MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amewataka wanachama wa chama hicho kutokata tamaa, bali wawe na roho ya ujasiri na kupambana.
Amesema misukosuko inayotokea ndani ya chama hicho isiwatishe bali ni sehemu ya maisha, akiendelea kusisitiza taasisi yoyote ni lazima ipitie katika misukosuko.
Mbowe alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati akizindua ofisi ya CHADEMA Wilaya ya Kinondoni, mkoa wa Dar es Salaam.
"Kazi za siasa hazipaswi kukata tamaa, tusikubali kuingiza roho za ukataji tamaa, tuwe na roho za ujasiri wa kupambana, na tunapoingiza roho za kukata tamaa, ndipo tunaanza kutafutana uchawi, hatupaswi kutafutana uchawi.
"Tuna kila sababu ya kuimarishana, kujengana, kukumbatiana kuisaidia CHADEMA yetu ikawe bora zaidi. Na mimi kama mwenyekiti wa kipindi changu, nitahakikisha jambo hili ninalisimamia kwa nguvu kubwa sana," alisema Mbowe.
Mwenyekiti huyo pia aliwaomba viongozi na wanachama wa chama hicho kuendelea kusimamia nidhamu ya chama.
"Niwaombe viongozi wangu, nimesikia matamko mbalimbali kuhusu mambo ya nidhamu, jambo hili ni jema, kasimamieni nidhamu, na si tu kutukanwa Mbowe, kutukanwa kiongozi mwenzetu yeyote, hata angekuwa wa wilaya, wa jimbo, sisi lazima tuijenge familia, na familia haiwezi kuwa taasisi ya kutukanana, familia inakuwa taasisi ya kujengana na kutiana matumaini.
"Kasimamieni nidhamu, si kwa kuangalia sijui wewe ulimtukana Mbowe... hapana! Kwa kuangalia wewe ni kiongozi wa chama, huwatukani viongozi wenzako.
"Hata mnapotofautiana makosa au mitazamo, kawaone kama ni watu ambao wana haki hiyo, mrekebishane, mnyooshe mambo, taasisi hii ikawe imara zaidi," aliagiza Mbowe.
Mwenyekiti huyo aliwaambia wanachama wake hao wakati akizindua ofisi hiyo ya chama chake wilayani Kinondoni kuwa ni lazima waendelee kuishi kwa matumaini ili kulinda imani ya chama hicho, wakizingatia malengo ya chama chao.
"Wala misukosuko isiwatishe, ni sehemu ya maisha, ukishakuwa huna misukosuko kwenye taasisi, wewe ni mfu! Nimesema mara nyingi na nitarudia mara nyingi.
"Sisi chama chetu ni chama ambacho kinaishi, kinabadilika, kinatafuta mbinu mpya, tunamtafuta kila mmoja wetu, awe ni kijana ni mama, mzee, mtoto, kila mmoja wetu ana mchango na anapaswa kuwa wa mchango katika chama chetu.
"Kwahiyo tusikubali umoja wetu kama taasisi, tukatofautiana katika mawazo, tukaona yule aliwaza tofauti ana dhambi... hapana! Tutaendelea kujengana, kuimarishana, kusaidiana, kuongozana, kuonyana ili kwa pamoja tukaijenge CHADEMA yenye nguvu kesho kuliko ilivyo kuwa jana," alisema Mbowe.
Alisema chama hicho kwa sasa kimekuwa tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma, akiwataka wanachama kuendelea kukijenga na wasitoke kwenye mstari.
"Hiki chama awali kilikuwa ni cha watu wachache, leo kimekuwa ni chama cha kitaifa, wapo ambao ni wana CHADEMA, wapo ambao siyo wana CHADEMA, wote wanaona CHADEMA ndio tumaini pekee lililobaki katika taifa hili.
"Hawa watu tukiendelea kuimarika watakuja CHADEMA, hatimaye tutakuwa jeshi kubwa kuliko chochote kinachoweza kufikiriwa na hapo ndoto yetu ya kuliongoza taifa letu itakuwa inakwenda kutimia.
"Mungu awabariki, mkae kwa amani, mwendelee kukijenga chama, na kukilinda na kulindana wenyewe kwa wenyewe ili wote tusitoke kwenye msitari," alisema Mbowe.
UCHUKUAJI FOMU
Wakati huo, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, jana alitangaza mchakato na ratiba ya uchaguzi wa chama ngazi ya taifa na mabaraza yake kwa kufungua dirisha la kuchukua na kurejesha fomu za kugombea nafasi mbalimbali kuanzia leo hadi Januari 5 mwakani.
Nafasi zinazogombewa ni za Mwenyekiti Taifa, Makamu Mwenyekiti Bara, Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Katibu Mkuu Baraza la Wazee (BAZECHA) Bara, Naibu Katibu Mkuu Bara, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar na Mweka Hazina.
Wengine ni wajumbe watano wa Baraza Kuu ambao wanne kutoka Tanzania Bara na mmoja kutoka Tanzania Zanzibar, pamoja na wajumbe 20 wa Mkutano Mkuu ambao 15 kutoka Tanzania Bara na watano kutoka Tanzania Zanzibar.
Mnyika pia alitolewa ufafanuzi hoja za Lissu kuhusu uadilifu ndani ya chama, ikiwamo ya kupenyezwa fedha chafu, akitoa angalizo kuwa hoja za aina hiyo zilipaswa kutolewa kwa kufuata utaratibu wa ndani ya chama hicho badala ya ilivyo sasa - kutoa tuhuma nje ya utaratibu wao wa ndani.
"Nisisitize tu kama mtendaji mkuu wa chama, kwa nafasi yangu, ikiwa kuna kiongozi yeyote au mtu yeyote kwa maana ya mwanachama wa CHADEMA, ana tuhuma dhidi ya yeyote, aziwasilishe ili zishughulikiwe kwa mujibu wa katiba, itifaki na maadili ya chama na si kutoa tuhuma za jumlajumla, bila kusema kwamba 'hapa kuna huyu anatuhumiwa na hili na hili'.
Na katika hatua yoyote ile ya uendeshaji wa CHADEMA, tukipata tuhuma ambazo tunaona zina ushahidi wa kushughulikiwa, tutapeleka kwenye vikao vya kikatiba vya chama ambavyo kwa ngazi ya taifa.
"Tuhuma yoyote inayohusu mtu yeyote kwenye ngazi ya taifa, inapelekwa kwenye Kamati Kuu ya chama na yenyewe inaweza kuamua ama kushughulika na tuhuma hiyo yenyewe au kuikabidhi kwa Kamati ya Maadili ya Taifa ya chama," alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED