KLABU ya Singida Black Stars, imetangaza kumtoa golikipa wao, Mohamed Kamara, kwa mkopo wa miezi sita kwa Klabu ya Pamba Jiji.
Taarifa iliyotolea na klabu hiyo, imeeleza kuwa imeamua kumtoa kwa mkopo kipa huyo raia wa Siera Leone ili kupata muda wa kucheza, huku ikifuatilia kwa karibu maendeleo yake.
"Tumefikia uamuzi wa kumruhusu golikipa wetu (Kamara), kwenda kuitumikia Pamba Jiji kwa mkopo wa miezi sita. Atajiunga rasmi na timu hiyo kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili ambalo limefunguliwa Desemba 15, mwaka huu, huku benchi la ufundi likifuatilia kwa ukaribu maendeleo yake kupitia programu yetu maalum ya 'Loan Watch', kabla ya kumrudisha kikosini mwishoni mwa msimu," ilisema taarifa hiyo ya Singida Black Stars.
Kipa huyo tangu aliposajiliwa mwanzoni mwa msimu huu, amekuwa hapati namba mbele ya kipa Metacha Mnata, ambaye amekuwa akikaa langoni karibuni mechi nyingi za timu hiyo.
Kupelekwa kwa mkopo kwa mchezaji huyo kunaifanya Pamba Jiji kuwa na wachezaji watano mpaka sasa iliyowapata kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.
Timu hiyo imetangaza kuwasajili wachezaji, Deus Kaseke, Habin Kyombo, Hamad Majimengi na Cherif Ibrahim kutoka Coton Sport FC ya Cameroon.
Wakati huo huo, Singida Black Stars imepangwa kucheza dhidi ya Simba, Desemba 28, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Liti, Singida.
Kwa mujibu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), awali siku hiyo ilikuwa ichezwe mechi ya Ligi Kuu kati ya Tabora United dhidi ya Simba, lakini sasa itacheza na timu hiyo, huku mchezo huo ulioondolewa sasa utapangiwa siku nyingine.
TPLB imesema maboresho hayo yamefanyika ili kuweka uwiano sawa wa idadi ya michezo kwa klabu zote katika kukamilisha michezo ya duru la kwanza, kabla ya kuendelea na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED