MOJA ya matukio ya kushangaza na kukumbukwa kwenye Ligi Kuu Tanzania wiki hii ni Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga, kufungwa mara mbili mfululizo kitu ambacho kimewaacha mdomo wazi mashabiki na wapenzi wa timu hiyo.
Ilifungwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC Jumamosi ya Novemba 2, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, kabla ya kuchabangwa mabao 3-1 dhidi ya Tabora United, Alhamisi iliyopita.
Kipigo cha pili ni kikubwa zaidi kwa timu hiyo, ambapo si mara nyingi sana kwa timu kubwa kama Simba na Yanga kupoteza kwa idadi kubwa kama hiyo ya mabao.
Yalikuwa ni mabao mawili ya Offen Chikola, dakika ya 19 na 45 na la Nelson Munganga, dakika ya 78, huku Clement Mzize akifunga bao la kufutia machozi dakika za majeruhi, Tabora United ikiibuka na ushindi wa 3-1.
Kilikuwa ni kipigo kikubwa cha sita kwa timu hiyo kwa misimu 17 iliyopita ya Ligi Kuu.
Katika makala haya tunakuletea matokeo ya mechi ambazo Yanga ilikumbana na vipigo vikubwa zaidi, vitano kwenye Ligi Kuu kuanzia msimu wa 2008/09...
1# Yanga 4-5 Villa Squad (2008/09)
Ulikuwa mchezo wa mwisho wa kumaliza Ligi Kuu msimu wa 2008/09, uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Yanga ilipokubali kipigo cha mabao 5-4 dhidi ya Villa Squad iliyokuwa ikijipapatua kubaki Ligi Kuu.
Mechi hiyo ilichezwa Aprili 27, 2009, ambapo mabao ya washindi yalifungwa na Chesido Mathew aliyepachika mawili, Jackson Makweta, Mau Aniu na Ally Msigwa.
Mabao ya Yanga yalifungwa na Boniface Ambani aliyefunga mawili, Bernad Mwalala na Idd Moshi.
2# Yanga 3-4 Simba (2009/10)
Msimu uliofuata, Yanga ilikutana na kichapo kingine kikubwa cha mabao 4-3 dhidi ya watani wao wa jadi, Simba, mechi ikichezwa, Aprili 18, 2010, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Ulikuwa ni msimu wa Ligi Kuu 2009/10, huku mabao ya washindi yakifungwa na Uhuru Selemani, Mussa Hassan Mgosi aliyepachika mabao mawili, na Hillary Echessa aliyefunga bao la ushindi dakika za majeruhi.
Mabao ya Yanga yaliwekwa kwenye nyavu na Jerry Tegete, aliyefunga mawili, na Athumani Idd 'Chuji.'
3# Yanga 0-5 Simba (2011/12)
Kipigo kingine kikubwa ilichokipata Yanga, kilikuwa tena dhidi ya Simba, safari hii ulikuwa ni msimu wa 2011/12 wa Ligi Kuu, mechi ikichezwa, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Ilichezea kipigo cha mabao 5-0, mchezo ukipigwa, Mei 5, 2012, ambapo Simba ilipata mabao yake matatu kwa mikwaju ya penalti zilizofungwa na Felix Sunzu, Juma Kaseja na Patrick Mafisango na zote zilipatikana baada ya mchezaji hatari kipindi hicho aliyekuwa akicheza kama winga, wakati mwingine straika, Emmanuel Okwi, kuangushwa ndani ya eneo la hatari. Mganda huyo alifunga mabao mengine mawili katika mchezo huo.
4# Yanga 0-3 Mtibwa Sugar (2012/13)
Wakati ikiongozwa na kocha Mbelgiji, Tom Saintfiet, Yanga ilikumbana na kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, msimu wa 2012/13, katika mchezo uliochezwa, Septemba 19, 2012, Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Dakika ya 12 tu, Dickson Daudi aliifungia Mtibwa bao la kwanza, kabla ya straika tegemeo wa timu hiyo wakati huo ambaye baadaye alihamia Yanga, Hussein Javu, kufunga mabao mengine mawili, dakika ya 45 na 77.
5# Yanga 0-3 Kagera Sugar (2019/20)
Ilikuwa ni Januari 15, 2020, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Yanga iliangukia pua kwa kuchabangwa mabao 3-0 dhidi ya wageni Kagera Sugar.
Mbelgiji Luc Eymael ndiye aliyekuwa akiifundisha timu hiyo, ambayo ilishindwa kuwazuia vijana wa Kagera Sugar kupata ushindi mnono katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2019/20.
Yusuph Mhilu, aliipatia Kagera Sugar bao la kwanza dakika ya 13, kabla ya Ally Ramadhani 'Kagawa' kufunga bao la pili na aliyeshindilia msumari kwenye jeneza la Yanga, alikuwa ni Peter Mwalyanzi, akifunga bao la tatu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED