Wanufaika wa TASAF na simulizi kuuaga ufukara

By Restuta James , Nipashe
Published at 07:36 AM Jul 30 2024
Shufaa Mfinanga mkazi wa Kilimani Manispaa ya Moshi, mnufaika wa TASAF, anayeendeleza biashara.
PICHA: RESTUTA JAMES
Shufaa Mfinanga mkazi wa Kilimani Manispaa ya Moshi, mnufaika wa TASAF, anayeendeleza biashara.

TAKWIMU za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, zinaonesha kwamba idadi ya Watanzania ni milioni 61. Kati yao, asilimia nane wanaishi katika wimbi la umaskini, wakishindwa kumudu milo mitatu kwa siku, makazi na mavazi.

Asilimia hiyo ni sawa na Watanzania 5,195,605 wanaoishi katika umaskini uliokithiri au mafukara ambao kwa uwiano asilimia 55.7 ni wanawake na 44.3 wanaume.

Ili kuliondoa kundi hilo kwenye lindi la umaskini, serikali ilianza kutekeleza mradi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), kuanzia mwaka 2000, ikiwa ni moja ya mbinu ya kuzinusuru kaya zinazoishi katika mstari wa umasikini.

Katika jitihada za kuzikwamua, serikali imekuwa na mipango kadhaa ukiwamo ule wa utoaji wa ruzuku ya fedha taslimu kwa kaya hizo kila mwezi na utekelezaji wa miradi muhimu ya huduma za kijamii kama afya na elimu.

Mipango hiyo imeonesha mafanikio katika sekta za afya, elimu na kuongezeka kwa rasilimali katika kaya. Matokeo hayo chanya yamepanua afua za TASAF, kiasi cha kuwa ni mfumo wa kinga ya jamii tangu mwaka 2012, yakilenga kuziwezesha kaya maskini kuongeza vipato na fursa za kujikimu.

Ni afua hizo ambazo zinahitimisha kipindi cha pili cha TASAF awamu ya tatu kinachofikia tamati mwakani. Aidha, mpaka sasa ni takribani kaya 400,000 zilizonusuriwa kutoka kwenye ufukara hadi kumudu mahitaji yote ya msingi pamoja na kuweka akiba.

Kaya hizo ni zile zinazohudumiwa na TASAF kutoka Halmashauri 187, Tanzania Bara na Visiwani.

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Shedrack Mziray, anaanza kwa kueleza kuwa, madhumuni ya kipindi cha pili katika awamu hii ni kuongeza fursa za kujiongezea kipato na kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii kwa kaya za walengwa na kulinda masilahi ya watoto wao.

Anasema mfuko huo umejikita katika kuzikwamua kaya za walengwa kupitia maeneo matatu ambayo ni ruzuku ya fedha kwa wanufaika ili kujiongezea kipato na kuwekeza katika afya na elimu ya watoto.

Mziray anasema ili kuinua uchumi wa kaya, mfuko huo unazijengea uwezo katika utunzaji wa rasilimali, kutengeneza njia mbadala na endelevu za kipato na ajira za muda mfupi mathalani kwa kushiriki katika kazi za jamii.

“Kwenye ile miradi ambayo inaibuliwa na jamii katika ngazi ya kijiji au mtaa, kaya zenye watu wenye uwezo wa kufanyakazi tunawawezesha kuitekeleza ili kupata ujuzi na stadi za maisha,” anasema Mziray.

Mziray anasema mikakati hiyo imefanikisha kaya 400,000 kuondoka kwenye ufukara (umaskini uliokithiri), baada ya kufanikiwa kumudu huduma za msingi za chakula, makazi na mavazi. Zikifanikiwa kujenga nyumba na kuziwekea umeme na kuanzisha miradi ambayo inawahakikishia kipato cha muda mrefu.

Anasema, kaya hizo zinaondolewa kwenye mpango baada ya kufanyiwa tathmini na kujiridhisha kwamba zinaweza kujitegemea.

"Kaya hazitakiwi zikae kwenye mpango milele. Utaratibu unataka kwamba, tukishawatambua tuwaondoe kwenye umaskini uliokithiri. Tunawawezesha kiuchumi, kukuza kipato cha kaya na kutengeneza rasilimali watu kupitia utekelezaji wa miradi ya ujenzi inayowapa stadi za maisha," anasema Mziray.

Kwa mujibu wa Mziray, kipindi cha pili cha TASAF awamu ya tatu kilichoanza mwaka 2020 hadi 2025, kinagharimu Sh. trilioni mbili, ambazo ni mkopo wa Dola za Marekani 650 kutoka Benki ya Dunia (WB) na michango ya wadau wa maendeleo kutoka Jumuiya ya Ulaya (EU), Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN), Sweden, Ireland, Norway na Dola milioni 50 kutoka Umoja wa Nchi zinazouza zaidi mafuta duniani (OPEC).

Mkurugenzi wa Mradi wa TASAF, John Stephen, anasema kaya zinazoondolewa zinapatiwa ruzuku ya Sh. 350,000 kwa ajili ya kuanzisha mradi utakaoziingizia kipato cha uhakika kwa muda mrefu.

Anasema kaya 83,666 zimepewa Sh. bilioni 17.1 kama ruzuku ya tija ya kujikimu, mafunzo na ushauri wa biashara ambazo zimefanikiwa kuanzisha miradi midogo ya kuwaingizia kipato.

Anataja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ufugaji wa nguruwe, kuku wa nyama, njiwa wa mapambo, mbuzi, uanzishaji wa biashara ndogo kama za genge, uuzaji wa gesi ya kupikia na kilimo cha bustani.

"TASAF inasaidia uwekezaji huu kwa ujuzi wa kukuza biashara na mafunzo ya kiufundi. Jumla ya vikundi vya akiba vya wanufaika 60,327 vyenye wanachama 838,241 vimeundwa. Kiasi cha akiba katika vikundi ni Sh. 7.9 bilioni. Kati ya akiba hizo, Sh. bilioni 3.2 zimetolewa kama mikopo kwa wanachama kwa ajili ya kuwekeza katika shughuli zao za kuwaingizia kipato," anasema.

KAULI YA WANUFAIKA

Baadhi ya wanufaika wa ruzuku ya uzalishaji, katika Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wameonyesha ubunifu kwa kuanzisha miradi ya ufugaji, ushonaji na biashara ndogo.

Mkazi wa Mtaa wa Kariwa Chini, Kata ya Rau, Caroline Minja, anasema, alijiunga na TASAF mwaka 2015 akiwa anaishi kwenye chumba kimoja cha udongo na watoto wake watatu na kwamba ruzuku ya kila mwezi imemwezesha kununua mahitaji ya watoto na kujenga nyumba ya kuishi.

Anasema TASAF imempa mafunzo ya namna ya kutunza fedha, kuendesha biashara na kuikuza jambo lililomwezesha kufuga nguruwe, kuanzisha kilimo cha bustani na genge linalomwingizia kipato kila siku.

“Kama mnavyoona nimejenga nyumba ya vyumba viwili kwa matofali ya kuchoma, ina umeme na nimefanikiwa kuanzisha genge kwa ajili ya kipato cha kila siku. Nimejiunga pia na kikundi cha kuweka na kukopa ili niendelee na nidhamu ya kutunza fedha,” anasema.

Anasema mtoto wake mmoja, amefanikiwa kusoma hadi chuo kikuu na amepata mkopo kwa asilimia 100 baada ya TASAF kumtambulisha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Mkazi wa Mtaa wa Sabasaba katika Kata ya Rau, Lucy Tenga, anasema ruzuku ya uzalishaji imemwezesha kuanzisha mradi wa kufuga kuku wa nyama ambao unamwingizia kipato cha uhakika kila baada ya wiki nne.

“Watoto nao wamesoma na nimejifunza kuweka akiba. Ninachoweza kusema ni kwamba fedha kidogo inaweza kutupeleka mahali pazuri, kwa sababu ruzuku tuliyokuwa tunapewa haikuwa kubwa lakini baada ya mafunzo kutoka kwa wataalamu tumejua kutumia na kuweka akiba,” anasema.

Selina Msofe, anasema amefanikiwa kujenga nyumba na kuweka maji na umeme, pia anafuga nguruwe na kuku ambao wanamwingizia kipato cha uhakika.

“Umaskini sasa kwa heri. Kwa sasa nafuga kuku na nguruwe. Nilianza na nguruwe mmoja, akazaa nikauza nikajenga banda la pili kisha nikaongeza zaidi. Baadaye nikajenga banda la kuku ambapo nao wananiingizia kipato,” anasema.

Kama walivyo wanufaika wengine, Anna Raphael, mkazi wa Sabasaba katika Kata ya Kiborloni, anasema ruzuku ya TASAF imemwezesha kufuga njiwa wa mapambo ambao wanamwingizia kipato kikubwa.

“Njiwa hawa, jozi inauzwa kati ya 250,000 hadi 300,000. Nimejenga nyumba kama mnavyoona na nafuga kuku na njiwa. Nimeondoka kwenye aibu ya kukosa mlo na sasa naweza kusimama mbele za watu. Tumefundishwa utaratibu mzuri wa kuhakikisha tunaweka akiba kila wiki kupitia vikundi tulivyounda,” anasema.