Mabao 6 ya faulo kati ya 135 Ligi Kuu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:35 AM Oct 28 2024
Winga wa Yanga, Maxi Nzengeli, akimbeba na kumpongeza, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Clatous Chama, baada ya kufunga bao kwa faulo ya moja kwa moja katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya timu hiyo na JKT Tanzania, uliochezwa, Oktoba 22, 2024.
Picha: Mtandao
Winga wa Yanga, Maxi Nzengeli, akimbeba na kumpongeza, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Clatous Chama, baada ya kufunga bao kwa faulo ya moja kwa moja katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya timu hiyo na JKT Tanzania, uliochezwa, Oktoba 22, 2024.

HADI kufikia jana, jumla ya mabao 135 yamefungwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, ambayo imeingia raundi ya tisa, huku baadhi ya timu zikiwa zimecheza michezo minane, Mashujaa FC na Yanga zikiwa zimecheza michezo zaidi, saba kila moja.

Kati ya mabao hayo, ni sita tu ndiyo yamefungwa kwa mikwaju ya faulo za moja kwa moja mpira ukatinga wavuni.

Timu ambazo mpaka sasa zimefanikiwa kufunga mabao ya faulo za moja kwa moja ni Fountain Gate ambayo imepachika mawili, Yanga, KMC, Prisons na JKT Tanzania.

Katika makala haya tunakuletea rekodi za faulo zote hizo, jinsi zilivyofungwa pamoja na wachezaji ambao wamezipachika nyavuni. 

1# Dickson Ambundo - (Fountain Gate vs Dodoma Jiji)

Dickson Ambundo, winga wa zamani wa Yanga, ndiye mchezaji wa kwanza msimu huu kufunga bao la faulo ya moja kwa moja kwenye Ligi Kuu.

Alifanya hivyo Septemba 15 mwaka huu, wakati timu yake ya Fountain Gate ikicheza dhidi ya Dodoma Jiji, Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati, Karatu.

Ilitokea faulo kwenye wingi ya kushoto nje kidogo ya eneo la hatari la Dodoma Jiji, huku wachezaji wawili wakijipanga kupiga.

Alikuwa ni Ambundo na Amos Kadikilo. Wakati wote wakidhani Kadikilo atapiga na mguu wa kushoto, Ambundo alipiga faulo kwa mguu kulia uliokwenda kutinga kwenye engo ya pembeni juu ya lango la Dodoma Jiji.

Bao hilo lilifungwa dakika tano kabla ya mechi kumalizika na lilikuwa la kusawazisha, timu hizo zikitoka sare ya mabao 2-2. 

2# Redemtus Mussa - (KMC vs KenGold)

Siku moja baada ya kupatikana kwa bao la kwanza la faulo kwenye Ligi Kuu ya Tanzania, katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam, lilipatikana bao la pili lililowekwa wavuni na Redemtus Mussa, KMC ikicheza dhidi ya KenGold.

Ibrahim Elias aliangushwa nje ya eneo la hatari pembeni, wingi ya kulia na mwamuzi akaamuru faulo.

Ilionekana kama mpigaji atapiga krosi, kwa sababu faulo hiyo ilitokea karibu na kibendera cha kona.

Haikuwa hivyo, Redemtus alitumia mguu wake wa kushoto kupiga mpira huo kuelekea golini moja kwa moja, ukawachanganya beki na kipa wake kabla ya kujaa wavuni, dakika ya 14, mechi iliyochezwa Septemba 16, mwaka huu, KMC ikiondoka na ushindi wa bao 1-0. 

3# Ezekia Mwashilindi - (Prisons vs Fountain Gate)

Beki wa Prisons, Ezekia Mwashilindi, anaingia kwenye rekodi ya kuwa mmoja wa wachezaji waliofunga mabao kwa faulo za moja kwa moja, kwenye Ligi Kuu msimu huu, baada ya kufanya hivyo, Oktoba Mosi, mwaka huu, Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, timu yake ikicheza dhidi ya Fountain Gate na kuondoka na ushindi wa mabao 3-2.

Beki mmoja wa Fountain Gate aliunawa mpira nje na mbali kidogo ya eneo la hatari. Ilikuwa ni pembeni kidogo wingi ya kushoto.

Aliupiga kiufundi zaidi na kuonekana kama unatoka nje, lakini ulizunguka na kujaa wavuni, akiipatia timu yake bao la kusawazisha dakika ya 48.

Wakati huo timu yake ilikuwa nyuma kwa mabao 2-1 na kuingia kwa bao hilo kuliamsha ari ya wachezaji wenzake, dakika mbili baadaye wakapachika la tatu lililofungwa na Vedatus Mwihambi. 

4# Said Ndemla - (JKT Tanzania vs Tabora United)

Kiungo mshambuliaji wa JKT Tanzania, Said Ndemla yumo kwenye orodha hii, baada ya kupiga faulo ya moja kwa moja iliyozaa bao la nne katika mchezo uliochezwa, Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Oktoba 18, mwaka huu, dhidi ya Tabora United, ikishinda mabao 4-2.

Kipa raia wa Nigeria, Sochima Victor, alitokea na kuudaka mpira nje ya mstari, hivyo kusababisha faulo na yeye mwenyewe kuoneshwa kadi nyekundu.

Faulo iliyopigwa kwa shuti kali umbali ya mita yadi 35 hivi na kwenda moja kwa moja wavuni, dakika ya 68 ya mchezo. 

5# Dickson Ambundo - (Fountain Gate vs KMC)

Kwa mara nyingine tena, Ambundo anarejea tena katika orodha na rekodi ya wapachikaji mabao ya faulo kwenye Ligi Kuu.

Safari hii akifanya hivyo, Oktoba 21, mwaka huu, Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Manyara timu yake ikicheza dhidi ya KMC na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Alipiga faulo mbali kiasi cha takriban yadi 30 hivi, bila yoyote kudhania kama lingeweza kuwa bao.

Lilikuwa ni shuti dhaifu, kwa mastaajabu wa wengi, kipa Fabian Mutombora raia ya Burundi, alionekana kama ameukamata, lakini ulimpita tobo na kujaa wavuni dakika ya nane ya mchezo.

Ndiye anaongoza kwa kufunga mabao mengi ya faulo kwenye Ligi Kuu mpaka sasa. 

6# Clatous Chama - (Yanga vs JKT Tanzania)

Rekodi inaonesha kuwa, Clatous Chama ni mchezaji pekee wa kigeni aliyefunga bao la faulo kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa. Watano waliobaki wote ni wazawa.

Chama alifunga bao kwa mtindo huo, Oktoba 22, mwaka huu, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, akiisaidia timu yake kushinda mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania.

Makosa yalianzia kwa kipa Denis Richard, aliyedaka shuti la Pacome Zouzoua nje ya eneo analoruhusiwa kufanya hivyo.

Moja kwa moja alizawadiwa kadi nyekundu na timu yake kulazimika kumtoa Hassan Kapalata na kumuingiza kipa mwingine, Omary Gonzo, ambaye alishindwa kuzuia faulo ambayo alisababishwa na mwenzake, iliyopigwa na Chama.