Wakati dunia ilipokuwa ikijiandaa kwa Mkutano wa COP29 uliofanyika huko Baku, Azerbaijan, watoto wa Tanzania waliwasilisha ujumbe wa wazi uonaosema “mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi yanaanza na elimu.”
Taarifa ya Shirika la Kimataifa la Save the Children, inasema wawakilishi wa watoto wa Tanzania katika kusanyiko la mapema kabla ya mkutano huo walisisitiza umuhimu wa elimu ya mabadiliko ya tabianchi kujumuishwa katika ngazi zote za shule.
“Watoto wa Tanzania wanadai kufundishwa maarifa na stadi zitakazowalinda na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika hatua za kukabiliana na tabianchi,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo iliyopewa jina la ‘Children Climate Demand’, na kuongeza:
“Kwa kujumuisha elimu ya tabianchi katika mtaala, Tanzania inaweza kulea kizazi cha raia walio na maarifa, walio na ustahimilivu, na wenye kuchukua hatua.”
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF katika ripoti yake inyoitwa ‘Time to Act’ ikimaanina “wakati wa kuchukua hatua” (kwa tafsri isiyo rasmi) linasema mbadiliko ya tabianchi yanawaathiri watoto kwa kiasi kikubwa, yakidhoofisha haki zao za elimu, afya, na usalama.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nchini Tanzania, watoto wanakabiliwa na changamoto za elimu kukatizwa kutokana na majanga ya tabianchi kama mafuriko, hatari za kiafya zinazotokana na magonjwa ya majini, na ugumu wa kupata maji safi na chakula chenye lishe.
“Licha ya changamoto hizi, watoto hawapaswi kutazamwa kama tu, bali wanaweza kufanywa kuwa mawakala wa mabadiliko,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo na kuongeza:
“…dunia inapaswa kuwasikiliza vijana na watoto wa Tanzania na kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha maono yao ya mustakabali endelevu na wa usawa yanatimia.”
Shule ya Msingi Kawe A, iliyopo Halmashauri ya Wilaya Kinondoni, Dar es Salaam, imeonyesha njia kwa kuanza kuitikia sauti za watoto wa Tanzania kwa kuanzisha programu za kuwajengea uwezo wa kutunza mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi, wanafunzi wa shule hiyo.
Kupitia mradi unaofadhiliwa na Shirika lisilokua la kiserikali la WeWorld, shule hiyo imebuni mpango wa “Pamoja Tudumishe Elimu”unaowapatia watoto elimu ya vitendo ili waweze kukabiliana na changamoto za mazingira shuleni na nyumbani.
Kupitia Klabu ya Wakulima Chipukizi, watoto wamefundishwa kulima mboga kama mchicha, nyanya na maboga, kilimo hicho huchangia si tu lishe bora, bali pia huimarisha afya zao kwa kupunguza uwezekano wa kushambuliwa na magonjwa yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi kama pumu na saratani ya ngozi.
Shule hiyo tayari imepanda miti 60 kuzunguka maeneo ya shule, ili kupunguza ukame na kuhifadhi uoto wa asili. Lengo ni kupanda miti 50 zaidi, hasa ya matunda, ili kutoa kivuli na lishe bora kwa wanafunzi. Kupitia juhudi hizi, watoto wanajifunza umuhimu wa mazingira na jinsi ya kuyatunza.
Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Kawe ‘A’, Cuthbert Mfwangawo, anasema mabadiliko ya tabianchi yameathiri shule kwa njia mbalimbali, ikiwemo ukame unaosababishwa na uharibifu wa mazingira.
Chimbuko la madai
Chimbuko la mawazo ya watoto wa Tanzania katika mkutano wa COP29 ni mashauriano kuhusu mabadiliko ya tabianchi yaliyowashirikisha watoto na vijana balehe zaidi ya 1,200 katika mikoa ya Kigoma, Mbeya na Zanzibar, katika utafiti uliopewa jina la U-Report.
Utafiti huo uliratibiwa na Ofisi ya Tanzania ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) kwa kushishirikiana Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) na Wizara ya Maenedeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalum.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotokana na mashauriano hayo, asilimia 60 ya watoto na vijana hao walieleza wasiwasi wa ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu mabadiliko ya tabianchi mashuleni.
Matokeo ya utafiti huo yalijadiliwa katika kusanyiko la vijana zaidi ya 150 waliokutana jijini Dar es Salaam, Oktoba 2023 ambako vijana na watoto walishirikisha uzoefu wao wa maisha na changamoto walizokutana nazo kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Ripoti ya UNICEF ya ‘Time to Act’ inasisitiza kwamba watoto wanapaswa kuwa washiriki hai katika suluhisho za tabianchi, si wapokeaji wa misaada pekee. “Kujumuisha elimu ya mabadiliko ya tabianchi mashuleni kunaweza kuziba pengo la maarifa, kuhakikisha watoto wanaelewa dhana kama upandaji miti, usimamizi wa taka, na nishati endelevu,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Klabu za mazingira
Watoto pia wanapendekeza kuanzishwa kwa Klabu za shule zinazojihusisha na uhifadhi wa mazingira kwamba zinaweza kuwa ukwaa kwa wanafunzi kutekeleza wanachojifunza kupitia shughuli kama upandaji miti na usafi wa jamii.
“Nadhani tunahitaji msaada wa serikali kufundisha watu kuhusu upandaji miti na urejeshaji wa misitu. Ni muhimu kujifunza jinsi ya kupanda miti ili kupunguza madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi,” ripoti hiyo inamnukuu Shalimila (20) kutoka Kigoma.
Mwalimu Dannyce Innocent ambaye ni msimamizi wa Klabu ya Mazingira na Bustani katika Shule ya Msingi ya Kawe ‘A’ anasema kupitia elimu ya mabadiliko ya tabianchi, watoto wanajifunza mbinu za kulima wakati wa masika na wa jua kali, akiwapa maarifa ya kumwagilia bustani mara kwa mara na kulima matuta ili kuhifadhi maji.
“Hii inawasaidia kufahamu umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kuwa sehemu ya suluhisho dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,” anasema mwalimu Innocent na kuongeza kuwa watoto wanapenda kushiriki kazi za usafi wa mazingira, kufyeka na kutunza bustani. Hata hivyo, changamoto ni uwezo wa kuandaa miche bora ya matunda na kivuli.
Mwanafunzi Buruhan Salum ambaye ni mshiriki wa Klabu ya Wakulima Chipukizi, anasema kupitia mafunzo wanayopewa amefahamu umuhimu wa mazingira na jinsi ya kuyatunza. Anasema kwake ni hatua muhimu kufahamu uhusiano uliopo kati ya utunzaji mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa watoto.
Naye Esther Benjamin, kutoka Klabu ya Mazingira, anasisitiza kuwa shughuli kama kupanda miti na kulima bustani zinawapa watoto maarifa muhimu ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
KUJENGA AFYA, MAADILI
Sheria ya Mtoto ya Tanzania ya Mwaka 2009, kupitia kifungu cha 13, inalinda haki za watoto dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Sheria hiyo inasisitiza umuhimu wa kulinda maeneo ya makazi ya watoto dhidi ya majanga ya asili.
Tanzania imeridhia mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za mtoto wa mwaka 1989, ikifanya hivyo mwaka 1991. Mkataba huo unasisitiza haki ya mtoto kuishi katika mazingira salama na yenye afya. Haki hii inajumuisha kulindwa dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kama majanga ya asili, kuongezeka kwa joto, na ukosefu wa rasilimali za maji, hali ambazo zinaathiri maisha ya watoto.
Ripoti ya Shirika la Save the Children katika mkutano wa COP29 inasema kujumuisha elimu ya mabadiliko ya tabianchi katika mtaala kutakuwa na manufaa mengi ambayo ni pamoja na kuwajengea watoto uelewa kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye maisha yao na kujifunza jinsi ya kuhimili kwa ufanisi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, manufaa mengine ni kufundisha stadi za kijani na kujenga uwezo endelevu wa kutawaandaa watoto kuzikabili changamoto na kutambua fursa za baadaye na kuwezesha mabadiliko ya tabia kwa kuwaelimisha watoto kuacha michezo inayoathiri mazingira na kuhamasisha ushirikiano katika kukabihatua za pamoja.
Mwalimu Innocent anasema mboga wanazolima shuleni husaidia kujenga na kuimarisha kinga ya mwili. Pia, watoto wanajifunza maadili ya kijamii, kama kushirikiana, kuwajibika, na kuwa na nidhamu ya kutunza mazingira yao.
Kwa upande wake, Rehema Issa, anasema elimu ya utunzaji mazingira imeipata akiwa shuleni, na imemsaidia kufahamu mambo anayopaswa kuyafanya kukabiliana na mabadiliko ya tabinchi akiwa shuleni na nyumbani kwa kupanda miti na kufanya usafi wa mazingira.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED