Wanamapinduzi Kusini mwa Afrika, China kumuenzi Nyerere

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:44 AM Oct 02 2024
Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Professa Marcelina Chijoriga, kada wa CCM Steven Wasira, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara mstaafu, Phillip Mangula.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Professa Marcelina Chijoriga, kada wa CCM Steven Wasira, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara mstaafu, Phillip Mangula.

OKTOBA 14 kila mwaka Tanzania na wapenda amani na maendeleo duniani hufanya kumbukizi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Ndiye aliyeiongoza nchi kwa mafanikio kati ya mwaka 1961 hadi 1985 alipong’atuka uongozini, ameiachia Tanzania amani na mshikamano.

Nyerere ni kiongozi wa pili kustaafu kwa hiari madaraka ya urais barani Afrika, akifuata nyayo za Rais wa kwanza wa Senegal, Leopold Sedar Senghor aliyestaafu 1980 na kumkabidhi madaraka aliyekuwa Waziri Mkuu wake, Mamadou Dia Abdou Diouf.

Ni kwa msingi huo waliokuwa wapigania uhuru wa Afrika Kusini, Zimbabwe, Angola, Msumbiji, Namibia na CCM Ijumaa ijayo Oktoba 11 wanakutana Kibaha kwa Mfipa mkoa wa Pwani kumuenzi  Mwalimu Nyerere.

Ni katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere -Julius Nyerere Leadership School (MJNLS) kwenye mdahalo wa kuukumbuka na kuenzi mchango wa Baba wa Taifa katika harakati za ukombozi Afrika.

Profesa Marcelina Chijoriga, Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere anaeleza kuwa mdahalo huo unatarajiwa kuhudhuriwa na wageni 200 kutoka ndani na nje ya nchi.

Anafafanua kuwa utaendeshwa kwa kauli mbiu “Mwalimu Nyerere na Harakati za Ukombozi wa Bara la Afrika: Tafakuri ya Mshikamano, Uongozi, Umajumui na Umoja wa Afrika”.

Aidha, Profesa Marcelina, anasema utafunguliwa rasmi na rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Anaongeza kuwa rais mstaafu amethibitisha kufungua na kushirika mdahalo huo ambao pia unatarajiwa kuhudhuriwa na Thabo Mbeki rais mstaafu wa Afrika Kusini na Mkuu wa Majeshi wa Zimbabwe, Luteni Jenerali, Anselem Sanyatwe.

Taarifa zaidi za mdahalo huo zinaonyesha kuwa mada tisa zitawasilishwa na kujadiliwa zikiwa na maudhui mbalimbali kuhusu Mwalimu Nyerere na harakati za mapambano ya ukombozi wa Afrika.

Mada hizo pamoja na watakaoziwakilisha katika mabano ni  Uongozi na Urithi: Matokeo ya Maono ya Mwalimu Nyerere kwa Viongozi wa Sasa wa Afrika(Thabo Mbeki), na Jukumu la Mwalimu Nyerere katika Mapambano ya Ukombozi  Afrika, Kanali mstaafu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Joseph Simbakalia.

Mada zaidi zitakazowakilishwa na kujadiliwa ni ile inayotolewa na Mkuu wa Majeshi ya Zimbabwe, Luteni Kanali, Sanyatwe atakayezungumzia “Changamoto na Fursa za Kuendeleza Dira ya Nyerere: Mtazamo kutoka kwa vyama Rafiki Sita”.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) atajikita katika andiko lenye mada “Ujenzi wa Madaraja: Matokeo Endelevu ya Msaada wa Nyerere katika Uhusiano wa Kimataifa na Afrika.

Dk. Charles Mubita Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama tawala Namibia SWAPO, atazungumzia “Jukumu la Elimu ya Itikadi katika Kuhifadhi Alama ya Nyerere.”

Itakumbukwa kuwa vyama vya CCM, MPLA cha Angola, ZANU PF ya Zimbabwe, ANC ya Afrika Kusini, FRELIMO cha Msumbiji, SWAPO ya Namibia, na Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kwa pamoja vinamiliki chuo cha MJNLS.

Vyama hivyo vitawakilishwa na Stephen Wasira MNEC na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.

 “Komredi Wasira atawasilisha mada ya Maono ya Mwalimu Nyerere kuhusu Afrika kujitegemea kiuchumi huku mjumbe wa Bodi ya Usimamizi ya MNJLS inayoundwa na wawakilishi kutoka CCM, SWAPO, MPLA, FRELIMO, ANC, ZANU PF na CPC, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda akitoa neno la shukurani na kufunga mdahalo huo,” anafafanua Professa Marcelina. 

 Historia ya harakati za ukombozi inasema kuwa mara baada ya kupinduliwa kwa serikali ya Rais, Kwame Mkrumah wa Ghana 1966, Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika ililazimika kuhamishia makao makuu Tanzania, baada ya serikali  kukubali kuipokea.

Kuwapo kwa makao makuu ya Kamati ya Ukombozi ya OAU kulifanya vyama vya kupigania uhuru vya Guinea Bissau na  Cape Verde,  ZANU PF, ZAPU PF vyote vya Zimbabwe na ANC, PAC na SACP vya Afrika Kusini kuhamishia makao yake  Dar es Salaam.

Au kuwa na ofisi za uwakilishi hapa nchini hali iliifanya Tanzania kuwa kinara wa harakati za mapambano ya ukombozi wa Afrika.

Vyama vya ukombozi wa ANC na PAC, ZANU-PF chini ya uongozi wa Dk. Robert Mugabe, SWAPO kikiongozwa na Sam Nujoma, FRELIMO ikiiongozwa na  Erduado Mondlane na baadaye Samora Machele vilikuwa na  makambi ya kufundishia wapigania uhuru wa majeshi ya ukombozi ya vyama hivyo.

Makambi ya wapigania uhuru hao yalikuwa katika mikoa ya Iringa (Mgagao), Dodoma (Kongwa), Mtwara katika Wilaya ya Nachingwea, eneo maarufu kama Farm 17, Tabora (Kigwa) na pia mkoani Morogoro (Dakawa).

 “Ni Makambi ya ANC chini ya uongozi wa Oliver Tambo ambaye alikuwa na makao makuu yake huko Lusaka na ya FRELIMO ndiyo yalikuwa makubwa sana hapa nchi ambapo ANC walikuwa na kambi ya Solomon Mahlangu, Mazimbu nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro,” anasema ofisa mmoja jina tunalo. 

Akiwa mmoja wa maofisa katika Kamati ya Ukombozi wa Afrika iliyokuwa na makao makuu Dar es Salaam, anaomba jina lake lisitajwe akisema ni kinyume cha kiapo na maadili ya kazi yake.

Anaongeza kuwa katika kambi au shule ya uongozi ya ANC ya Solomon Mahlangu Mazimbu au Solomon Mahlangu Freedom College (SOMAFCO) kulikuwa na maelfu ya wapiganaji wa ANC wakipata mafunzo ya aina mbalimbali.

Anasema walifunzwa uongozi na kujitayarisha kuchukua nafasi za uongozi mara serikali ya kidemokrasia chini ya ANC itakapotwaa madaraka huko Afrika Kusini jambo lililokuja kutokea mwaka 1994 pale Nelson Mandela alipoapishwa kuwa rais wa kwanza Mwafrika.

 “Kwa upande wa FRELIMO na ZANUPF pia zilikuwa na idadi kubwa ya wapiganaji wakipata mafunzo huko Kongwa, Mtwara, Mbeya, Iringa na Bagamoyo katika mkoa wa Pwani.” Anasema.

Anaongea kuwa ni katika kambi ya Bagamoyo ambapo Rais wa sasa wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, aliishi na kupata mafunzo, baadaye kuwa moja ya maofisa wa tawi la kijeshi la ZANUPF.