UTAJIRI wa mafuta licha ya kuonekana neema kwa raia wa Sudan Kusini, sasa umegeuka kuwa chanzo cha vifo na mateso kwa raia maskini wa taifa hilo jipya na changa duniani.
Ni katika jimbo la Unity ambako mafuta yamesambaa ndani ya mito na mabwawa ya maji ya kunywa tatizo likiongezwa na mafuriko.
Serikali na kampuni zinazochimba mafuta nchini humo zinalaumiwa kwa tatizo hilo ambalo limesababisha vifo, ulemavu na watoto kuzaliwa wakiwa na kasoro za kimaumbile kama viungo kuungana.
Jimbo hilo ndilo kubwa Sudan Kusini linalozalisha mafuta mengi na linakumbwa na mafuriko kila wakati wa mvua.
Tangu 2019, mvua kubwa zinazonyesha zinasababisha mafuriko na maji kutuama, kuharibu mashamba, makazi vijijini na pia misitu.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilithibitisha kwamba theluthi mbili ya jimbo la Unity ilifunikwa na maji, hadi sasa karibu asilimia 40 ya jimbo hilo liko chini ya maji.
Hata hivyo, mafuta kusambaa na kufikia maeneo yenye maji yamesababisha janga kubwa kiasi ambacho asilimia kubwa ya watu wa eneo hilo wanakunywa maji yaliyochanganyika na mafuta.
Chifu katika eneo hilo, Chilhok Puot, anasema wapo hatarini kutokana na mafuta kutoka kwenye machimbo kusambaa kwenye maji wanayokunywa, kupikia na kunywesha mifugo.
"Maji ni machafu kwa sababu eneo hili lina mafuta ambayo yana kemikali hatarishi,” anasema chifu Puot.
Nyatabah, mwanamama kutoka jamii ya wafugaji wanaoishi katikati ya Unity, anasema mtu akinywa maji hayo anapumua kwa nguvu na kukohoa.
“Tunajua ni maji machafu, lakini hatuna mahali pengine popote, tunakufa kwa kiu." Anaeleza Nyatabah.
SERIKALI LAWAMANI
Mhandisi wa zamani wa kampuni ya mafuta ya Greater Pioneer Operating Company (GPOC), David Bojo Leju, ameiambia BBC, kuwa mafuriko katika eneo hilo yanabeba mafuta hadi kwenye vyanzo vya maji.
Eneo kubwa la jimbo hilo liko kwenye maji kwa miaka kadhaa baada ya mafuriko ambayo hayajawahi kutokea, na wanasayansi wanasema yamepata nguvu kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Sudan Kusini ni taifa changa duniani na mojawapo ya nchi maskini zaidi, ambayo serikali inategemea mafuta kupata pato la taifa.
Bojo Leju alifanya kazi kwenye kampuni hiyo ambayo ina ubia kati ya kampuni ya mafuta ya Malaysia, India na China, huku serikali ya Sudan Kusini ikimiliki asilimia tano pekee za hisa.
Baada ya bomba kubwa kupasuka miaka mitano iliyopita, Bojo Leju alianza kupiga picha ya madimbwi ya maji yenye mafuta na marundo ya udongo mweusi katika eneo hilo.
Anasema umwagikaji wa mafuta kutoka katika visima vya mafuta na mabomba lilikuwa ni jambo la kawaida na yeye alihusika katika kuondoa udongo uliochafuliwa katika barabara ili usionekane.
Alielezea wasiwasi wake kwa wasimamizi wa kampuni, lakini anasema hatua iliyochukuliwa ni ndogo na hakukuwa na mpango wa kuusafisha udongo huo.
Bojo Leju anasema maji yanayotolewa kutoka ardhini wakati mafuta yanapotolewa, mara nyingi yanakuwa na hidrokaboni na kemikali zingine hatari.
"Swali ni wapi maji hayo yanakwenda?" Anahoji na kuongeza: “Yanakwenda mpaka mtoni, hadi kwenye vyanzo vya maji ambapo watu wanakunywa, mengine kwenye madimbwi ambako watu huvua samaki."
ATHARI VIUMBEHAI
Wanakijiji wa Roriak, wanakunywa maji machafu ambayo yanasababisha athari kwao na mifugo.
Wanasema mifugo inazaa ndama ambao hawana vichwa au viungo.
Waziri wa Kilimo wa Jimbo la Unity anasema vifo zaidi ya ng'ombe 100,000 vimeripotiwa ndani ya miaka miwili kutokana na mafuriko pamoja na uchafu wa mafuta.
Katika msitu ulio karibu na Roriak, wanaokata miti kutengeneza mkaa wanasema maji yaliyopo ndani ya msitu ni machafu.
Wakimbizi wanaoishi karibu na mji mkuu wa jimbo hilo, Bentiu, inayohifadhi watu 140,000 waliokimbia vita au mafuriko anasema kambi hiyo imezungukwa na maji ya mafuriko.
Wanatumia maji kutoka kwenye kisima ambacho sio salama kwa ajili ya kunywa na kupikia.
Wataalamu wa afya na wanasiasa katika eneo hilo wameambia BBC, kuwa wanaamini uchafuzi wa mazingira na ukosefu wa maji safi unaathiri afya ya umma.
Katika hospitali moja katika mji wa Bentiu, mama amejifungua mtoto aliyeungana na pua na mdomo .
“Inawezekana uchafuzi unaohusiana na mafuta unaweza kuchangia kuongezeka kwa hatari ya kuzaliwa kwa watoto wenye kasoro," anasema Dk. Nicole Deziel, mtaalamu wa afya ya mazingira katika Chuo Kikuu cha Yale.
Uchafuzi wa mazingira ni sababu ya matatizo ya kuzaliwa watoto njiti, maumbile kutokamilika, matatizo ya uzazi na maambukizi mengine.
Mwaka 2014 na 2017, shirika lisilo la kiserikali la Bojo Leju la Ujerumani lilifanya tafiti karibu na maeneo ya uchimbaji mafuta katika Jimbo la Unity na kubaini kiwango kikubwa cha chumvi na metali nzito katika maji karibu na visima vya mafuta.
Pia maji kulionekana viwango vya juu vya kemikali ya risasi na bariamu katika sampuli za nywele za binadamu.
SERIKALI HAIJALI
Bojo Leju anasema kuzungumzia mafuta ni kama kugusa moyo wa serikali, kwani unaweza ukapoteza maisha.
Anasema 2020 alifuatwa na mawakili wa Sudan Kusini ambao walitaka kuishtaki serikali kuhusu uchafuzi wa mafuta.
Alikubali kutoa ushahidi, lakini anasema maofisa wa usalama walimzuia, kumpiga kichwani na bastola na kumlazimisha kutia saini hati ya kubatilisha ushahidi wake.
Kwa sasa anaishi nchini Sweden kama mkimbizi wa kisiasa.
Muungano wa mafuta wa GPOC na ofisi ya Rais wa Sudan Kusini hajatoa kauli kuhusu ripoti hiyo ya kisayansi.
BBC
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED