaishukuru Wizara ya Afya kudumisha ushirikiano wake na China, akitamka " ushirikiano huu unamanufaa makubwa sana Tanzania hasa katika sekta ya afya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED