Fadlu awajia juu CS Sfaxien

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:35 AM Dec 17 2024
Fadlu awajia juu CS Sfaxien
Picha:Mtandao
Fadlu awajia juu CS Sfaxien

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davis, amewalaumu wachezaji na benchi la ufundi la CS Sfaxien ya Tunisia kuwa chanzo cha vurugu zilizotokea juzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, katika mchezo wa raundi ya tatu wa Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mechi hiyo, Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1, lakini mchezo huo ukimalizika kwa vurugu kubwa iliyosababishwa na mashabiki, wachezaji wa benchi la ufundi la CS Sfaxien ambao walionekana kutoridhishwa na muda ulioongezwa, alisema ni aibu kwa timu kubwa kama hiyo kufanya vurugu, akilitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kufanya uchunguzi na kuchukua hatua.

Fadlu ambaye alitumia muda mwingi kulizunguzia suala hilo, alisema sababu kubwa ilianza kwa wachezaji wa timu hiyo kusingizia wameumia wakati si kweli na hata zilipoongezwa dakika saba, bado waliendelea kusingizia kuumia kitu ambacho kilimfanya mwamuzi kuongeza dakika.

"Unakuwa na timu ambayo inapoteza muda kila wanapokabiliana na wachezaji wa timu pinzani, kipa wao alikuwa kinara wa kupoteza muda, mwamuzi amefidia tumepata bao, bado haitoshi, wachezaji na benchi lao la ufundi wameingia uwanjani kwenda kumshambulia mwamuzi.

"Nadhani yote yaliyotokea na vurugu zote, CAF wanatakiwa kufanya uchunguzi wao kwa kuwatumia makamisaa wao ili kubaini chanzo cha yote na kuchukua hatua," alisema kocha huyo.

Katika mchezo huo, mashabiki CS Sfaxien pia walifanya vurugu jukwaani na kusababisha kuvunjwa kwa viti huku wakiving'oa na kuvirusha uwanjani.

Wakati Kocha Fadlu alisema hayo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetoa taarifa ya kusikitishwa na vitendo vya mashabiki kung'oa na kuharibu viti vya kukalia watazamani katika mchezo huo.

Waziri wa Wizara hiyo, Profesa, Palamagamba Kabudi, amesema kuwa amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuchukua hatua mara moja kwa kuwaandikia Klabu ya Simba na kuwanakili Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), ili gharama za uharibifu uliosababishwa wakati wa mchezo huo zilipwe.

Nalo Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, katika taarifa yake limesema litashirikiana na mamlaka zingine za kisheria kuona hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya vitendo vya mashabiki wa CS Sfaxien kufanya fujo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa wakati wa mechi yao dhidi ya Simba.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Kamanda Kanda Maalum ya Polisi, Jumanne Muliro, imeeleza kuwa katika fujo hizo, shabiki mmoja wa timu hiyo ya Tunisia aliumia na kupatiwa huduma ya kwanza, kabla ya kuruhusiwa, huku viti vya rangi ya bluu 156 na vya machungwa 100 viking'olewa na mashabiki hao.

"Fujo hiyo ilisababishwa na mashabiki wa timu ya CS Sfaxien kwa kutoridhishwa na maamuzi ya refa wa mchezo huo kuacha uendelee kwa zaidi ya dakika saba ambazo aliziongeza kama dakika za nyongeza jambo lililosababisha timu ya Simba kupata bao la pili la ushindi. Wachezaji wa ndani ya uwanja, bechi la ufundi, walikasirika, wakamfuata mwamuzi wa mchezo na kuanza kumfanyia vitendo vya kumshambulia," ilisema taarifa hiyo.

Simba ilipata ushindi kwa mabao ya Kibu Denis, yote akifunga kwa kichwa, matokeo ambayo yameifanya kufikisha pointi sita, sawa na Bravo do Maquis ya Angola ambayo juzi ikiwa nyumbani iliichapa CS Contantine ya Algeria mabao 3-2.

Pamoja na kufungwa, CS Constantine iko kwenye nafasi ya pili, nayo ikiwa na pointi sita, Simba ikiwa ya tatu kutokana na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, CS Sfaxien ikishika mkia, ikiwa haina pointi.