Ulinzi wa misitu kwa kufuata mila na desturi za jamii, jadi

By Gaudensia Mngumi , Nipashe
Published at 09:53 AM Oct 01 2024
Misitu ya mikoko inayopunguza makali ya athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kukata kasi ya mawimbi ni rasilimali muhimu Pemba.
PICHA: MTANDAO
Misitu ya mikoko inayopunguza makali ya athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kukata kasi ya mawimbi ni rasilimali muhimu Pemba.

KUTUMIA mila na desturi kulinda misitu na hifadhi za maji ni jambo linalowezekana, ushuhuda ukitokea kisiwani Pemba. Ni ukweli kuwa siyo lazima wanajamii wafunzwe kutunza mazingira yao ni jambo walilolifanya tangu enzi.

Ni kweli misitu mingi ambayo wananchi wanailinda kwa njia za mila na desturi za jadi ina miti mingi, mikubwa na minene, ina maji ya chemchemu za asili tena mazingira yanayotamanika, anasema Samira Juma, Ofisa Mkuu Misitu Pemba.

Anapozungumza na Nipashe kwenye makala hii anasema elimu ya kutunza mazingira ni muhimu na matumizi ya mila na desturi kuyalinda ni jambo dhahiri na linaloendelea.

Anasema mila na imani za watu Pemba, zimejengeka kwamba ukiharibu maeneo ya misitu na hifadhi zinazoheshimiwa na jamii kwa matumizi ya kijadi kama matambiko na dua utadhurika kwa namna yoyote ile.

 “Utapigwa bakora, utaumwa, utakufa, utapotea, kitatanishi au kuondoka bila kujijua. Hivyo mila hizi  zimerithishwa  kizazi hadi kizazi na anayekua anajua eneo la msitu fulani haitakiwi kuharibika kwani kuna mapango ambayo hutumiwa kutambika.

Wengine wanatambika kila mwaka na wapo wanaofanya matambiko kwa siku maalum na wote huenda huko kuomba mahitaji kama kuombea wagonjwa, maisha bora na mafanikio,” anaongeza  Samira.

Anaitaja misitu hiyo kuwa ni pamoja na ile ya Kisiwa Pembe, kilichoko Shehia ya Mtambwe Kusini, kuna msitu mkubwa ambao unatumiwa kufanya mila za kijadi.

 Samira anasema hairuhusiwi mwanamke kwenda huko wala yeyote na  inapofika  saa 6:00  mchana kila aliye ndani anatakiwa uondoke kisiwani mara moja. 

Anaongeza kuwa usipofuata masharti hayo unaweza kudhurika na hata sasa msitu uko salama.

Katika Shehia ya Kiuyu kuna msitu ambao ndani yake kuna mapanga ambayo yanatumiwa na wanajamii wa maeneo hayo kijadi.

 “Hairuhusiwi kwa mgeni yeyote kwenda peke yake ni lazima afuatane na mwenyeji kuepusha uharibifu wa eneo hilo.” Anaongeza Ofisa Misitu Mkuu.

Ukienda kinyume na ukafanya uharibifu wowote utadhurika na hata sasa misitu imehifadhika, anaongeza, Samira. 

Anataja msitu wa mikoko wa Kwa Mwanawembe ulioko shehia ya Kiungoni,  akisema ni sharti kwenda na mwenyeji ili kuingia na kwamba  mgeni akienda peke yake atapotea lengo la kutaka awepo msindikizaji ni kuepusha uharibifu.

Anataja mingine kama  misitu ya Matumbini Mwavi Mweusi, kwa Nyundo na kwa Goa Mdiba  ambayo iko kisiwa cha Panza kuwa ni minene na miti mikubwa na wananchi wanafahamu kuwa ukienda kichwakichwa unadhurika iwe kuumwa ama kupigwa na watu usiowaona.

Kisiwa N’gombe kilichoko kwenye shehia ya Shumba Mjini anakitaja kuwa kina  msitu mnene na kinatumiwa kijadi na kimetunzwa kwa sababu ya kuamini na kuheshimu mila na desturi hasa kudhibiti wasiofahamika kuingia kiholela. Anasema  mgeni haruhusiwi kwenda peke yake.

Ipo misitu mingi kama ile ya Kisiwa Mbale, Michi

Zimwi, Kwa Konondo na maeneo ya makaburini kote kumehifadhika. Misitu ni minene na imehifadhika kwa taratibu za kimilia . Yakiwa ni maeneo ya kutambika na kuzika jamaa.

FAIDA KIJAMII

“Faida za kutumia mila na desturi ni pamoja na kuleta msukumo katika kulinda na kuhifadhi misitu Pemba na kupata mahitaji ya kijamii kwa urahisi. Wanavuna matunda asilia, mboga, asali, uyoga na dawa. ”

Faida nyingine ni kuongeza kipato kwa jamii hasa zinazofuga nyuki kibiashara kwa mfano msitu wa Kiungoni, anasema.

Kubwa jingine Samira anasema ni kuhifadhi vianzio vya maji na chemchem za asili, hasa kwa sababu eneo ni kisiwa na mawimbi ya bahari yanasogea.

“Kuna jingine muhimu ni kuimarisha haiba ya kijani ya kisiwa cha Pemba. Tena kuzuia uharibifu wa visiwa kwani maeneo mengi yamo ndani ya visiwa vidogo vidogo,” anasema Samira.

Anasema misitu inaimarisha hali ya hewa na kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi, inazuia  pepo za bahari kuingia kwa kasi kubwa katika maeneo ya makazi na mashamba.

“Kwenye misitu ya mikoko ni muhimu inazuia mawimbi ya bahari kuathiri mashamba na makazi. Pia inahifadhi viumbe hai wakiwamo wanyama na ndege, wanaohifadhiwa  baharini.”

USHIRIKI WA SERIKALI

Samira anasema Zanzibar Forest Project, inashirikiana wanajamii kulinda na kuhifadhi maeneo hayo, wakifanya juhudi mbalimbali.

“Mosi tumeanzisha kamati shirikishi za uhifadhi wa misitu ya jamii. Tunashirikiana na kamati hizo kuhifadhi maeneo hayo ambayo yana misitu ya ardhini na mikoko ufukweni.”

Aidha, anasema wameanzisha Community Forest Management Agreement (COFMA), ni makubaliano ya usimamizi shirikishi wa misitu baina ya Idara ya Misitu na shehia.

Anasema wanajamii wanatenga maeneo yao kwa mujibu wa matumizi yao na wanatunga sheria ndogo ndogo za kusimamia maeneo hayo ikiwa na pamoja na kugawa misitu kwa matumizi maalum. Anasema yeyote anayevunja sheria hizo adhabu na faini zimeainishwa kwa kila kosa na anaadhibiwa kwa mujibu wa sheria hizo.

Anasema ikishindikana anapelekwa Idara ya Misitu na anaadhibiwa kwa mujibu wa sheria za misitu.

Hata hivyo, anataja changamoto mojawapo kuwa ni baadhi ya maeneo kuwa na ubaguzi kijinsia kwa vile wanawake pekee ndiyo hawaruhusiwi kwenda hivyo wanakosa mahitaji muhimu katika misitu hiyo. 

Kwa ujumla anazipongeza jamii, akisema kuwa hata sasa mila na desturi hizo zinaendelea kutumika  maeneo mengi na misitu  imehifadhika bila ya kutumia nguvu wala gharama. 

“Wananchi wa maeneo hayo wanaheshimu mila na desturi zao kutokana na imani na kwa upande wa Idara ya Misitu inashukuru kwa kutumia mila na desturi hizo kwani misitu inaendele kuhifadhika na ridhaa na juhudi za wananchi wenyewe.” Anasema Samira.