KUUAWA JENERALI OGOLLA Helkopta kitanzi kinachonyonga vigogo Kenya

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 11:50 AM Apr 24 2024
Hayati Mkuu wa Majeshi, Jenerali Francis Ogolla, pembeni sehemu ambayo Helkopta aliyokuwamo ilipoanguka.
Picha: Mtandao
Hayati Mkuu wa Majeshi, Jenerali Francis Ogolla, pembeni sehemu ambayo Helkopta aliyokuwamo ilipoanguka.

KWA familia, Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) na taifa zima ni kilio kutokana na wiki kumalizika na kifo cha Mkuu wa Majeshi, Jenerali Francis Ogolla na baadhi ya maofisa wa ngazi za juu wa jeshi waliopoteza maisha kwenye ajali ya ndege.

Ogolla na wenzake walikuwa kazini  katika ziara ya kukagua vikosi vya askari wanaopambana na mauaji ya raia, wizi na kutorosha mifugo .

Tukio hilo lilitokea Alhamisi Aprili 18, na kumuua mkuu wa KDF, katika eneo la Marakwet, umbali wa kilomita takriban 400 kutoka  Nairobi.
 Kuanguka kwa helkopta aliyopanda Jenerali Ogolla na kupoteza maisha yake na ya maofisa wenzake nane, wakati wakitembelea vikosi vya kijeshi vinavyopambana na uhalifu, ikiwamo wa wizi wa mifugo kunaandika historia nyingine ya vifo angani nchini humo.
 
 Itakumbukwa Mkuu wa  Majeshi anafariki dunia kwenye  helkopta ikiwa ni miaka 12  tangu kiongozi mwingine Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo Profesa George Saitoti  kufariki dunia kwa ajali ya usafiri kama huo.

Pamoja na maofisa wengine Profesa Saitoti alifariki na Naibu wake Peter Orwa Ojode, wakiwa kwenye safari ya kushiriki tukio la kijamii kijijini kwa  Naibu huyo.

Ndege yao ilianguka na kuwaka moto  na taarifa kuwa ilikuwa na sumu ambayo ilisababisha kukosa hewa safi na kupoteza maisha ya viongozi hao zikiwa zimezagaa japo hazikuthibitishwa .

Kinara na mbobezi wa mahesabu Profesa Saitoti alikuwa msomi, mtaalamu wa fikra tunduizi mchumi na mbobezi wa masuala mengi ya kisayansi, alikufa wakati taifa hilo likiongozwa na Mwai Kibaki.
 
 Mkasa huo ulitokea June 10, 2012, na kusababisha mshangao, huzuni na hofu kwa Wakenya kutokana na kumpoteza kiongozi huyo aliyekuwa pia Makamu wa Rais wa  nchi hiyo na watu wote saba waliokuwamo walikufa.

 Waliopoteza maisha nao ni walinzi wao na rubani wa helkopta hiyo, iliyokuwa  ikielekea  Nthiwa nyumbani kwa Naibu Waziri Ojode iliyoanguka katika milima ya Ngon’g nje kidogo ya Nairobi.

Kuanguka na kuungua helkopta hiyo kulitokea baada ya  mkasa kama huo kuibuka  Juni 10 mwaka 2008 kuwaua , Waziri wa Barabara, Kipkalya Kones na Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais Lona Laboso.

Miaka minne baadaye, yaani mwaka 2012 nchi hiyo ilikumbwa tena na tukio lingine la ajali ya helkopta ambayo iliondoa uhai wa aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Profesa George Saitoti na kuongeza maswali kuhusu helkopta na vifo vya viongozi.
 
Lakini miezi miwili baadaye, DW iliwakariri maofisa wa Jeshi la Kenya wakitangaza kupotea kwa helkopta tatu za Uganda ndani ya ardhi ya Kenya zikiwa njiani kuelekea nchini Somalia.
 
 DW ilimkariri msemaji wa jeshi hilo Bogita Ongeri, akisema helikopta hizo zilipotea karibu na eneo la Mlima Kenya, lakini rubani mmoja aliweza kuwasiliana nao, akiomba msaada.
 
 Baadaye Agosti 14 mabaki ya helikopta mbili za kijeshi za Uganda yalipatikana katika msitu wa Mlima Kenya zikiwa zimeteketea, na kwamba helkopta ya tatu ilianguka katika mlima huo.
 
 Hata hivyo, inaelezwa kuwa wanajeshi waliokuwa katika helkopta hiyo waliokolewa. Msemaji wa jeshi la Kenya Ongeri, alikaririwa akisema helkopota hizo za kivita zilikuwa zikienda kuimarisha kikosi cha Umoja wa Afrika kukabiliana na kundi la kigaidi la Al-Shabaab.
 
 Ikiwa ni miaka minne kupita tangu kupotea kwa helkopta hizo za Uganda ndani ya nchi ya Kenya,  kuanguka kwa helkopta iliyopanda Jenerali Ogolla na maofisa wenzake nane  walikuwa katika ziara ya kutembelea vikosi vya kijeshi vinavyopambana na uhalifu, ikiwamo uhalifu sugu wa wizi wa mifugo, linakuwa tena habari ya kusikitisha.
 
 Inaelezwa kuwa helikopta hiyo ilikuwa imetua katika uwanja wa shule moja, baada ya muda au  dakika chache ikapaa, lakini ikashindwa kuendelea na safari na kuanguka kasha kuua watu saba na kujeruhi wawili.
 
        UCHUNGUZI WA AJALI
 Rais wa nchi hiyo, William Ruto anasema, serikali itafanya uchanguzi wa kifo cha Jenerali Ogolla  na utawekwa wazi, ili Wakenya wajue chanzo cha ajali ya helkopta iliomuua na maofisa wenzake.
 
 "Ninataka kuhakikishia nchi kwamba wanajeshi wa Ulinzi wa Kenya na Jeshi la Wanaanga wana uadilifu na weledi unaohitajika ili kuhakikisha kuwa hakutakuwa na mashaka yoyote kuhusu kilichompata Jenerali Ogolla," Rais Ruto anasema.
 
 Katika ujumbe wake, Rais Ruto anamsifia Jenerali Ogolla kwamba alikuwa kamanda mwenye ari ya kufanya kazi na raia mzalendo wa Kenya mwenye unyenyekevu na uadilifu mkubwa.
 
 Wakati akisema hayo, hasimu wake kisiasa Raila Odinga anatupilia mbali madai kwamba Jenerali Francis Ogolla alijaribu kubatilisha ushindi wa William Ruto katika uchaguzi wa Agosti 2022.
 
 Mwanasiasa huyo mkongwe, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Kenya kuanzia 2008 hadi 2013, anasema hayo  Ijumaa jijini Nairobi  wakati wa kumuaga kijeshi marehemu Ogolla.
 
 Jenerali Ogolla ameacha mjane na watoto wawili, alizikwa nyumbani kwake Jumapili iliyopita, kijijini Ng'iya, katika Kaunti ya Siaya.