Ushirika yaingilia soko pamba, ikibeba wakulima kwa ubunifu ‘malipo ya pili’

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 06:17 AM Apr 19 2024
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme (katikati), akikabidhi mfano wa hundi ya Sh. milioni 128.304 kwa Mwenyekiti wa AMCOS ya Isanjabadugu Jumanne Gwesa, kuwalipa wakulima wa pamba wa Ushetu, Msalala na Manispaa ya Kahama, waliokiuzia KACU.
Picha: Shabani Njia
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme (katikati), akikabidhi mfano wa hundi ya Sh. milioni 128.304 kwa Mwenyekiti wa AMCOS ya Isanjabadugu Jumanne Gwesa, kuwalipa wakulima wa pamba wa Ushetu, Msalala na Manispaa ya Kahama, waliokiuzia KACU.

KATIKA Kanda ya Ziwa, zao la pamba linashika nafasi kutetea maisha yao kiuchumi, ikiwa ni zao la biashara.

 Walioko shambani ni wakulima wadogo,  ambao mchango wao unategemewa zaidi kuleta mageuzi, wakimiliki mashamba ukubwa kuanzia ekari moja, hadi 10. 

Aidha, wakulima hao wanakaodiriwa kufikia 600,000 nchini wametapakaa katika mikoa takribani 17, katika Kanda mbili; Magharibi na Mashariki. Wengi wanalima mazao mchanganyiko kujiongezea kipato na chakula kifamilia. 

Pamba inayolimwa Tanzania, inategemea zaidi soko la nje kwa asilimia 60 na asilimia 40 kwa viwanda vya ndani. Inatajwa sokoni inahitajiwa sana, kuliko kiwango cha uzalishaji uliopo, kwa sasa unafika marobota 300,000 pekee. 

KACU KWENYE USHINDANI 

Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU) kwa kuona umuhimu huo, kimeingia kwenye ushindani wa kununua pamba, kuchakata na kuuza nyuzi zake dhidi ya kampuni nyinginezo. 

KACU ilianza hatua hizo kwa mtindo wake kimasoko ‘malipo ya kwanza na pili’. Mara ya kwanza msimu wa kilimo 2019/2020, ambao kila kilo ililipa Sh.40 na zaidi ya Sh. milioni 90 zilitumika kwa malipo, hasa kutoka wilaya za: Kahama na Kishapu mkoani Shinyanga, pia Nyang’hwale mkoani Geita. 

USHIRIKA KACU 

Mwenyekiti wa Bodi ya KACU, Tano Nsabi, anasema kuna zaidi ya wakulima 1000 wanaolima mazao mchanganyiko ya chakula na biashara, ikiwamo pamba katika halmashahuri za Msalala, Ushetu na Manispaa ya Kahama. 

Pia, wanahakikisha mbolea na pembejeo zinawafikia kwa wakati kulingana na majira yake. 

Anasema, ongezeko la uzalishaji pamba umekuwa ukitegemea. Hata hivyo anasema, kunapokuwapo mvua nyingi, zao hilo hushidwa kuchanua kupata pamba za kutosha. 

Nsabi anasema ni hatua inayolenga kuwafanya kuweka ushindani wa bei na kampuni nyingine, pia, wakiwawezesha wakulima kuzalishe zaidi. 

Anasema fedha zinazotumika kununua mazao, zinatokana na mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB). 

Pia, anataja msimu wa kilimo 2023/2024, walikopa shilingi bilioni tisa na kununua jumla ya kilo milioni sita za pamba mbegu.

 Hivyo, anasema baada ya uchambuaji pamba kukamilika, wamefanikiwa kuzalisha marobota 10,608 za nyuzi zenye uzito kilo 1,959,715 na kilo 2,891,260 za mbegu.

 Kwa maana hiyo, anasema wamebakiza kilo 6,038 za pamba mbegu ambazo hazijachambuliwa, kwa ajili ya majaribio ya mitambo kwa msimu ujao.

 MALIPO YA PILI

 Nsabi anasema, malipo ya pili yameanza kutolewa tangu msimu wa kilimo wa 2020/2021 kwa kutolewa shilingi milioni 90.9 na faida iliyopatikana baada ya kununua na kuuza pamba nyuzi na mbegu, baada ya kuichakata katika kiwanda chao, mwaka huo walilipa shilingi 40 kwa kila kilo moja.

 Anasema, msimu huo walinufaika wakulima kutoka Wilaya ya Kishapu, Msalala, Ushetu, Manispaa ya Kahama na Nyang’hwale wa moa jirani, Geita. Kuna kilo milioni 2.2 zilinunuliwa na shilingi bilioni 2.049 zilitumika kununua pamba kwa wakulima.

 Aidha anasema, katika milioni 90 iliyotolewa wakulima wa Kishapu walipata milioni 56.071 sawa na kilo Milioni 1.4, Msalala milioni 3.2 sawa na kilo 82,045, Ushetu milioni 23.9 sawa na kilo 598,435, Manispaa ya Kahama milioni 1.003 sawa na kilo 25,091 na Nyang’hwale Mkoani Geita milioni 6.6 sawa na kilo 166,300.

