ZAMANI wakati kuna vituo vichache tena vya kuhesabika vya redio, achilia mbali luninga ambayo haikuwa akilini mwetu, tulihimizwa sana utulivu wakati wazee wetu wakisikiliza taarifa za habari au mijadala ya kuelimisha umma.
Lilikuwa kosa la jinai kifamilia, baba au mama anasikiliza redio halafu wewe unapiga kelele, au kuleta mchezo unaosababisha kuondoa utulivu wa masikio ya wasikilizaji hao.
Bila shaka kama mjeledi au mkwaju vilikuwa mbali, hukukosa kofi, kibao au kwenzi la nguvu kutoka kwa wakubwa hao ukaugulie, ili kurejesha utulivu na taarifa ya habari isikike vizuri na hasa siku ambayo Mwalimu Nyerere alizungumza.
Lakini kulikuwa na vipindi kama Chakula Bora na hata cha Michezo, ambako kila mwenye timu yake, alitaka kujua imefanya nini au kulitokea nini katika mechi zipi siku hiyo.
Vipindi kama Majira, Watoto Wetu na Utabiri wa Hali ya Hewa vilipendwa sana, kwani vilijulisha matukio ya siku, pia kunyesha au kutonyesha mvua na hata radi na kuziepuka pamoja na kuelimisha watoto.
Nakumbuka kipindi pekee kilichokuwa na mbwembwe ni cha Klabu Raha Leo, pia Misakato, ambayo bendi za muziki wa dansi zilikwenda studio kurekodi na kupiga muziki mubashara, pia nyimbo mpya zilizosikika mtawalia.
Watangazaji wa vipindi hivyo hususan vya taarifa, walitulia na hakuna aliyesikika akikohoa au kupiga chafya, achilia mbali kupasuka kicheko cha kuvunja mbavu, isipokuwa kipindi cha Mahoka!
Ingawa hakukuwa na wasomi wengi kama sasa, lakini watangazaji walitumia Kiswahili fasaha na usingesikia mahali wanachanganya na kilugha chao au hata lugha ya kigeni hususan Kiingereza.
Na kama walilazimika kutumia Kiingereza, ilikuwa ni katika idhaa ya Kiingereza, ambayo kila kitu kilikwenda kwa lugha hiyo, bila kuingiza Kiswahili au lahaja yoyote.
Tunaambiwa studio kulikuwa na msimamizi wa kipindi, ambaye alihakikisha kila kitu kinakwenda kilivyopangwa, bila mtangazaji kuchanganya mbwembwe.
Leo hii, tuna vituo kibao vya redio mpaka vijijini, huku vikizidiana kwa ukubwa unaoendana na ukwasi wa wamiliki, ambao sasa vimekuwa ni miradi ya ujasriamali.
Ndivyo pia vipindi vinavyopangwa kijasiriamali.
Tofauti na awali, hivi sasa msikilizaji ndiye anakimbia kelele zinazopigwa na watangazaji, wakishindana kupaza sauti, ili kila mmoja asikike kuwa ndiye gwiji katika mada kuliko mwenzake, wakikatishana hapa na pale.
Aliyeanzisha kituo leo hatofautiani na aliyeanzisha jana, kwa sababu ya kuigana maudhui. Ukianzisha cha michezo, nami nakuja na cha michezo, sawa tu na mama lishe mtaani, akiuza vitumbua na mwenzake anaiga.
Kinachonisikitisha sasa, ni utiriri wa vituo ambavyo vimeanzisha vipindi vya michezo, vinavyotawaliwa na wachambuzi, baadhi yao wakijifanya kujua michezo kuliko hata wachezaji na makocha wao.
Nongwa zaidi ni pale wanapotumia zaidi Kiingereza katika vipindi vya Kiswahili, ambavyo hata hivyo vina majina ya Kiingereza! Ni mshangao mtupu! Unajiuliza wanamtangazia nani nchini? Mwingereza au Mswahili?
Aachiwe mwalimu wa kigeni watimu atiririke Umombo sasa, nani wa kufasiri? Thubutu! Utaambiwa tu kama mlivyomsikia kocha…!
Juzi asubuhi ikabidi niamke kitandani, nikakaa nisikilize kipindi fulani hivi cha watangazaji wanaojifanya mahiri, wakiwa wamemwalika mbunifu studio kuzungumzia ubunifu wake.
Nikamsikia mmoja akisema, nchini wabunifu hawatambuliwi wala kujaliwa kama wa kigeni, akasema ukitaka ubunifu wako utambuiliwe labda basi ufuatane na Mzungu hata kama ni kichaa, ili mradi awe karibu na wewe.
Kwamba Mzungu anapewa kipaumbele kuwa ndiye hasa anaweza kubuni jambo likakubaliwa katika jamii ya Kitanzania. Wakati nashangaa hiyo, nikidhani mtangazaji mpenzi anasema hivyo kwa dhati, nikamsikia papo hapo anachanganya Kiswahili na Kiingereza katika kauli zake.
Nikamwona na yeye kama hajui akisemacho, kwani anampiga vita Mzungu, huku naye akishindwa kujiamini, kwamba hawezi kuzungumza Kiswahili muda wote, bila kuchaganya, kwani hataonekana anajua kazi anayofanya!
Msomaji wangu, ukisikiliza vipindi vya michezo vyenye wachambuzi, kama hujui Kiingereza basi acha tu kuhangaika, kwani hutaambulia kitu ingawa hata hao Watangazaji wanaojinasibu kukijua, hawakijui ila wanachomekea maneno ambayo pia si yenyewe, ila yanafanana na Kiingereza.
Zamani, watangazaji wetu, ingawa nao walikuwa vijana, lakini hawakutangaza kujitafutia kiki kama tuwasikiao leo, wakipiga kelele na kukatizana kauli na hata wakiwa na wageni watawakatiza hata kabla hawajamaliza kujieleza.Hali hiyo, si tu inatuchanganya wapenzi wasikilizaji wao, bali inatuchosha masikio na kutamani hata kukaa vijiweni kusikiliza soga za soka za huko, badala ya watangazaji ambao huingia studio bila kujiandaa na badala yake kukosoa kishabiki bila kuzingatia ukweli. Jirekebisheni bhana. Oriti uru!
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED