MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA... Magwiji dunia wakusanyika Dar kuumiza vichwa mapambano yake

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 09:59 AM May 02 2024
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, katika kongamano hilo.
Picha: Maktaba
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, katika kongamano hilo.

NCHI zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwamo Tanzania, zinatajwa kuwa na hatari kubwa ya watu wake kuugua Magonjwa Yasiyoambukiza (NCDs), huku Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema takriban vifo nusu milioni vinavyoepukika, hutokea kila mwaka, Kati ya vifo hivyo 100,000 husababishwa na magonjwa manne; kisukari aina ya kwanza; selimundu; mfumo wa hewa; magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo.

Tanzania imekuwa mwenyeji wa kongamano la kimataifa barani Afrika dhidi ya NCDs katika mradi ‘PEN Plus’ (Kifurushi cha Huduma Muhimu za Afya), kwa magonjwa hayo, lililoandaliwa na WHO, likikaribisha washiriki zaidi ya 300.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akifungua kongamano hilo lililoanza Aprili 23 hadi 25, mwaka huu, anasema: “Nchini, NCDs huchangia takriban asilimia 70 ya magonjwa mengine kama vile figo na moyo.

“Asilimia tisa ya Watanzania wanaugua kisukari huku asilimia 15 wanaugua presha. Lengo la dunia ni kufikia angalau theluthi moja kupunguza NCDs, 

“Asilimia 77 ya NCDs ipo katika nchi za uchumi kati na mdogo. Zipo hatua tunachukua kama nchi, kwa kuhimiza ufanyaji mazoezi, kutoa elimu kubadili mtindo wa maisha, kufanya vipimo na matibabu.” 

AFRICA CDC

Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Magonjwa na Kukinga kutoka Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Magonjwa Afrika (Africa CDC), Dk. Abdulaziz Mohammed, anaeleza:

“Afrika tunachangia masuala kadhaa na pakubwa katika NCDs, hakuna afya bila tiba ya NCDs. Unyanyapaa unatakiwa kuondolewa. Kuna watoto wanaugua kisukari aina ya kwanza. Hakuna huduma.

“Kwa kuunganisha juhudi, tutaweza kupambana na NCDs, tuachane na unyanyapaa. CDC tutaendelea kushirikiana na wadau dhidi ya NCDs Afrika.”

USHUHUDA WAKE

Akiushuhudia umma uliohudhuria kongamano hilo, Emmanuel Kisembo, mzaliwa wa Kampala, nchini Uganda, pia Meneja wa Programu katika taasisi ya Sonia Nabeta Foundation huko kwao, anasi simulizi ya namna aligundulika kuwa ana kisukari aina ya kwanza.

“Nasimama hapa nikiwawakilisha wenzangu, mimi mwenyewe, kwa watu ambao wanaishi na kisukari. Mtoto nayegundulika na kisukari aina ya kwanza, tumesikia mawasilisho hapa yakisema, watoto hawa hawawezi hata kushehereka siku ya yao ya kuzaliwa ya kwanza.

“Huu ndio uhalisia. Tuna wakilisha watu ambao hufa, bila hata kugunduliwa, kutokana na uhaba wa huduma za afya. Ninawakilisha watu ambao wana familia, ambao hutumia fedha za kwa ajili ya matibabu, ada duni, nawakilisha watoto ambao wanaugua na wanashindwa kwenda masomoni. 

“Tunahitaji fursa zaidi katika kuongeza wigo hali hii, wakati kwenye kongamano hili tukiwa nane, tunawawakilisha Waafrika wengi,” anasema Kisembo. 

Anasema kuna haja ya kutekeleza yanayopangwa na wadau mbalimbali, kwamba: “Nilifanikiwa kwenda shule, kuoa na kuwa na watoto. Hii si hadithi ya wengi waliopo huko duniani, tusirudi nyuma katika kuwafikia wengine.

“Watu wanaoishi na NCDs wanahitaji waishi miaka mingi, wakiwa na afya njema,” anaongeza Kisembo.

KUTOKA WHO  

Taasisi yake imejikita katika kupunguza gharama kubwa za matibabu kwa watoto wenye kipato cha chini wenye kisukari cha aina ya kwanza, barani Afrika.

Kisembo, ni miongoni mwa maelfu ya Waafrika, wanaoishi na kisukari aina hiyo. Anatoa elimu kwa njia tofauti. Ndiye mwandishi wa kitabu cha ‘Embracing the Pricks: The Journey to Acceptance through the Lens of an African Type 1 Diabetes Warrior.’

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), nchini, Dk. Charles Sagoe-Moses, anasema NCD's, husababisha mamilioni ya vifo kwa mwaka, ambayo vingeweza kuepuka, kutokana huduma duni kukabili magonjwa hayo.

“Takriban vifo 100,000 husababishwa na sababu nne; kisukari aina ya kwanza, selimundu, magonjwa ya mfumo wa hewa na moyo kwa watoto. 

“Katika nchi nyingi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, huduma za matibabu kwa NCD's hupatikana tu kwenye hospitali za rufani.

“Watu wengi na familia zao wanakumbana na gharama kubwa za matibabu haya au zile za usafiri kwenda na kurudi, kutoa huduma na kusababisha ulemavu ama vifo,” anasema Dk. Charles.

Kwenye nchi hizo, anasema watoto wakigundulika kuwa na kisukari aina ya kwanza, uwezekano kwa kuishi ni kwa kipindi cha chini ya mwaka mmoja, ikilinganishwa na nchi zilizoendelea ambao uwezekano ni hadi umri wa kati.

“Kila siku watoto wa Kiafrika 1000 wenye selimundu huzaliwa. Bila ya kuwa na hydroxyurea (moja ya tiba), ambayo ni tiba iliyodumu kwa takribani muongo mmoja, nusu ya watoto hawa watafariki kutokana na ugonjwa huu kabla ya kufikishwa miaka mitano.

“Asilimia 20 ya wenye umri wa miaka tisa kwenye nchi za uchumi chini ambaye pengine angepona kwa magonjwa ya mfumo wa hewa, atafariki akiwa na miaka sita,” anaeleza Dk. Charles.

Ongezeko la NCDs, mkuu huyo kutoka WHO, anasema inatia shaka, akifafanua kuna kitu kimeachwa kinapaswa kurejewa “Zamani magonjwa haya ilikuwa ni watu wazima.”

MTAFITI NCDs

Dk. Mary Mayige, Mtafiti Mkuu Mwandamizi katika NCDs kutoka Taasisi ya Taifa ya Tafiti za Magonjwa ya Binadamu (NIMR), amejikita katika kufanya tafiti za magonjwa hayo.

Anasema magonjwa yameongezeka zaidi kuanzia miaka ya 2000, kwa kuwa idadi ya wagonjwa inathibitika kwenye hospitali.

“Kuna mpango wa serikali uliandaliwa kuyadhibiti mwaka 2008 mwaka 2016 hadi 2020 na unaondelea ulianza 2021 hadi 2026,” anaeleza .

Kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa kongamano hilo la kwanza, ni kutokana na hatua zake za kudhibiti kama vile NCDs kuingizwa katika Mpango wa Tano wa Sekta ya Afya.

Aidha, mpango wa kudhibiti NCDs ukazinduliwa, ukitekelezwa kwa afua tofauti kwa kushirikiana na taasisi za umma na binafsi.

“Juhudi zinaendelea kufanyika ila kuna changamoto ya rasilimali; fedha, watu, miundombinu nikiri kuna juhudi, huduma za kibingwa, bobezi na wengi hufika nchini kutibiwa NCDs.

“Mradi huu unafanyika kwenye nchi 11 duniani na Tanzania imeonekana kufanya vizuri zaidi, ndio mkutano wa kwanza umefanyika Tanzania, ili waje kujifunza, tumewezaje kufika hadi vituo vya afya. 

“Tumeanzisha kliniki za wagonjwa NCDs na huduma za kibingwa katika wilaya mbili Karatu na Kondoa. Hadi sasa Kondoa kuna wagonjwa zaidi ya 93 na tumelenga kufikia hadi 400 kupitia mradi huu,

MAAZIMIO YALIYOPO

Akisoma maazimio yaliyofikiwa watekelezaji wa mradi huo kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya, Dk. Hamad Nyembea, anasema lengo ni kuongeza uwekezaji katika afya.

Kwamba maazimio ni bajeti ya asilimia 0.3 katika Sekta ya Afya duniani, ijikite kwenye NCDs katika nchi zinazoendelea, pia washirika wa mapambano wa magonjwa hayo kuongeza mafunzo, vifaa tiba katika maeneo ya kutoa huduma za afya.