WAFUGAJI WAMWAMBIA NCHIMBI: Licha ya kushinda kesi mahakamani hakuna anayewafidia ‘walichoporwa’

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 08:35 AM Oct 23 2024
Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, akuhutubia mkoani Simiyu.
PICHA: HALFANI CHUSI
Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, akuhutubia mkoani Simiyu.

ZIARA ya Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, mkoani Simiyu imeahidi kutoa mwanga kwa wafugaji waliodhulumiwa haki yao baada ya kushinda kesi mahakamani.

Ni wilayani Meatu, anapoarifiwa kuwa licha ya baadhi ya wafugaji kushinda kesi ya kutaifishiwa mifugo yao, miaka mitatu iliyopita hata leo hawajalipwa. 

Mbali na kero za wananchi pia ziara hiyo, inajikita kuangalia uhai wa chama, kuhamasisha watu kujitokeza kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa na pia mambo yanayokwamisha maendeleo kama kuwanyima wananchi haki zao. 

Akipinga unyanyasaji, wilayani Meatu, Dk. Nchimbi, anasema hatavumilia mambo yanayofanywa kinyume cha sheria na viongozi serikalini, akisema ni muumini wa utawala wa sheria. 

Ni baada ya Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, kudai kuwapo kwa wafugaji ambao mifugo yao ilitaifishwa na kushinda kesi mahakamani miaka mitatu iliyopita lakini mpaka leo hawajalipwa. 

"Nitalibeba suala hilo mpaka nihakikishe haki inapatikana kama walishinda kesi mahakamani hatupaswi kuwakimbia," anaahidi Nchimbi.   

Baada ya hoja za Mpina, Nchimbi anasema chama kitatetea wananchi wanyonge na kuwashirikisha katika masuala yote muhimu. 

Akiwa Bariadi, Dk. Nchimbi aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, anapokea kero ya soko na stendi akisema serikali itazitatua. 

Hata hivyo, pamoja na majibu hayo kwa wananchi, anawasiliana kwa simu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, kutoa ufafanuzi kwa wananchi waliokuwa na shauku ya kujua ufumbuzi wa changamoto hizo. 

Akijibu Mchengerwa anasema:  "Rais amezingatia malalamiko hayo na ametuelekeza eneo hilo linapelekewa fedha ya ujenzi wa soko na barabara. 

"Tutakuwa hapo Lamadi kuanzia mwezi ujao kufanya maboresho kwa sababu fedha tulionayo inalenga kujenga soko la kisasa na barabara kwa kiwango cha lami urefu wa kilomita nane," anasema Mchengerwa kwa simu na kushangiliwa na Wanalamadi.  

Anaongeza kuwa wataalamu watakaokwenda mategemeo yao ni kufanya tathmini na kuongeza ujenzi wa stendi na kwamba kuanzia mwezi ujao wanategemea kutangaza zabuni ya ujenzi wa soko la kisasa na barabara.

Akikata simu ya Mchengerwa katika mkutano huo, Dk. Nchimbi alirusha dongo kwa vyama vya upinzani kwamba havina mipango thabiti ya kuongoza nchi. 

"Kiongozi madhubuti anazungumzia mipango ya kuongoza nchi. Lakini vyama vya upinzani wakipata nafasi wanazungumza maandamano, kuchana kanga na kuzomea.

 "Viongozi wa CCM wanaandaliwa, hakuna kiongozi ndani ya chama atakaa miaka 40. CCM itaendelea kuwa chama kijana zaidi kwani ina viongozi vijana na wazee wenye kuwalea vyema," anasisitiza. 

Anatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na CCM akisisitiza chama hicho kina nia njema ya kuwatumikia wananchi. 

Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji unaotarajiwa kufanyika mwezi huu anatoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi akiahidi kuwa chama chake kitateua wagombea wenye kujali changamoto za wananchi na siyo maslahi binafsi. 

Akiwa Lamadi anaahidi chama hicho kitatoa 2,000,000 kuunga mkono ujenzi wa vituo vya madereva wa bodaboda katika mji wanaolalamikia kuteseka na jua. 

UMOJA, AMANI

Kwa wakazi wa Bariadi, kiongozi huyo anasisitiza umoja, amani na mshikamano na kwamba hiyo ndio njia ya kuliunganisha taifa. 

Anasema ndicho kitu cha thamani taifa lilichonacho kuliko kingine chochote, na hivyo, Watanzania lazima walinde kwa wivu mkubwa. 

“Watanzania wa vyama vyote tunapaswa tujue jambo ambalo tulilonalo lenye thamani kubwa ni amani, umoja, mshikamano wa taifa letu," anasema Nchimbi.  

Anasema kila anayejaribu kuuvuruga umoja aambiwe kwamba hatupo tayari kuvumilia nchi iingie katika machafuko. 

Anamsifu Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuonyesha kwa vitendo kuwa anawapenda watu wake kwa kuhangaika kutafuta fedha za miradi ya maendeleo, kusimamia na kuhakikisha inatekelezwa. 

“Tunapenda na tunataka kuwa na Rais ambaye anaweza kuonyesha kwa vitendo kwamba anapenda watu wake, kwa jinsi anavyohangaika kutafuta fedha za miradi ya maendeleo lakini anavyoisimamia na kuhakikisha inatekelezwa.” 

“Kwa hiyo kazi tuliyonayo ni ya kuendelea kumuunga mkono ili aendelee kuitumikia nchi yetu kwa uaminifu, upendo mkubwa na nchi yetu iendelee kupata maendeleo.” Anasisitiza Nchimbi.  

MAKALLA

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, anapozungumzia uchaguzi anasema kuhamasisha wananchi kujiandikisha, kuweka mawakala waaminifu kisha kuhimiza kujitokeza kwa wingi katika upigaji kura. 

Anaahidi chama kitateua wagombea wenye sifa ya kuwatumikia wananchi, akidai upinzani umepoteza sera, unazungumzia udini, ukabila, kuchoma moto kanga, lakini ruzuku wanazopata hawachomi. 

"Rais Dk. Samia amerejesha mikutano ya kisiasa, akawarudishia ruzuku waliyokuwa wanadai, lakini ruzuku hawarudishi. Tunawaeleza kwamba CCM itashinda kwa haki kwani inaungwa mkono na Watanzania," anasisitiza. 

HAKUNA MAENDELEO

Kada wa CCM aliyejiengua CHADEMA, Peter Msigwa anasema Tanzania iko salama chini ya uongozi wa chama hicho na kwamba wanaodhani vyama vya upinzani vitawaletea maendeleo wafumbue macho kwani vimebaki kile anachokiita kulialia. 

Anasema  alikuwapo huko kwa zaidi ya miaka 20, ameona hakuna maendeleo wala  demokrasia, akisisitiza kwamba Rais Samia ameua upinzani kwa vitendo. 

 “Niwaombe wananchi tujitokeze kuchagua viongozi wanaotokana na chama hiki wala msidanganyike kule hakuna viongozi wa kuendesha nchi 

“Ninaomba niwaulize kati ya sungura na mamba nani anayajua maji vizuri? Mimi ni kama mamba kwa CHADEMA naijua  ndani na nje,” anasema Msigwa.  

Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Rabia Abdallah Hamid, anawataka vijana kujituma na kufanya kazi za kuwaingizia kipato akiwahimiza kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotarajiwa kuanza kutolewa muda wowote kuanzia sasa.

Mikopo hiyo ya halmashauri hutolewa kwa wanawake asilimia nne, vijana kiwango hicho na wenye mahitaji maalumu hupata asilimia mbili, ikipewa jina la uwiano wa 4:4:2.