MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kupiga ‘darubini’ ya kiuchunguzi kwa wakati wote kwenye matumizi ya mitandao na simu katika kuhamisha fedha za rushwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika mwakani.
Mbali na kuelekeza nguvu zaidi katika uchaguzi ujao, pia ameelekeza TAKUKURU kufanyia kazi Taarifa ya Ukaguzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa taasisi 44 za umma zilizokaguliwa mwaka 2022/23.
Dk. Mpango alikuwa akizungumza jana jijini Arusha, wakati alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa viongozi wa TAKUKURU. Makamu wa Rais alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa Dk. Mpango, taarifa hiyo ya ukaguzi ya PPRA inaonesha zabuni 15 zenye thamani ya Sh. bilioni 67.27 zimetolewa kwa kutumia maelezo ya zabuni (tender specifications) yenye kubagua baadhi ya wazabuni.
"Wazabuni walichaguliwa na kupewa mikataba 25 yenye thamani ya Sh. bilioni 56.7 pasipo kuidhinishwa na Bodi ya Zabuni. Aidha, majadiliano ya mikataba 23 ya taasisi saba, yenye thamani ya Sh. bilioni 64.5 yalifanyika bila kuwapo mpango wa mahojiano, yaani 'negotiation plan'.
"Lakini pia, mikataba 60 yenye thamani ya Sh. bilioni 54, ilitiwa saini pasipo kuidhinishwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Na mikataba 10 ya ununuzi kwenye taasisi tano yenye thamani ya Sh. bilioni 7.48 iliongezwa muda bila kufuata utaratibu.
"Sasa yote haya yanadhihirisha kuwa katika taratibu za ununuzi vipo viashiria vikuu vya rushwa. Kwa hiyo ni vyema TAKUKURU ifanyie kazi taarifa hizi na kuchukua hatua stahiki," aliagiza.
Katika hotuba yake hiyo, Dk. Mpango alitaja maeneo tishio yanayotikisa kwa rushwa hivi sasa nchini kuwa ni sekta za ardhi, Jeshi la Polisi, rushwa kubwa kwenye ukusanyaji mapato ya serikali kuu na kwenye halmashauri na zabuni.
"Vitendo vya rushwa bado vinaonekana katika sekta mbalimbali hadi sasa, na yako maeneo mengi yanayotajwa. Kuna tatizo kubwa ardhi, kuna tatizo polisi, kuna rushwa kubwa ya rushwa kwenye kusanyaji wa mapato ya serikali kuu na kwenye halmashauri.
"Kuna upande wa zabuni, kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo, kuna rushwa kwenye upatikanaji leseni lakini pia upande wa uchaguzi na kadhalika.
"Na wananchi wetu bado wana malalamiko juu ya rushwa na kunyimwa haki. Taarifa za kila mwaka za TAKUKURU, lakini pia PPRA zinathibitisha," alisema.
Kabla ya Makamu wa Rais kuagiza hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Umma na Utawala Bora, nchini, Crispin Chalamila, alisema rushwa sasa ni tatizo la kidunia lenye madhara makubwa kwa mtu, jamii, nchi na kimataifa.
Alisema rushwa imetumika kupoka haki za watu kwa kumnyang’anya kwa mfano haki ya ardhi, yeye aliyestahili na kumpa yule asiyestahili, kwa sababu mwenye jukumu la kutoa haki amepokea fedha au kuahidiwa kupewa fedha akipindisha sheria.
"Uwezeshaji wa serikali tunaopata, umetuwezesha kwa mfano kuokoa fedha zaidi ya Sh. bilioni 18 kupitia operesheni mbalimbali za uchunguzi pamoja na ufuatiliaji miradi ya maendeleo," alisema Chalamila.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu, akizungumza katika mkutano huo, alisema katika kipindi cha mwaka 2022/23-2024/25, TAKUKURU imepewa vibali vya ajira 1,190 vya watumishi wapya wa wilaya, mikoa na vituo maalumu kulingana na uhitaji.
Alisema taasisi hiyo pia imepewa magari mapya 195 yaliyogharimu Sh. bilioni 39.174, majengo ya ofisi 23 zenye thamani ya Sh. bilioni 12.5 na kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kutandaza mfumo na kununua vifaa, jumla ya Sh. bilioni 3.446.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED