MIAKA 63 ya Uhuru wa Tanganyika imetimia na katika sekta ya usafirishaji serikali imefanya mengi ikiwamo kujenga reli ya kisasa na pana maarufu kama SGR. Ni jambo la kihistoria.
Mafanikio ya SGR yatapatikana iwapo itaweza kusafirisha shehena kubwa na nyingi ya Congo DRC, Uganda, Zambia, Malawi, Zimbabwe na Tanzania yenyewe.
Lakini ni mradi unaohitaji umeme wa uhakika ili kusonga mbele bila kutetereka kwani nishati hiyo ni kila kitu.
Ili kupata mafanikio na mavuno ya matunda ya uhuru kwenye reli hiyo, shirika la TANESCO lijenge gridi maalumu itakayotumika kwenye usafirishaji wa reli ili kufanikisha mikakati na maono ya kuwa miundombinu bora katika ukanda huu.
Anasema Dk. Peter Kafumu, mtaalamu wa nishati na madini, anapozungumzia mambo ya kujivunia ndani ya miaka 63 ya uhuru kwenye sekta za usafirishaji akigusia SGR kwenye kusafirisha abiria na shehena.
“Tunahitaji kuwa na gridi maalum kutoka vyanzo vingine kama joto ardhi, upepo, jua na gesi kwa ajili ya kulisha usafirishaji huo,” anasema.
Gridi ya umeme ni mtandao unaohusisha kuzalisha au kufua kutoka vyanzo mbalimbali, kuukusanya pamoja na kusambaza kwa wateja.
Anafafanua kuwa ni kwasababu utahitajika umeme wa kutosha kupeleka bidhaa ndani na nje ya nchi zikifika Mpanda, Mwanza, Burundi hadi Uganda.
“Hapo ndipo kinapohitajika chanzo kingine mahsusi na gridi maalumu.” Anashauri Dk. Kafumu aliyewahi kuwa Kamishna wa Madini.
Anasema kutegemea gridi ya taifa kama ilivyo sasa kunaweza kuleta changamoto kwenye usafirishaji wa reli hiyo na kwamba ikiwezekana serikali ikope fedha kujenga chanzo na kutenga gridi hiyo isiyotegemea ile ya taifa.
Anaeleza kuwa Ulaya mfano Ufaransa na Ubelgiji umeme unaotumika kuendesha treni hizo na za mijini zina gridi maalumu iliyojengwa kulisha sekta hiyo pekee.
Anataja Ubelgiji kuwa usafirishaji mijini unategemea ‘trams’ au mabasi yanayopita juu ya reli yakitumia umeme muda wote na kwamba nishati yake haiingiliani na matumizi mengine akipendekeza Tanzania kufanya kama taifa hilo.
“Tuwe na chanzo chenye megawati kuanzia 200 kuendesha SGR yetu isitegemee gridi ya taifa.”
Dk. Kafumu anakumbusha kuwa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere ambalo ni tegemeo la SGR linazalisha umeme wa maji ambao unaweza kuathirika na changamoto za kimazingira.
“Yapo mabadiliko ya tabianchi na ukame wa muda mrefu vinaweza kuwa kitisho kwenye umeme wa maji. Nashauri kufikiria njia bora ya kuwa na gridi mahususi ya SGR,” anasema.
Anasisitiza kuwa pamoja na kutumia reli hiyo ya umeme ni vyema pia ile ya zamani ya MGR inayokwenda Mwanza, Kigoma, Kilimanjaro na Tanga itanuliwe na kuongezewa ukubwa ili kusafirisha bidhaa na abiria.
Anakumbusha kuwa marekebisho ni lazima kwa miundombinu hiyo, akisema usafirishaji wa reli ni muhimu duniani kote.
Akizungumzia maendeleo ya nishati na jubilii ya uhuru, Dk. Kamugisha Byabato, anasema kinachohitajika si gridi mpya ya SGR bali ni TANESCO kubadilika na kuwajibika.
Anashauri iwajibike kwenye hasara zinazotokana na kukatika ovyo kwa umeme hata kwa nusu dakika na kwamba kitakuwa kufidia hasara ili iwe makini zaidi.
Anasema miaka 63 ya uhuru suala la nishati ya uhakika siyo la kupuuzwa ni lazima iwepo kwa ajili ya maendeleo ya kila kitu na kufanikisha mikakati inayopangwa na wateja wadogo hadi wakubwa.
Anasema kuwapo kwa SGR kunalenga ulazima wa kuwa na umeme wa kutosha kuendesha treni hiyo tena mifumo ya kuiwezesha kutembea na kufanya kazi kwa uhakika kwa ajili ya kufanikisha kubeba shehena na abiria wa ndani na nje ya nchi na kuzuia isikwame au kusimama ghafla.
“Niseme kuboresha umeme ni lazima na kukatikakatika umeme ghafla kuishe kusiweko tena na shida hiyo tunapoelekea miaka mingine ijayo.” Anasema.
Dk. Byabato mhadhiri wa vyuo vikuu kikiwamo cha Dar es Salaam, Ardhi na sasa SAUT anasema SGR haihitaji gridi yake pekee bali TANESCO kuwa na mbinu za kuuzuia umeme uliopo usikatike ovyo, kuwa na uangalizi wa mitambo ya kuufua na kuutunza usiachwe kuvuja bila kujali.
Dk.Byabato anaamini kuwa hilo linalowezekana kwa kutumia teknolojia na kuhakikisha kuwa athari kwa reli ya SGR zinakomeshwa.
Anasisitiza kutumia vituo vya umeme vilivyopo na kujenga vingine ili kuweka akiba ya umeme utakaoendesha SGR na pia kutumia teknolojia na miundombinu bora inayolinda treni ili umeme ukikatika usiumize vyombo vya usafiri kama reli hiyo.
“Teknolojia zipo za kuwa na mifumo bora na vituo vya kutunza umeme wa akiba ili endapo mwingine utakatika utumike kutoka stesheni nyingine zinazotunza wa akiba ili kuendesha usafiri wetu.” Anaongeza.
KUBORESHA UMEME
Akirejea maendeleo ya upatikanaji nishati ndani ya miaka 63 ya uhuru Dk. Byabato injinia wa teknolojia na nishati nyadidifu anasema kwenye kipindi hicho kuna vitu vilitakiwa kufanyika mara baada ya uhuru mojawapo ni kuvipatia vijiji umeme.
“Umeme kwa kila kijiji ulitakiwa kufanyika mapema zaidi si baada ya miaka 50 ya uhuru. Ni mambo ya kitaifa yaliyohitaji kutekelezwa mapema ili kufanikisha elimu, tiba, uzalishaji hasa viwanda vidogo kwa vikubwa, kutoa huduma za mawasiliano zikiwamo simu. Kwa ujumla kuharakisha maendeleo.”
Anatoa angalizo kuwa ili umeme vijijini uwe endelevu ni lazima taifa lizalishe mafundi umeme kwa kila kijiji ili kudhibiti kukatika, kuanguka nguzo na kulipuka transfoma.
“Tulitakiwa pamoja na mradi wa Umeme Vijijini REA tuwe na mafundi umeme vijijini, kwani inawezekana ukakatika kwa zaidi ya siku 10 bila kasoro kurekebishwa kwa sababu hakuna mafundi.”
Anashauri kuwe na programu ya kufundisha mafundi umeme vijijini na kwamba utekelezaji wa dira ya maendeleo ya taifa 2050 ifanikishe upatikanaji wa mafundi wa ngazi mbalimbali watakaowahudumia wananchi.
NISHATI KITAIFA
Dk. Byabato anasema kitaifa bado umeme haujakaa sawa kwenye upatikanaji wa nishati hiyo kwa uhakika na kwamba kuna ulazima wa kuwasikiliza wataalamu ili kumaliza changamoto za nishati na umeme.
“Nashauri wanasiasa wawasikilize wataalamu tusiamue mambo ya nishati bila utaalamu, kufanya mambo kisiasa zaidi kunapunguza ufanisi na mafanikio.”
Anaonya kuwa wakati mwingine wataalamu wanaposhauri mambo wanaonekana kama wanabishana na viongozi na wanapotofautiana mwanasiasa anachukua hatua ambazo zinaathiri wataalamu.
Akizungumzia vyanzo mbadala vya nishati anashauri kuwa na kapu la nishati mchanganyiko ‘energy basket’, yenye vyanzo vingi kuanzia mabwawa, joto ardhi, nyuklia, gesi na makaa.
Anasema ni lazima kuviboresha na kutumia njia zilizoyapa mataifa yaliyoendelea mafanikio kiuchumi bila kuogopa kuwa nchi zilizoendelea zinakataza.
Kwa wakati huu dunia inasisitiza kutumia nishati safi isiyoongeza joto duniani kama jadidifu, lakini ikumbukwe kwamba yalitumika makaa wa mawe, gesi, nyuklia na mafuta hadi kufikia maendeleo waliyo nayo leo.
“Tutumie pamoja na vile ambvyo wenzetu walitumia wakapata umeme wa uhakika kama makaa ya mawe na mafuta…” anasema DK. Byabato.
“Baba wa Taifa Ghana, Kwame Nkurumah alisema tunataka kupata uhuru wa kuamua mambo yetu wenyewe, hivyo tuangalie tusiwe watu wa kufanyiwa maamuzi ya kupata maendeleo na wenzetu wa Ulaya na Marekani.”
Anashauri kutumia wataalamu na kuandaa teknolojia ya kuchakata na kupata nishati ya uhakika kwa maendeleo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED