Makundi haya kufaidika kiuchumi kupitia mafunzo, mikopo na teknolojia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:14 AM Jul 30 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa Mkombozi, Respegi Kimati.
PICHA: MWANDISHI WETU
Mkurugenzi Mtendaji wa Mkombozi, Respegi Kimati.

SERIKALI inasisitiza umuhimu wa kuwezesha watu kiuchumi na kijamii, kupitia mikopo na misaada ya kifedha, mafunzo na teknolojia ili kuwakwamua wanawake na vijana ambao ndiyo wapo wengi kwenye wimbi la umaskini.

Miaka ya hivi karibuni, Baraza la Taifa la Kuwezesha Wananchi Kiuchumi, limeendesha mafunzo na kampeni za kuwainua watu kiuchumi ili kuondokana na adha ya umaskini mijini na vijijini. 

Aidha, baraza linasisitiza kuwa, kuongeza mali na fedha ni muhimu ili kuwawezesha wananchi, na  kujenga taasisi zinazokuza uwekezaji wa umma kama benki, vikoba na vyama vya ushirika ambavyo ni muhimu kwa kutoa mikopo, gawio kwa wanahisa, teknolojia na mafunzo ya kuendeleza miradi ya kiuchumi nchini. Mathalani, linapozungumzwa suala la uwekezaji na uwezeshaji, linagusa mitaji (fedha) na taasisi zinazotoa huduma hiyo. 

Kitaifa, katika kuupa nguvu uwekezaji na uwezeshaji, serikali imeunda kamati ya kitaifa ya kusimamia, ambacho ni chombo kilichoundwa kisheria ili kusimamia na kuangalia ufanikishaji wa mikakati hiyo, kama kifungu cha 5(1) cha sheria ya uwekezaji kinavyoelekeza. 

‘…ili kuhamasisha, kuwezesha na kutekeleza kwa ufanisi miradi ya uwekezaji, kutakuwa na Kamati ya Taifa ya Uwekezaji, itakayokuwa na wajumbe wafuatao: Waziri Mkuu ambaye ni Mwenyekiti, Waziri wa Uwekezaji ambaye ni Makamu Mwenyekiti, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Fedha.” 

Aidha, wapo pia mawaziri wa katiba na sheria, serikali za mitaa, sera na uratibu, Gavana wa Benki Kuu, Kamishna Mkuu wa TRA ili kusimamia uwezeshaji huo. 

Katika uwezeshaji kimitaji hasa kifedha, Benki ya Mkombozi ni sehemu ya wadau wanaojitokeza kuendeleza jukumu hilo, chini ya sera na sheria ya ushirikano wa sekta binafsi na umma (PPP). 

Ili kuwafikia na kuwahudumia wananchi, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Mkombozi, Respige Kimati, anasema wakati wowote kuanzia sasa vijana walio katika sekta ya usafirishaji mfano, bajaji watanufaika baada ya benki hiyo kupata majibu ya namna gani ya kuwawekea mazingira bora ya kuwapa huduma maalumu. 

Anasema zama hizi ni lazima benki na taasisi zitoe mitaji, ziwe karibu na vijana na wanawake kwenye kutoa huduma ili kuwaletea maendeleo endelevu. 

Akizungumza na wanahabari wakati wa mkutano mkuu wa 15 wa wanahisa wa Benki ya Mkombozi mwishoni mwa wiki, anasema benki hiyo inayatazama kwa jicho pevu makundi ya wajasiriamali wanawake na vijana kuanzia wajasiriamali wadogo zaidi, hadi wa kati na kuwaandalia huduma maalumu kwa kuangalia changamoto zao. 

“Vijana wanaojishughulisha na usafirishaji, mfano bajaji tunafikiria kuwawekea mazingira bora yatakayowapa huduma bora zaidi ili kuwapeleka mbele zaidi,” anasema Kimati. 

Aidha, anaeleza kuwa wanazingatia na kuchambua changamoto za kila mteja ili kuwahudumia, na kuwa na mifumo inayolenga kuwafikia kwa hali yoyote waliyo nayo.  

Anawasifu wanawake kwa uaminifu kwa kurudisha mikopo ya vikundi, na kwamba kundi hilo linaongoza kulipa mikopo na siyo wakwepaji kama makundi mengine. 

Katika juhudi za kuwahudumia wananchi kifedha, anasema Mkombozi imejisogeza zaidi na wananchi ikifikia mikoa tisa na matawi zaidi ya 13 tangu ulipoanzishwa mwaka 2009.

Kimati, anaongeza kuwa Benki ya Mkombozi inatarajia kutoa gawio mwaka huu kwa wanahisa, ambao walikuwa wanalitamani kwa muda mrefu. 

Aidha, akizungumzia kuwapo kwa mazingira ya kuendeleza uwezeshaji wananchi kwenye huduma za kibenki akisema kuwa wamefanikisha kupata faida, kukua na kuongeza zaidi wateja. 

 “Tumepata faida (kabla ya kodi) takribani Sh. bilioni 8.6 kwa mwaka huu na tuna matumaini ya kupunguza pia uwiano wa gharama za uendeshaji dhidi ya mapato, vilevile kupunguza kiwango cha mikopo isiyolipwa ili kifikie chini ya asilimia tano,” anasema. 

Anasema kazi ya kuwawezesha wananchi inafanyika kila mahali kwa kushirikiana na mawakala zaidi ya 1,200 kwa nchi nzima.  

MWASISI AGUSA WANAWAKE 

Edwina Lupembe ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Mkombozi, anasisitiza kuwa ni  muhimu zaidi kuendeleza uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, kama ilivyoainishwa na kaulimbiu ya mwaka 2024 ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake ambayo ni "Wekeza katika wanawake: Kuharakisha maendeleo.” 

Akishiriki mkutano wa wanahisa, anawaasa wanawake kuachana na mikopo ya kausha damu, akiwakumbusha kuwa kuna taasisi nyingi zinazotoa mikopo ya vikundi na mtu mmoja mmoja na namna ya kuitumia mikopo hiyo. 

“Wanawake waachane na mikopo ya ‘chap chap’ waliona wapi? Wawe na subira, wafanye kazi na taasisi zinazoheshimika kama benki.” 

Edwina anasema watumie benki ambazo zinazowakopesha, kuwafunza na kuwaelekeza namna bora ya kuendeleza biashara, kulipa deni kwa utaratibu huku biashara ikiendelea kustawi. 

“Kuna taasisi zinazokopesha na kuwezesha watu kisheria, sasa mtu unakwendaje kwenye mikopo  ya kaushadamu? Unapewa Sh.100,000 unalipa Sh. 200,000 unazipataje au wapi baada ya wiki moja?”Anahoji.  

Anawataka wanawake kuwa na nia na subira wanapoanza kuomba mikopo ya vikundi ili wakue baada ya muda wafikie hatua ya kukopa peke yao na kuondoka kwenye vikundi. 

Edwina, anasema alipoanzisha benki hiyo baada ya miaka minne alitoa gawio na kueleza anachoona kwa benki hiyo. 

“Naiona Mkombozi kama Benki ya Centenary ya Uganda ambayo imekua na kusambaa nchi nzima na kufikia mamilioni ya wateja” anasema na kuongeza kuwa, lengo ni kukomboa watu kiuchumi (kimwili) na kiroho kupitia huduma za mafundisho ya Injili. 

“Naona fahari kama mwanamama, kitu nilichoanzisha kinakwenda vizuri, najisikia vizuri kuona mafanikio na mbio kuanza tena kutoa gawio na mikopo isiyolipiki ikiondoka,” anasema Mama Edwina. 

Kasmir Njuu ni Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Mkombozi, anayeeleza kuwa kazi ya kuwezesha wananchi imefikia zaidi ya wateja 100,000. 

Anasema huwezi kuwafikia watu bila kutoa huduma kidijitali, bila kutumia mawakala na kwamba kwenye makanisa kuna huduma ya sadaka dijito, ambayo waamini wanatoa sadaka zao kielektroniki. 

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mkombozi, Askofu Beatus Kiyaiya, anazungumzia malengo ya uwezeshaji kupitia taasisi hiyo kuwa ni kuwezesha wananchi wa hali zote hasa wa chini zaidi walioko vijijini na mijini. 

“Mkombozi tunahitaji kumkomboa mwananchi wa hali zote yaani mkulima wa chini, mvuvi na mfanyabiashara mdogo ambapo benki itawafikia na kuwapa huduma ili kujenga maisha yao,” anasema. 

Anasema zaidi ya wanahisa 600 kutoka Tanzania nzima wameshiriki mkutano huo na kujadili mfanikio, uwezeshaji na mikakati ya kusonga mbele.