Stendi, gereji, foleni barabarani, ndani ya lori

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:20 AM Jan 28 2025
Kufanya shughuli pembeni ya barabara zenye foleni ni chanzo cha upofu
Picha: Mtandao
Kufanya shughuli pembeni ya barabara zenye foleni ni chanzo cha upofu

WAKAZI mijini karibu na barabara zenye foleni, wanaokaa vituo vya mabasi kupiga debe na wanaofanyakazi kwenye gereji jueni kuwa yajayo yatawasikitisha.

Ni kwa sababu moshi wa dizeli unaotoka kwenye injini unasababisha upofu na huenda ukikaa kwa muda mrefu utakuwa kipofu kutokana na wingi wa moshi huo, unaoathiri hata madereva pia.

Utafiti na ripoti kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), unasema kuwa moshi wa injini za magari unahusishwa na hatari kubwa ya kuongeza upofu.

Hali ya kupoteza kwa kiasi kikubwa uwezo wa jicho wa kuona, unatokana na vichafuzi vya hewa kama vile chembe chembe na gesi ya  ‘naitrojen dayoksaidi’  inayopatikana katika moshi huo wa injini.

Kwa hiyo kwa wakazi wa miji na majiji mengi ya Tanzania ambako foleni ni jambo la kawaida, au kufanya kazi katika maeneo yaliyo na moshi mwingi wa magari kama vituo vya mabasi au barabara zenye msongamano  kuna hatari maradufu ya kuwa kipofu uzeeni au baada ya miaka 50.

Pamoja na hayo, kufanyabiashara kwenye vituo vya mabasi na watoto mgongoni au kuwatandikia chini wacheze au kulala hakuwaachi salama.

Ni jambo la kuepuka kwa sababu ya kumharakishia mtoto upofu.

WHO inasema ni kwa sababu moshi wa magari huharibu retina na mishipa ya kuona ambayo  ni  sehemu ya jicho inayowezesha binadamu kuona.

Retina na ‘optic nerve’ ndizo zinazoathirika moja kwa moja kutokana na moshi wa dizeli, utafiti huo ukieleza kuwa hata kuwa au kufanyakazi kando ya barabara si salama.

Baadhi ya barabara zenye foleni kama za Mandela, Morogoro, kituo cha mabasi cha Magufuli na vituo vingine kama Mbezi, Mbagala, Makumbusho vyote vya   Dar  es Salaam, si sehemu salama kuna  hatari ya upofu.

Tatizo la macho linaanza kuwanyemelea kuanzia miaka 45 na kuendelea.

Kwa upande wa Iringa kipande cha kutoka Mahenga hadi Ilula nacho kuna foleni inayosababishwa na Mlima Kitonga, wasafiri na wasafirishaji wakielezwa kuwa wanakaa kwenye foleni hata zaidi ya saa tatu.

Moshi wa magari huchangia kwa kiwango kikubwa kwa ugonjwa unaofahamika kama Age-Related Macular Degeneration (AMD) ambao husababisha watu wa kuanzia miaka 45 kupoteza uwezo wa kuona, inasema WHO.

Wakazi wa mijini wanaofanya mazoezi pembeni ya barabara hawako salama wanaambiwa  kuwa wanajiletea shida ya macho kiasi miaka inavyokwenda.

Ugonjwa wa upofu uzeeni awali ulihusishwa na kuvuta sigara lakini pia unaweza kuwa sawa na moshi  wa  magari ambao una madhara sawa na sigara kwenye kudhuru macho.

Moshi unaotolewa na magari umejaa  ‘kaboni monooksaidi, naitrojeni oksaidi’ na kemikali nyinginezo zilizoko kwenye dizeli na petroli ambazo zinahusishwa na kusababisha maradhi mbalimbali pamoja na saratani.

WHO inakadiria kuwa moshi wa magari huchangia zaidi ya asilimia 25 ya saratani  ya mapafu na magonjwa mengine ikiwamo  pumu au asthma.

Kwa mujibu wa mtandao wa ‘American Cancer Society,’ katika tafiti za seli zinazofanyika maabara, moshi wa dizeli , pamoja na  masizi na kemikali nyingine unasababisha mabadiliko katika nasaba za viumbe hai (DNA) za seli.

Kubadilisha utaratibu wa chembe hai na kuanzisha   saratani mwilini kwani udhaifu wa seli au DNA huchochea mwili kuwa kinyume na utaratibu wake asilia.

DNA inapovurugwa husababisha chembe zenye saratani  kukua, ingawa sio vitu vyote vinavyosababisha mabadiliko ya DNA pia husababisha saratani.

Tafiti kadhaa zinagundua kuwa kuvuta kwa muda mrefu moshi mzito wa dizeli kunaweza kusababisha saratani ya mapafu kwa wanyama wa maabara kama  panya, hivyo hali hiyo hutokea kwa binadamu.

Aidha, tafiti kadhaa zimegundua kuwa kuna uhusiano kati ya  moshi wa dizeli na saratani nyingine, ikiwa ni pamoja na kansa ya kibofu cha mkojo.

Nyingine ni ya ‘larynx’ au sanduku la sauti koromeo, tumbo na kongosho. Uchunguzi pia umehusisha saratani ya mfumo wa damu kama vile ‘lymphomas na lukemia’ pamoja na lukemia kwa watoto kuwa chanzo ni moshi wa dizeli.

Kwa mtaji huo sekta ya usafiri huchangia asilimia kubwa ya  vifo vyote vinavyotokana na hewa chafu ya dizeli.

Pamoja na changamoto hiyo Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP),  linaeleza kuwa, kuvuta  mara kwa mara hewa chafu au moshi wa injini za magari zinazotumia dizeli kuna uwezekano wa kuugua maradhi ya kusahau au ‘dimensia’.

Ni wazi kuwa kama juhudi hazitafanyika na kubadilisha injini ili zitumie nishati safi kuna uwezekano madhara yanayosababishwa na moshi wa magari  kuongezeka maradufu kwa muda mfupi.

UNEP inasema ni kwa sababu ununuzi wa magari ni mkubwa na hata yale yaliyotumiwa kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Mataifa yanayoendelea ya Afrika usajili wa magari ni mkubwa kwa sababu watu hununua magari kila uchao. 

Lakini magari yanayonunuliwa kila siku na uchache au uhaba wa miundombinu umesababisha foleni barabarani na kuathiri afya za watu na hali ya hewa angani kwa sababu inaongeza joto zaidi.

Wakati umefika wa sheria kuelekeza polisi kuondoa magari ya usafiri wa umma, malori ya shehena na hata ya watu binafsi yanayotoka moshi ili kuwanusu watu na janga la moshi wa dizeli.