SERIKALI kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, imeipongeza timu ya Simba kutokana na ushindi iliyoupata juzi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, dhidi ya SC Sfaxien ya Tunisia.
Akizungumza baada ya mchezo huo wakati wa kukabidhi zawadi ya Sh. milioni 10 maarufu Bao la Mama, ikiwa ni zawadi ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alisema Simba imefanya juhudi mpaka kupata matokeo ya ushindi mnono.
Rais Samia amekuwa akitoa Sh. milioni tano kwa kila bao la ushindi kwa timu za Tanzania zinazofanya vinazoshinda kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo kwa Simba kushinda mabao 2-1 juzi, ilikabidhiwa Sh. milioni 10 baada ya mchezo huo.
"Ninaipongeza timu ya Simba kwa ushindi kwani imefanya juhudi kubwa ikaweza kuipeperusha vema bendera ya nchi yetu," alisema Msigwa.
Katibu huyo alisema hayo yametokana na kazi kubwa inayofanywa na benchi la ufundi la timu hiyo kwa kushirikiana na viongozi na wachezaji.
Alisema wachezaji wamefanya kazi kubwa na kuweza kuwapa furaha Watanzania pamoja na wadau wa soka hapa nchini.
"Ushindi huu umewapa furaha Watanzania pamoja na wadau wa soka hapa nchini, naamini michezo ijayo watafanya vizuri zaidi," alisema.
Aidha, aliwataka wachezaji hao kuongeza juhudi ili wafanikishe malengo yao kwenye mashindano hayo ya kimataifa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED