Dk. Mollel: Kiwanda mionzi kinanusuru, vifaa, teknolojia, utaalamu, miundombinu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:29 AM May 02 2024
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, alipokuwa mkoani Tabora wikiendi iliyopita.
Picha: Maktaba
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, alipokuwa mkoani Tabora wikiendi iliyopita.

CHINI ya wiki moja imepita, tangazo la Wizara ya Afya katika tovuti yake ikifafanua ‘uendeshaji wa huduma za kibingwa za wiki mbili mikoani, kati ya Aprili 29 na Mei 11’, ikiwa na nukuu:

“Huu ni uwekezaji mkubwa uliofanywa na Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuhakikisha mwananchi anapata huduma za kibingwa katika ngazi ya mkoa.”

Ni taarifa iliyofafanua azma ya Rais katika vipaumbele vyake; kuimarisha kupatikana huduma za kibobezi, kuwapo miundombinu bora na matabibu mabingwa.

Siku mbili kabla, daktari na Naibu Waziri wa Afya, Godwin Mollel, akiwa mjini Tabora anafafanua mageuzi ya kisekta aliyofanya Dk. Samia katika sekta ya afya, yanagusa uwekezaji kwenye; teknolojia, elimu na wataalamu na vifaa vya afya vinanunuliwa kwa wingi kitaifa kufika kila kona.

Ni ufafanuzi wake Jumamosi iliyopita mjini Tabora, akimwakilisha Naibu Waziri Mkuu, Dk. Dotto Biteko, kwenye Maadhimisho ya Miaka 25 ya Huduma ya Maendeleo ya Mtoto na Kijana nchini, yaliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Compassion.

Dk. Mollel anafafanua kuwa, Rais Dk. Samia ameonyesha upendo kwa jamii yake, akisogeza nyumbani huduma tiba iliyofuatwa mbali, pia teknolojia na utaalamu, sasa asilimia 97 ya huduma hizo ziko jirani.

Hapo anatumia stadi ya fani yake akifafanua mgonjwa wa kifua, miaka minne au zaidi iliyopita nchini ‘alifumuliwa’ kifua chote, sasa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), sasa mgonjwa huyo wa moyo anapitiwa padogo zaidi.

Naibu Waziri anafafanua: "Dk. Samia Suluhu Hassan alikuja Muhimbili, tukamwambia tuna shida maana watu wanakaa wodini na ugonjwa wa moyo unaleta gharama katika jamii kwa kukaa muda mrefu.”

Dk. Mollel, anataja faida ya bajeti yao pana, fedha zaidi ya shilingi bilioni 28 zimetolewa kununua vifaa tiba, ambavyo mgonjwa akiingizwa katika mashine, hakuna haja ya kufungua kifua na baada ya muda mfupi anaruhusiwa kurudi nyumbani.

"Tunaingia kwenye mshipa mkubwa hapa mguuni tunaelekea kwenye moyo tunakupiga operesheni, baada ya siku mbili unaelekea kwako una nda nyumbani," anatamka Dk. Mollel. 

Anafafanua kuwapo wagonjwa wengi waliokuwa wakipelekwa nchini India kutibiwa na fedha nyingi zilitumika, sasa hilo linafanyika nyumbani.

Kuhusu wagonjwa wa selimindu nchini, Rais Samia anatamka kuletwa teknolojia mpya ya kutibu ugonjwa huo, na ya kifafa na ufafanuzi wake:

"Leo pale Hospitali ya Kanda ya Rufani ya Benjamini Mkapa (Dodoma) tunachukua kitu kwenye mifupa kwa ndugu yako ambaye hana tatizo hilo, unapandikizwa unapona,” anaeleza.

Dk. Mollel anataja kuwapo waliozaliwa wana ‘vibiongo’, pia Rais Dk. Samia akaridhia kununua mashine maalumu, ambayo imetatua changamoto hiyo.

Eneo lingine analitaja ni kiwanda kipya cha kuzalisha mionzi tiba nchini, Tanzania ikiwa katika nchi tano pekee zilizo nazo Afrika, wakati huduma hiyo ya mionzi ilitoka nje ya nchi.

Vilevile, anafafanua hadi sasa, Tanzania ina uwezo wa kugundua ugonjwa wa kansa kabla ya miaka mitano, kutokana na kuwapo mashine za kisasa zilizowekezwa na Rais Dk. Samia.

Anasema teknolojia hizo sasa zimeshuka mpaka katika ngazi ya zahanati, hata kuwasaidia wahitaji wengi katika Taasisi ya Kansa ya Ocean Road

"Juzi tumeenda na Kamati ya Bunge (ya afya), asilimia 70 wamepatikana na hatua ya kwanza wanatibiwa na watapona," anabainisha Dk. Mollel

Anaeleza kwa miaka mitatu Shirika la Afya Duniani (WHO), lilitegemea wastani wa vifo vya kinamama mwakani kuwa 250 kati ya vizazi hai 100,000, lakini uwekezaji wake Rais Samia, fedha shilingi trilioni 6.6, zimeshusha wastani kutokanana  huduima muhimu sasa zimefika ngazi ya zahanati.