Miezi minne ziara zake maalum RC Chalamila, akitakatisha ‘uvunguni’

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 11:27 AM Jun 07 2024
 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Picha: Pilly Kigome
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.

ILIKUWA Februari 19, mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alipoanza ziara yake kuzunguka halmashauri zote tano na majimbo yanayopatikana katika halmashauri hizo kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi wake katika mikutano ya hadhara iliyofanyika maeneno tofauti na azipatie ufumbuzi.

Mbali na kusikiliza kero na dukuduku kutoka kwa wananchi, lengo la ziara pia lilikuwa kutembelea miradi inayotekelezwa katika majimbo husika kuona kasi na utekelezaji wake.

Akiwa jimboni Temeke, alitembelea mradi wa kupunguza makali ya ukosefu wa umeme pamoja na kuboresha miundombinu mkoani Temeke mradi unaogharimu shilingi bilioni 16, mradi utakaoleta umeme wa uhakika wa kutokukatika katika wenye ujazo wa KV 132 kutoka Ilala hadi  Kurasini ukiopita chini ya ardhi watekelezaji ni kampuni binfasi, unatajwa kukamilika Machi mwaka huu.

Mku wa Mkoa alitembelea mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Lumo iliyopo Yombo na hapo akabaini ‘madudu’ ya wizi na ubadhirifu kwa baadhi ya watendaji.

Pia, alizindua mradi wa shule mpya ya msingi ya Ushirika iliyogharimu jumla ya shilingi milioni 475 iliyopo kata ya Yombo Vituka.

Awali alitembelea mradi wa Shule ya mazoezi ya Chang’ombe iliyopo kata ya Migulani katika Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu cha DUCE mradi huo ulikuwa na jumla ya madarasa saba na matundu kumi ya vyoo.

Vilevile, alikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya mita 350 iliyopo mitaa ya Wailesi na Kitomondo, Temeke  ambako katika mradi hiyo, tayari fedha za DMDP zimeshapokewa kuendeleza mradi huo ikiwamo kutengeneza na kukarabati mitaro iliyopo katika mradi huo.

Akiwa katika mkutano wa hadhara Lumo Sheli mwananchi walipoanza kutoa kero zao mdokeza mkuu huyo kuna wizi umefanyika katika mradi wa Shule ya Sekondari Lumo, RC Chalamila aliwaagiza Kamanda wa Polisi na TAKUKURU kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo ndani ya saa 24 na ikithibika watu hao watachukuliwa hatua za kisheria haraka.

Waliodaiwa kuhusika na wizi huo idadi yao walikuwa saba wamedaiwa kuiba vifaa vya ujenzi wa shule hiyo mpya inayoendelea kujengwa yenye idadi ya vyumba 32 vya madarasa, ofisi 16 za walimu na matundu 96 ya vyoo kwa fedha za maendeleo ya elimu zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kutoka serikali kuu na mapato ya ndani. Mradi ulianza Januari mwaka huu.

Ziara iliendelea katika Halmashauri ya Kinondoni na huko alitembelea miradi ukiwamo Shule ya Serikali ya Chekechea na Msingi ya mchepuo wa Kiingereza iliyopo Kigogo, alitembelea mradi wa ujenzi wa jengo la ghorofa moja cha Kituo cha Afya Kinondoni.

Pia, alitembelea mtaa wa viwanda eneo la Mikocheni kwa mwekezaji wa raia wa China, akizalisha chupa za plastic zinazosafirishwa nje ya nchi.

Baadaye, Chalamila aliweza kusikiliza kero za wananchi huko katika viwanja vya Mwananyamala Mwinjuma na Mabwepande, wilayani Kinondoni.

Akiwa Mabwepande, mengi yalijitokeza huku wananchi kupiga mayowe mbele ya mkuu huyo kwa kumwomba wapatiwe shule ya msingi katika kata hiyo ambayo hakuna watoto wanakwenda umbali mrefu kufata huduma hiyo.

Wananchi hao walipiga mayowe kwa kusema kuwa kuna eneo kubwa kupitiliza ambalo halitumiki linalomilikiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), wakitaka wajengewe shule hiyo. Pia wakaomba wapatiwe eneo la maziko, kwa kuwa hawana wanafuata umbali mrefu huduma hiyo.

Akiwa katika Manispaa za Ubungo na Kigamboni, nako akakagua miradi  na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi, ikiwamo za maji, miundombinu, ardhi na ukatili na kuzipatia ufumbuzi katika ofisi zake.

RC Chalamila akahitimisha ziara yake katika Halmashauri ya Jiji la Ilala, alikotumia siku tatu kutembelea majimbo matatu; Ukonga, Ilala na Segerea, akikagua miradi na kusikiliza kero za umma.

Ni safari iliyoanza na Jimbo la Ukonga na baadaye akasikiliza kero za wananchi katika Uwanja wa Pugu Kona na ziara ikaendelea siku iliyofuata jimboni Ilala, alikokagua miradi mbalimbali, ikiwamo kutembelea Shule ya Sekondari Benjamini Mkapa.

Hapo akakagua mradi wa jengo jipya la vyumba vya madarasa na ukumbi wa mikutano wenye thamani ya shilingi milioni 800.

Akiwa hapo, Chalamila akaelezwa kutofurahishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo, akitamka anaona linanasuasua. 

Pia, akatembelea mradi wa Kituo cha Afya Mchikichini, utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni tano, akibaini matofali yanayotumika katika ujenzi huo hayakuwa katika viwango stahiki.

Ni mradi anaodai unasuasua, baada ya mkandarasi aliyepo sasa kusuasua na ujenzi, akiurithi mradi kutoka kwa mkandarasi wa awali, aliyeshindwa kuendelea na ujenzi kwa kukosa fedha, licha ya kuwa alipatiwa fedha ya awali zaidi ya shilingi bilioni moja.

Hapo akatoa agizo kwa viongozi wanaotoa tenda za miradi katika halmashauri hiyo, kuwa makini na wanaowakabidhi miradi, akiwataka watumie sifa stahiki na si kupeana tenda kwa kujuana, kunakochangia madhara katika miradi hiyo.

Awali alikagua mitaro iliyoziba kando mwa barabara eneo la Posta, ambako akawaagiza wanaosha magari ya wanaoosha magari yao, kando mwa barabarani wasiendelee na shughuli hizo pembezoni.

Nako akaziagiza manispaa husika kuwatafutia sehemu stahiki na si kando mwa barabara. Baadaye akakagua barabara za watumiaji Mtaa wa Lindi Kata ya Gerezani, alikotajiwa ilikuwa kero.

Baadaye akahitimisha na mkutano wa hadhara eneo la Ilala Kota na kupokea kero mbalimbali za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.

Siku iliyofuata, iliyoyoma katika jimbo la Segerea alikitembelea kiwanda cha Nondo cha Metro kilichopo Kiwalani kisha kuelekea Shule ya Sekondari Minazi Mirefu, alikoukagua mradi wa ujenzi wa ghorofa nne wa vyumba vya madarasa.

Baadae akaenda kukagua Kituo cha Afya Kinyerezi na kuhitimisha na kusikiliza kero za wananchi wa Tabata Kimanga, alikopatowa malalamiko mengi sana, Chalamila akidumu kuzisikiliza hadi muda wa giza.