WAKATI serikali ikiendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ikilenga asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati hiyo mpya kama Rais alivyoagiza, wadau katika kikundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni, Dar es Salaam wameanza mchakamchaka kuitikia kwa namna yao.
Hilo wanalifanya wakiwafundisha majumbani wanawake wajasiriamali wenye ulemavu, namna ya kutengeneza mkaa mbadala wakitumia taka mbalimbali, zikiwamo zinazoweza kuloanishwa na maji.
Kurejea mzizi wa utekelezaji huo, mnamo Oktoba 5 mwaka jana, aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, akafafanua kuwa, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameibeba kwa dhati ajenda ya matumizi ya nishati mbadala kutokana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.
Katika kauli yake hiyo mkoani Ruvuma, sanjari na ugawaji majiko, mitungi ya gesi iliyotolewa na serikali, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Naibu Waziri akafafanua:
“Ninyi nyote mnafahamu ajenda ya Mheshimiwa Rais kuhusiana na umuhimu wa nishati mbadala. Tunafahamu changamoto ya mabadiliko ya tabianchi na changamoto za mazingira kwa ujumla.
‘Hii ni ajenda ambayo Rais ameibeba kwa dhati kabisa, kuhakikisha tunaanza mchakato wa kuelimisha Watanzania, ili kuondokana na nishati ambazo sio rafiki kwa mazingira na kutumia zilizo rafiki kwa mazingira,”.
Tamko hilo la Naibu Waziri Kapinga, ni mwendelezo wa kilichojiri mwaka mmoja kabla, Novemba 2022, Rais Dk. Samia, aliposhiriki ‘mjadala wa kitaifa kutafuta suluhu ya nishati safi ya kupikia,’ aliyoitafsiri kuwa “hatua ya kwanza kuelekea suluhisho ni Watanzania wenyewe kubadilisha mtazamo wao.”
Taarifa zilizotolewa katika mjadala huo, ni kwamba Watanzania wanatumia nishati safi walikuwa asilimia tano pekee, waliobaki wakizama katika kuni na mkaa, hali iliyotajwa chanzo cha vifo takribani 33,000 kila mwaka nchini.
Akizungumza wakati akizindua mjadala huo wa kitaifa wa siku mbili, Rais Dk. Samia, ambaye ni mdau wa kutetea mazingira kitaifa, akanena hatua ya kwanza kupambana na matumizi ya kuni na mkaa, ni kwa Watanzania wenyewe kubadili mitazamo.
Rais Samia akafafanua kwamba matumizi ya kuni na mkaa ni suala mtambuka nchini; chanzo cha ukame unaosababisha uhaba wa maji, magonjwa na kusababisha unyanyasaji kijinsia katika jamii.
INAVYOTEKELEZWA KIPUNGUNI
Mkurugenzi wa kikundi, Seleman, Bishagazi, anasema lengo lao ni kuwafundisha wanawake hao kutengeneza mkaa huo ili iwapunguzie ukali wa maisha katika bajeti ya mkaa uliozoeleka.
Bishangazi anasema, wameanza na wanawake wa maeneo jirani ya Kivule na Majohe wilayani Ilala, wakilenga kufikishia elimu kwa kaya zaidi ya 200, zihamie katika mkaa mbadala.
Anafafanua; “Pia, wapo wanawake na wasichana wanaotumia zaidi ya saa sita kutafuta nishati ya kupikia. Kwa hiyo, tukiwafundisha kutengeneza mkaa mbadala kwa kutumia taka zinazotokana katika maeneo yao, ukataji hovyo wa miti na uchomaji utapungua sana.”
Hadi sasa, asilimia kubwa ya Watanzania wanategemea kilimo cha mvua au maji na kadri wanavyoendelea kukata miti, uwezekano wa kupata maji ya kutosha unabaki mdogo, mkombozi dhidi ya magumu hayo ni kutumia nishati mbadala na rafiki kwa mazingira, unaookoa mengi.
“Tunawafundisha teknolojia hii waione kwamba ni fursa, lakini wakati huohuo tunalinda mazingira na kuokoa misitu yetu kwa faida ya vizazi na vizazi na kuepusha magonjwa yanayotokana na matumizi ya mkaa ule.”
Anasema kwamba, mafunzo ya kutengeneza nishati hiyo ya mkaa mbadala wamepewa na Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), ikiwa ji matokeo ya teknolojia mpya inayokinzana na ukataji miti hololela.
WALENGA NA YAO
Dorice Alfred ni mjasiriamali kutoka Kata ya Kivule, wilayani Ilala, anaeleza alivyonufaika katika ujasiriamali wake wa kupika uji na vitafunwa, mafunzo yamemsaidia pia kutunza fedha, tangu ajifunze kutengeneza mkaa unaotokana na taka, umeachana na mkaa wa miti.
“Mwanzoni nilikuwa natumia Sh.60,000 kwa mwezi kwa ajili ya kununulia mkaa wa kawaida, kila siku nilikuwa nanunua wa Sh.2000, lakini tangu nimejifunza na kuanza kutengeneza mwenyewe nimeokoa kiasi hicho cha fedha,” anasema Dorice.
Anasema amejifunza kutengeneza mkaa wa aina mbili; wa taka zitokanazo na boksi, karatasi na mabaki ya baadhi ya vyakula.
Mjasiriamali Seya Khasad, anasema hakufahamu kama taka hizo ni fursa za kupatamkaa mbadala, akijieleza kuwa: “Mimi ni mama mjane na nyumbani ninaishi na familia kubwa wakiwamo wajukuu.
“Nilikuwa nateseka sana, unaweza kununua mkaa lakini usitoshe kupikia vitu vyote, inabidi ukanunue mwingine na kuna wakati ninashindwa!”
Anaeleza kuwa elimu aliyo nayo imekuwa fursa, anayoifafanua kwamba,; “Mkaa mbadala umetusaidia, yaani ukiona karatasi unaokota, watoto daftari wametupa, sijui uchafu gani unaokota unatengeneza mkaa! Yaani hii teknolojia imetusaidia sana, unajikuta unatengeneza mkaa wa kutosha na hauhangaiki tena.’
NISHATI INAVYOUMBWA
Mkufunzi wa Teknolojia hiyo ya mkaa mbadala, kutoka asasi ya Sauti ya Jamii, Kipunguni, Tausi Msangi, anaeleza mkaa huo unatokana na taka tofauti, ukinufaisha uwekaji mazingira safi, huku ikipunguza ukataji miti ovyo uchomaji mkaa misituni.
Anaitaja kuwa teknolojia isiyohitaji mtaji mkubwa na kazi hiyo inaweza kufanyika majumbani, ubunifu ulioasisiwa ughaibuni miaka kadhaa iliyopita, akiitaja nchi jirani Kenya imeanza kuitumia mapema.
Tausi anataja malighafi yanayaohitajika katika kutengeneza mkaa mbadala, ni pamoja na vumbi la mkaa wa kawaida linalopatikana maeneo yao ya biashara.
“Unaweza kulipata bure au kulinunua kwa gharama ndogo halafu ukatumia gundi ya udongo unaonatanata kama ule ambao unatumika kutengenezea tofali za kuchoma na vyungu, unaweza pia kutumia uji wa muhogo kutengeneza mkaa huo,” anaeleza Tausi.
Malighafi mengine anayataja ni maganda ya machungwa yaliyokatwa vipande vidogo, yanakaushwa na kulowekwa maji kwa muda wa siku mbili au tatu.
“Kwa mfano, unaweza kuchukua vumbi lako la mkaa ambalo halina mabonge na kama yapo unatafuta mfuko ukaweka ndani halafu, ukatwanga mpaka yalainike kabisa, ukachekecha kuondoa mabonge ambayo yamebakia,” anasema.
“Tunachokihitaji hapa ni ule ungaunga ‘mlaini’ peke yake, kisha uweke kwenye chombo kama vile beseni au ndoo,” anaeleza na kuongeza:
“Baada ya hapo unatakiwa uchukue udongo mkavu ambao uko katika hali ya ungaunga, kama una mabonge utwange mpaka ulainike, kisha uchanganyie katika lile vumbi la mkaa mpaka vumbi la mkaa na udongo vichanganyike kabisa.
“Weka gundi katika huo mchanganyiko au ongeza maji ikiwa udongo umetumika kama gundi, halafu changanya hadi uridhike vyote kwamba vimechanganyikana vizuri.”
Tausi anaeleza baada ya kuvichanganya, huzalisha mkaa, anaoufafanua: “Unaweza kutumia mkono kwa kutengeneza muundo unaoupenda kama vile vitonge.
‘Wakati wa kutengeneza muundo huo, hakikisha unabinya kwa nguvu ili ziwe ngumu kwani kadri unavyokuwa mgumu ndivyo itakavyotengeneza mkaa mzuri zaidi.”
Anasema baada ya mtu kutengeneza muundo unaoutaka kulingana na jiko lake, hatua nyingine inaanikwa juani wastani wa siku mbili au tatu, ikauke tayari kwa matumizi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED