Mwanadada aeleza chungu, tamu safari ya ukombozi wa mwanamke wa Kimaasai

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 08:30 AM Oct 23 2024

Rose Njilo mwanaharakati na mpigania haki za wanawake wa jamii ya Kimasai.
PICHA: ELIZABETH ZAYA
Rose Njilo mwanaharakati na mpigania haki za wanawake wa jamii ya Kimasai.

MWAKA 1984 katika Kijiji cha Arash wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, anazaliwa Rose Njilo, mwanamama shujaa mtetezi wa haki za wanawake katika jamii zinazodumisha mifumo kandamizi.

Ni mwasisi na mkurugenzi wa asasi ya kirai ya Mimutie Women Organization (WMO), iliyoundwa 2012 wilayani Ngorongoro, akilenga iwe sauti ya kutetea haki za wanawake na watoto wanaoishi kwenye jamii za pembezoni.

Rose, anataja mlolongo wa misukosuko ya ukatili wa kijinsia aliopitia, akigusia ndoa ya utotoni, alipoozwa na miaka 12, akiuita mwanzo wa machungu kwenye maisha yake. Jasiri huyo alijinasua licha ya kukutana na milima mirefu kufikia ukombozi, hakukata tamaa, aliendelea kupambana mpaka akajiokoa licha ya kwamba tayari alikuwa ameshapata watoto katika ndoa hiyo chungu.

Baada ya kujiokoa na ukatili, ukandamizaji, unyanyasaji na vipigo alivyokuwa akipitia aliona haitoshi, alitafuta njia nyingine ya kurudi tena kwenye jamii kuwanusuru wanawake wenzake waliokuwa wakipitia madhila kama yake.

Kabla ya kufika kwenye simulizi ya namna ya alivyojiokoa yeye na wengine, Rose anasimulia machungu aliyokutana nayo baada ya kuozeshwa katika umri huo wa miaka 12 na mwanaume asiyemfahamu, namna mila ya Kimaasai inavyomweka mwanamke kando, ikimwona asiye na msaada na laana katika jamii hiyo, asiyepewa nafasi katika jambo lolote liwe la nje au ndani ya jamii yake.

Katika simulizi yake kwa mwandishi wa Nipashe, anasema  siku aliyoozeshwa ndio ilikuwa ya kwanza kukutanishwa na mwanaume huyo, na kwa sababu ya umri, aliamini kwamba huenda baada ya kutambulishwa  angerejeshwa tena nyumbani kuishi na wazazi wake mpaka atakapofikia umri mkubwa zaidi.

 ALIVYOOZESHWA

“Nilikutana na changamoto ya kuozeshwa na miaka 12, nilikatishwa masomo nikiwa darasa la tano miongoni mwa wasichana wachache sana wa jamii yangu waliopata bahati ya kuandikishwa shule. Nilipelekwa kwa mume nikiwa sielewi chochote na sikujua napelekwa wapi, wala sikuwahi kukutanishwa na huyo mwanamume hapo kabla. Kwa utoto niliokuwa nao nilijua wakinipeleka wananirudisha tena nyumbani, tena mwanaume huyo nikimwangalia ni mzee.”

“Nikawa naangalia mbona jua linazidi kukomaa na sirudishwi nyumbani, maana niliamini watanirudisha baadaye lakini ikafika mpaka usiku siku ikaisha. Siku ya pili kulikuwa na sherehe jirani na pale nilipopelekwa, nikawaona watu wa kwetu, nikatumia hiyo fursa kukimbia, lakini walinikimbiza wakanikamata na kunirudisha tena kwa huyo mwanaume.”

Rose anasimulia kwamba baada ya hapo hakuwa na namna nyingine ya kutoroka kwa kuwa kila alipojaribu kutoroka alikosa msaada kwa jamii iliyomzunguka hata kwa ndugu zake wa karibu, hivyo aliendelea kuishi maisha yenye maumivu kila siku.

“Niliishi kama niko kuzimu na nikiwa nimetengwa kwa sababu sina pa kwenda, na jamii yote iliyonizunguka inakubaliana na hiyo hali, hata kama unaonekana uko kwenye hatari ya kufa haikusaidii, kwa hiyo nikaishi kwa miaka 10 na nikazaa watoto wanne, nikiishi maisha ya uchungu na sikuwahi kufurahi katika kipindi hicho chote. Niliteseka mno sababu mazingira niliyokuwa nayo nilikuwa mdogo kwa hiyo hata majukumu mengine yalikuwa yananishinda.” Anasema. 

Aidha, walipompeleka kwa mume hawakutambua kama ni mtoto, waliona ni mke, kwa hiyo ni mtu mzima hata aliposhindwa kufanya majukumu mengine aliyopewa walihesabu ni kiburi. Lakini wakati huo akawa anapitia ukatili wa aina nyingi ikiwamo vipigo, wakati mwingine mumewe kumvua nguo mbele ya watoto wake, kwa hiyo alipomwona anarudi nyumbani alikuwa anatetemeka.

Anasema, kuna kipindi  akilala anaona kama kifo kinakuja, alikuwa anatoka nje na kukimbia, wakati mwingine akisikia jina lake limetajwa anashtuka na kwamba alifika wakati akikaa mahali, anakuwa haelewi kama jua limechomoza au limetua, akiathirika kisaikolojia kiasi kwamba hata akikutana na mtu analia, anakimbia asionane na watu na akienda mahali alitembea porini  si barabarani ili asikutane na yeyote.

Kadhalika, anasema baada ya vipigo na manyanyaso kuzidi, mama jirani yake alimuonea huruma na akamuahidi kumpa nauli  atoroke aende mbali.

“Alipoona mume wangu hayupo, aliniita, akanishauri niende mahakamani au kwa mwenyekiti wa kijiji nikamshtaki, lakini sikukubali kwa sababu niliamini sitapata msaada, huenda itaongeza zaidi tatizo nikiamini wote ni wale wale wa jamii ya Kimasai, akanipa nauli nitoroke.”

Anaongeza: “Lakini niliporudi nyumbani nikajifikiria, nikaenda kwa mwenyekiti wa kijiji, baada ya kumweleza kila kitu hakuamini na akaniambia natakiwa kuvumilia…nilienda mara nyingi mwishowe nikaona bora nitoroke, nikamfuata tena yule mama aliyesema atanipa nauli akanisaidia, nikaenda kuwaacha watoto kwa ndugu zangu nikaondoka.”

Rose Njilo akizungumza na mwandishi Elizabeth Zaya. PICHA: MWANDISHI WETU
KUPATA TALAKA

Rose anasema muda kidogo baada ya kutoroka, alipata taarifa kwamba mumewe amekuwa akiwafuata wanawe huko alikowaacha na kuwatesa, kwa hiyo ilibidi arudi kuwaokoa kwa kufuata taratibu za kisheria.

“Nililazimika kurudi tena nyumbani wakati huo hata kule nilikotorokea maisha yalikuwa bado ni magumu kwa sababu sikuwa na kazi ya kufanya, niliishi kwa rafiki yangu wa kike aliyekuwa ananisaidia, lakini nilirudi hivyo hivyo kudai watoto kwa mume wangu, nilikwenda mahakamani, nikaelezea mateso wanayopata, nikatendewa haki, tukatalikiana na nikapewa watoto wangu licha ya danadana nyingi kwa sababu alikuwa anatoa hongo sana,” anasema Rose.

 

KUANZISHA SHIRIKA

Anasema licha ya kuachana na mume,  mawazo ya kunyanyasika aliyokuwa anapitia yaliendelea kumtesa na wakati akiwa katika hali hiyo, alipata wazo la kuanzisha taasisi ambayo itakuwa sauti ya wanaopitia madhila kama yake, aliunda shirika licha ya kuwa  hakuwa na elimu wala kipato cha kumsaidia.

 “Kwa hiyo mwaka 2012 nikaanzisha taasisi yangu, lakini hata hivyo elimu pamoja na lugha ya Kiingereza ilikuwa  kikwazo tena kwa maana kwa mara ya kwanza nilikutana na mfadhili wa kunisaidia alikuwa ni Mzungu na alikuwa hajui Kiswahili, hata nilipotumia wale watafsiri wa lugha niliona kama kuna vitu hawamwambii ukweli kwa hiyo nikapata changamoto ya kujifunza Kiingereza.

“Nikatoka hapo nikamtafuta mzee mmoja kumwelezea ninachotaka kukifanya,  akanishangaa nitawezaje wakati sijasoma, lakini baadaye akanisaidia namna ya kuandika katiba na kusajili, na ikabidi nisome pia Kiingereza, nikasoma na kompyuta na ndipo nikaanza rasmi safari ya kupambania maisha ya wanawake wenzangu wanaopitia unyanyasaji na ukatili kama mimi, nikilenga zaidi jamii ya kimaasai.

Anasimulia kwamba hata baada ya kuanzisha taasisi yake hiyo mwanzoni hali haikuwa nzuri na kwamba alitumia fedha hata aliyopewa na ndugu au rafiki yake kama ya kujikimu, akiitumia kwenda kusaidia watu wanaopitia ukatili.

KULETA MAPINDUZI 

Rose nasema mara ya kwanza kupata ufadhili ilikuwa mwaka 2017 na ndio mwaka alianza kwenda Ngorongoro kutoa elimu ya kupambana na ukatili wanaofanyiwa mabinti na wanawake akiwaelimisha watambue umuhimu wa elimu pamoja na kumthamini mtoto wa kike na mwanamke kama alivyo mwanaume.

Anasema haikuwa rahisi kwa sababu wengi wanaamini haiwezekani mwanamke kama yeye hasa ambaye jamii inamfahamu kila kitu alichopitia, kubadilisha mila na tamaduni ambazo zimeheshimiwa miaka yote halafu atokee na kutaka kuzibadilisha kirahisi.

“Niliona nianzie kwenye jamii yangu kwa sababu wenyewe wanaamini na waliendelea kushikilia msimamo wao kwamba mtoto wa  kike katika jamii ya kimasai hahesabiki kama binadamu wengine, ni laana na hahesabiwi haki yoyote, na ukizaliwa wa kike unahesabiwa kama wa kuuzwa, yaani  ni wa kubadilishwa na kupata mali ikiwamo mifugo kwa familia.

“Kwa maana hiyo, mila hizo ziliendelea kuumiza watoto wa kike, kudidimiza haki zao lakini pia kuwaweka katika mazingira magumu na hatarishi kama ilivyotokea kwangu, ukatili wa mtoto wa kike ulikuwa ukianzia siku ya kwanza tu mama anapojifungua, kwa sababu kama kuna watoto wawili wamezaliwa, yule aliyejifungua wa kike hawezi kupewa huduma sawa na yule aliyejifungua wa kiume, kulikuwa na ubaguzi mkubwa. Kwa hiyo nilipopata fursa hiyo nikasema lazima nipambane kubadilisha hili, niokoe watoto wa kike katika jamii yangu wanaoendelea kuangamia.

 “Na hata mtoto wa kike alikuwa akifanya kosa hata kwa bahati mbaya, anayeadhibiwa ni mama yake kwa sababu walikuwa wanaamini kwamba ni ujinga wa mama yake. Kwa hiyo sikukubali, niliingia mzima mzima kwa hasira kama simba aliyechokozwa  bila kujali nitakutana na misukosuko gani, sikujihurumia kwa sababu tayari kama ni ukatili nilikuwa nimepitia vya kutosha mpaka nikafikia hatua ya kujikatia tamaa kwamba mimi ni wa kufa tu. 

KUZUILIWA KUTOA ELIMU

Rose anasimulia kwamba walivyomwona amerudi tena kwenye jamii yake na kuanza kutoa elimu kuhusu kuachana na mila hizo kandamizi, alianza kuchukiwa hadi na viongozi wa serikali za vijiji wakimfukuza aondoke kwa kuwa elimu anayotoa inawapotosha wanawake kuzikana tamaduni zao ambazo zilianzishwa tangu vizazi.

“Kwa hiyo hali ilikuwa ni mbaya kila mtu alikuwa ananichukia, wakaanza na kunibatiza majina mabaya, mara ohh ni malaya, nimeachana na mume wangu, nimekengeuka mila na tamaduni za jamii yangu, kwa hiyo niondoke nisiwaharibu wanawake wengine…jamii yote ya kimaasai ikawa inaniona mimi ni mbaya na ni adui yao. Na wakati huo wazazi wangu walikuwa wamefariki, kwa hiyo sikuwa na mtu yeyote wa kunitetea.

Rose anasema ndugu zake wakiwamo dada zake walikuwa wanashindwa wafanye nini bdala yake walibaki kuumia na kuteseka kwa namna jamii inavyomuona na kumchukulia.

“Lakini kwa yale madhila niliyopitia yalinijengea ujasiri mkubwa sana ambao pamoja na vita kubwa niliyokuwa nikipitia kutoka jamii ile niliendelea kuwa na nguvu ya kupambana. Siku moja ilifikia hatua Mwenyekiti wa kijiji akanitolea sime eti anichome nayo kisa eti nawakusanya wanawake kuwapa elimu  wasikubali kukandamizwa, lakini nashukuru walioniokoa siku ile walikuwa wanawake wenyewe, walisimama wote kuwa upande wangu wakanitetea, wakawa wanasema Rose ni Mmasai kama sisi, kwa hiyo hatuwezi kuona kila siku mnamnyanyasa, ikabidi wakawa upande wangu.

“Mwenyekiti wa kijiji akaogopa, maana walimwambia ukimgusa tena na sisi tunakugeukia wewe na tunakuja kukulaani, nilishangaa sana ujasiri uliooneshwa na akina mama wale kwa mara ya kwanza kusimama na kumbishia mwanaume tena kiongozi wao, nikashukuru sana kwamba angalau elimu niliyokuwa nimeanza kuwapatia imewaingia, hapo ndipo nikaanza kupata watetezi kwa jamii ile,” anasimulia Rose.

Rose anasema, baada ya siku ile, walewale wanawake waliomtetea ndio waligeuka wakaanza kuelimisha na wengine kwenye jamii ile namna ya kubadili mitizamo yao kuhusu mila kandamizi ambazo wameziamini kwa miaka mingi huku wao ndio wakiwa waathirika.

NABII HAKUBALIKI KWAO

Anasema pamoja na kwamba elimu ilikuwa imeanza kuenea lakini kuna watu walikuwa wanaendelea kupambana naye wakimwendea na kumshauri aachane na kazi yake hiyo, wakimwambia nabii hakubaliki kwao, hivyo asiendelee ili asije kupatwa na madhara na kwamba miongoni waliompa ushauri huo walikuwapo pia baadhi ya madiwani kutoka kwenye baadhi ya Kata za wilaya hiyo ya Ngorongoro.

Rose anasema aliwasikiliza lakini hakukata tamaa akaendelea na kazi yake hiyo ya kutoa elimu katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo ya Ngorongoro, na kwamba wale waliokuwa wanamwelewa aliendelea nao na wale waliokataa aliwapa muda.

 Anasema ilikuwa kama dhambi na laana kwa mwanamke wa kimasai kusimama kwenye kikao cha maendeleo ya kijiji au mkutano wa hadhara, kuzungumza hata kama kuna shida kubwa wanayotamani  kusema kwenye mkutano wa viongozi wa serikali.

“Na hata ikilazimika ukitaka kusimama ni lazima uende ukatafute majani mabichi ushikilie mkononi ndio uruhusiwe kuzungumza na ile ukishika hayo ni ishara kwamba wewe ni dhaifu ambaye hustahili kwa sababu inaaminika kwamba mwanamke akisimama ni laana kwa hiyo unashika hayo majani ili ile laana iondoke. Unakuwa umesalenda na unaomba msamaha kwa sababu mwanamke hustahili kusimama.

Lakini hata hiyo kusimama ni lazima kuwe kuna kitu cha msingi sana ambacho kimetokea umeshindwa kuvumilia, kwa hiyo inakuwa kama umejitoa mhanga na kila mtu anakutolea jicho kwa sababu siyo hali ya kawaida kuona mwanamke amesimama kijasiri.

“Hata mkisafiri kwenye gari ukiwa mwanamke, wanakuona kama laana kwa hiyo wanaweka jiwe kwenye gari ili isipate ajali, maana bila hivyo wanaamini hiyo laana yako itasababisha ajali. Unaweza pata picha ni namna gani mila za kimasai mwanamke si baraka bali laana,” anasimulia Rose.

ITAENDELEA WIKI IJAYO....