 Nsabi anasema, msimu huu wa 2023/2024 wamelipa malipo haya kwa wakulima waliokiuzia chama kikuu cha ushirika(KACU) pamba kiasi cha Sh.milioni 186,316,776 hali iliyosaidia kuongeza uzalishaji na ushindani wa bei na makampuni mengine yanayonunua zao hilo

 Aidha malipo hayo yametolewa kwa wakulima wa Halmashauri za Msalala, Ushetu, Kishapu na Manispaa ya Kahama na kulipwa Sh.36 kwa kila kilo moja na wale waliouza pamba yao kwenye makampuni mengine wanakosa nafasi hii.

 Kadhalika, wakulima wa ushetu wamelipwa milioni 113,843,016 sawa na kilo milioni 3,162,306, Msalala kilo 241,760 sawa na Sh.milioni 8,703,360, Manispaa ya Kahama  kilo 159,960 sawa na Sh.milioni 5.758,560 huku wakulima wa kishapu wakiuza kilo milioni 1,611,440 sawa na Sh.milioni 58,011,840.

 Anasema wakulima walikiuzia chama pamba mbegu kilo milioni 5,175,466 na baada ya kuchakata na kuuza, wamewalipa sehemu ya faida shilingio.36 kwa kila kilo moja sawa na milioni 186.3, watakaotumia kuandaa msimu ujao 2024/2025.

 USHINDANI BEI

 Meneja wa pamba wa KACU, Amiri Mwinyimkuu, anasema kwa kipindi cha miaka minne mfululizo, wamekuwa na ushindani mkubwa wa bei ya zao hilo, dhidi ya kampuni nyingine.

 Anafafanua, katika msimu 2019/2020, bei elekezi iliyoetolewa na serikali ilikuwa Sh. 8,010 kwa kilo, ila wao wakainunua kwa Sh.9020.

 Mwinyimkuu anasema, kwa msimu uliofuata 2021/2022 walinunua pamba kilo milioni 3.469 kwa bei shilingi 1,456, huku bei elekezi ya serikali ikiwa shilingi 1,825. 

 Kwa  bei elekezi shilingi 1,560, msimu wa 2022/2023, walinunua kilo milioni 5.175, kukiwapo fedha za ruzuku zilizotolewa na serikali.

 Amiri anasema, katika msimu huo walichakata kilo milioni 5.175 za pamba, wakaziuza  na kupata faida shilingi milioni 390 na baada ya kutolewa gharama zake, pia makato ya kodi, chama ushirika kikabakiwa na shilingi milioni 186.316, wakulima wakilipwa shilingi 36 kwa kila kilo, malipo ya pili.

 MRAJISI & RC SHY

 Hilda Boniphace, ni Kaimu Mrajisi wa Mkoa wa Shinyanga, anasema malipo ya pili ya pamba yamehamasisha uzalishaji pamba kuongezeka na kuwapo ushindani mkubwa wa bei, kutoka kampuni za ununuzi wa pamba.

 Anasema msimu uliopita, mkoa ulizalisha kilo milioni 10.4 na sasa msimu uliopo wa 2023/2024, uzalishaji umefika kilo milioni 38, ingawaje katika uzalishaji ujao, wataalamu wananena matarajio  yaliyopo ni uzalishaji kushuka, kutokana athari za mvua nyingi, kwani zao hili linahitaji mvua kiasi.

 Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Christina Mndeme, anachukua nafasi hiyo kuipongeza Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika Kahama, kwa kutumia sehemu ya faida wanayoipata, kuongeza thamani zao shambani, ikitoa malipo ya pili kwa wakulima.

 Pia, anawataka maofisa ugani wote wa kata kuwatembelea wakulima na kuwaelimisha njia sahihi ya uchangangaji wa viuatilifu, kudhibiti wadudu washambulizi, ili kuingrza mavuno.

 Anasema mkoa umepokea shilingi bilioni 27 za miradi mbalimbali ya kilimo, ikiwamo ujenzi wa mabwawa makubwa mawili ya kilimo cha umwagiliaji na kununua pikipiki 224 za maaofisa ugani, watakaowatembelea wakulima kuwasaidia kitaalamu.

 WAKULIMA PAMBA 

 Katibu wa Chama cha Msingi Gimagi-Kishapu Raphael Mongo, anaomba wapewe elimu ya kuchanganya dawa za viuatilifu kudhibiti wadudu sugu, hata wakayafikia malengo ya uzalishaji shambani.

 Anakiri malipo ya pili ya wanunuzi chama cha ushirika, yanawahamasisha kuzalisha zaidi, akinena wanaouza pamba nje ya ushirika, wanayakosa. Pia, anasema fedha za awamu hiyo huwa, wanazielekeza kwenye maandalizi ya msimu unaofuata.

 Mkulima, Jumanne Gwesa wa chama ilichoko Isanjabadugu – Ushetu, anasema, wanapokosea, wakitumia viatilifu kwenye mazao mengine, hususani mahindi na kiasi kidogo kinachobaki, kinashindwa kuua wadudu wa pamba.