Mabeki wakali wa nyavu Ligi Kuu Tanzania Bara

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:21 AM Dec 23 2024
Beki wa kulia wa Simba, Shomari Kapombe, akishangilia bao alilofunga juzi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera, kati ya timu hiyo na Kagera Sugar, akiiwezesha kushinda mabao 5-2.
Picha: Mpigapicha Wetu
Beki wa kulia wa Simba, Shomari Kapombe, akishangilia bao alilofunga juzi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera, kati ya timu hiyo na Kagera Sugar, akiiwezesha kushinda mabao 5-2.

JUKUMU mama la kwanza kwa mabeki, siku zote ni kuzuia mashambulizi kutoka timu pinzani, lakini kwa soka la kisasa, wanawajibika pia katika kufunga, hivyo kuna mabeki ambao wamejaaliwa vipaji au kuwa na uwezo wa ziada wa kusaidia mashambulizi na kufunga mabao.

Kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea kuna mabeki ambao wamefunga na kuzisaidia timu zao kupata ushindi au kuziongezea idadi ya mabao.

Mpaka sasa wapo mabeki ambao wana mabao zaidi ya moja hadi kufikia mechi za mzunguko wa kwanza, huku baadhi ya timu zikiwa bado hazijamaliza.

Katika makala haya, tunakuletea mabeki ambao wamefunga mabao mengi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa...

1# Shomari Kapombe (Simba)

Ni beki wa kulia wa Simba ambaye kwa sasa ana mabao mawili mpaka sasa. Juzi alifunga bao kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera wakati timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 5-2. Aliunganisha mpira wa krosi kutoka kwa Mohamed Hussein 'Tshabalala.'

Awali, mchezaji huyo alifunga bao lake la kwanza Oktoba 25, mwaka huu, kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Simba ikicheza dhidi ya Namungo na kushinda mabao 3-0.

2# Ibrahim Hamad 'Bacca' (Yanga)

Beki huyu wa kati wa Yanga, amefunga mabao mawili mpaka sasa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara. Yote ameyaweka wavuni kwa kichwa.

Bao lake la kwanza alilifunga Septemba 25, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, likiwa bao pekee ambalo Yanga iliifunga KenGold.

Oktoba 3, mwaka huu, 'Bacca', alifunga bao lingine kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Yanga ikiifunga Pamba Jiji mabao 4-0.

3# Antony Trabita (Singida)

Huyu ni beki wa kati wa Singida Black Stars raia wa Ivory Coast, naye ana mabao mawili mpaka sasa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Alifunga bao Agosti 23, mwaka huu, likiiwezesha timu yake kushinda bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera.

Novemba 25, mwaka huu, alifunga bao lingine kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Singida Black Stars ikitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Tabora United.

4# Fondoh Che Malone (Simba)

Che Malone ni beki wa kati wa Simba, raia wa Cameroon ambaye msimu huu ameonekana kuwa kwenye kiwango bora na mpaka sasa akiwa na mabao mawili.

Bao la kwanza alilifunga Agosti 17 mwaka huu, kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, wakati Simba ikiizamisha Tabora United mabao 3-0.

Lingine alilifunga Oktoba 22 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, alipofunga bao pekee timu yake ikishinda 1-0 dhidi ya Prisons.

5# Erasto Nyoni (Namungo)

Beki wa kati mkongwe nchini, Erasto Nyoni, ameweka rekodi ya kufunga mabao mawili kwa mchezo mmoja.

Ilikuwa ni Desemba 15, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, alipofunga mabao mawili kwenye mchezo dhidi ya KenGold, akiiwezesha Namungo kushinda mabao 3-2 dhidi ya wenyeji wa mchezo huo.

6# Nicolaus Gyan (Fountain Gate)

Raia huyu wa Ghana ambaye alipoingia nchini kuichezea Simba alikuwa anacheza kama straika, lakini baadaye akabadilika na kuwa beki wa kulia. Mpaka sasa ameendelea kucheza kwenye nafasi hiyo na amekuwa moja ya mabeki mwenye uwezo wa kufunga mabao.

Oktoba 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Tanzania Kwaraa, Manyara alifunga bao moja, akiwezesha timu yake ya Fountain Gate kutoka sare ya mabao 2-2, Desemba 13 mwaka huu, kwenye uwanja huo huo alifunga bao katika mchezo ambao timu yake ilishinda mabao 3-2.