KUMBUKIZI YA NYERERE: Ndivyo wengi wanavyomwangusha wamekimbia maarifa, kujielimisha

By Gaudensia Mngumi , Nipashe
Published at 09:46 AM Oct 15 2024
Hayati Nyerere .
Picha:Maktaba
Hayati Nyerere .

BABA wa Taifa Julius Nyerere alikuwa mwalimu kweli akiwafundisha wanafunzi ambao ni Watanganyika na baadaye Watanzania.

Taifa hili lilikuwa ‘darasa’, analolifundisha, kila kitu kuanzia kusoma, kuandika, kuhesabu, kulima, kutunza afya zao na kuwa na umoja.

Akiwa  mwalimu, Nyerere hakutaka taifa lenye watu wajinga akaanzisha na kutekeleza mipango mbalimbali ya elimu kuanzia, ya msingi hadi ya watu wazima miaka hiyo ikiitwa ngumbaru.

Akiamini kuwa elimu ni haki ya kila mtu, alifanya juhudi zote kuwaelimisha watoto hadi watu wazima  mijini na vijijini  na hata ‘madongo kuinama’ msamiati unaomaanisha ni sehemu ambazo hazifikiki. 

Pamoja na juhudi hizo, Nyerere alitamani kuona Tanzania ambayo elimu inatoa nafasi kwa yeyote mwenye uwezo kusoma hadi kufanikiwa.

Kwa njia hiyo aliandaa mipango ya watu kusoma  bila kujali kama ni  maskini au matajiri. Kwa msingi huo, wengi ambao wasingeweza kulipia masomo walisoma hadi vyuo vikuu na kufurahia matunda ya elimu bure.
 Mwalimu alikuwa mzee wa fikra ‘tunduizi’ alitamani Watanzania wanaposoma wajengeke kielimu wawe wadadisi wa mambo na kutafuta kujua na kusoma zaidi.

Katika maono yake alitaka elimu iwe nyenzo ya kumkomboa Mtanzania  tofauti na elimu ya kikoloni, ambayo ilikuwa inaendeleza fikra za utegemezi, kudhalilishwa.

Ni elimu iliyomfanya raia  kuwa mtumwa wa kumtumikia Mzungu au Mwarabu ama Mhindi na ikiwa na kasoro ya kujiona kuwa ukiwa na elimu kiasi juu ya Waafrika wenzako.

Kwa maana nyingine Mwalimu Nyerere alitamani kupata elimu inayoleta kizazi cha watu wenye  tabia ya kuheshimiana na siyo wenye kiburi na wanaojiona kuwa ni wasomi tena waliowazidi wote.
 
 Kwa Mwalimu Nyerere elimu ilikuwa si nadharia ambayo ni  kusoma vitabu na maandishi ya walimu ubaoni bali pia kuchanganya nadharia na vitendo.

Kuanzia miaka ya 1970, shule nyingi zilikuwa na mashamba ya kilimo na kuzalisha mazao mbalimbali kuanzia mboga, ya chakula na ya biashara.

Kadhalika, kulikuwa na ufugaji wa wanyama mbalimbali, na kazi za kujitegemea kama ufundi na useremala ili kufikia azma ya elimu na kujitegemea.

Alitamani wasomi  kuujua ufundi ili vijana wafahamu mengi zaidi ya kusoma vitabu darasani na kujibu maswali, alilenga pia skili  hasa kazi za mikono ambazo ni njia moja ya  kujenga msingi wa kujitegemea kwa mahitaji ya mwanafunzi.
 
 KISOMO KWA WAZEE

Mwalimu Nyerere alifundisha kuwa elimu haina mwisho wala haikwamishwi na umri ndipo, anapowahimiza watu wazima kusoma pia na  kujibidiisha kusaka  elimu kupitia mpango wa kisomo cha elimu ya watu wazima.

 

 Ni katika miaka ya 1970 Mwalimu mbali ya kushughulikia elimu ya watoto na vijana darasani na vyuoni, alianzisha mpango wa elimu ya watu wazima.

Wazee walisoma bila kujali wapo mijini au vijijini na  walipata fursa ya kujiongezea ufahamu kuanzia kujifunza kukaa darasani, kusikiliza walimu, kusoma na kuandika, kuhesabu kujua lugha hadi kufikia maarifa mengine ya juu katika fani na taaluma mbali mbali.
 Mwalimu alianza kuiongoza nchi ambayo wananchi wengi walikuwa hawajui kusoma chochote hata noti au sarafu ya fedha.

Kuanzia wakulima, wafugaji, wavuvi, wapasua mbao, walinzi kwenye ofisi za serikali, maseremala na viongozi wa serikali mitaani na vijijini walikuwa hawajui kitu.

Kupitia kisomo cha watu wazima aliwahimiza kujiandikisha vituoni na kusoma kwa bidii. Aidha, walihimizwa kujiongezea ujuzi kwenye fani na shughuli zao ili kuboresha maisha na kubadilisha maisha yao. 

Vitabu vilichapishwa katika fani za aina nyingi ambavyo viliwapa watu fursa ya kujifunza kusoma na pia kujiongezea maarifa na ujuzi wa kila aina.

Walijifunza kuanzia mapishi, ufugaji wa kisasa, kilimo cha mashamba na bustani, kujenga nyumba bora na ushonaji. 

 Kama ni mvuvi alijiongezea maarifa zaidi kuhusu kazi yako. Kadhalika mkulima alijizatiti kufahamu kuhusu kilimo cha kisasa, matumizi ya mbolea, viuatilifu na kuacha kulima kizamani.
 
 TULIKWAMAJE?

Ndiyo maana leo Watanzania wanapogeuka nyuma na kuangalia kazi na kampeni za Mwalimu tafakari inakuwa.


 “Kama Watanzania tungetii na kufuata maelekezo ya Mwalimu, mambo leo yasingekuwa kama yalivyo. Tungekuwa mbali kimaendeleo, na tungekuwa na mategemeo ya kufanikiwa zaidi kama ambavyo China na nchi nyingine za Asia zimefanikiwa.

 Miaka 63 ya Uhuru na 25 ya kifo cha Nyerere wapo watu wasiotaka kuelimika kama Mwalimu alivyotamani. Hawawapeleki watoto shule. Kuna baadhi wanashiriki kuwalazimisha wasichana wadogo kuingia kwenye ndoa badala ya kuwa darasani.

Leo ni zama za  utandawazi, elimu hasa masuala ya kielektroniki na kidijitali ndiyo inayoongoza dunia lakini Watanzania wengi hawana elimu wala  ujuzi wa masuala muhimu ya msingi mfano jinsi ya kutumia dawa kujitibu.

Watanzania wengi hawataki kujielimisha hata kusoma gazeti hawana muda. Ari ya kujielimisha inapungua sana  na wengi wanashindwa hata kuandika majina yao licha ya kumaliza sekondari.

 KUFOJI VYETI

Wanadaiwa wako wasomi, lakini walisaka vyeti badala ya kusoma darasani. Wanashikilia vyeti vya shahada za uzamili na uzamivu lakini hawakusoma kuna waliowafanyia mitihani na kuwaandikia tasnifu. (Dissertation).

Taifa linadaiwa kuwa na  wasomi lakini ‘vihio’ au mbumbumbu licha ya vyeti vyao kuwa na AAAA wakiita misonge au banda pamoja na  B+ ambao kiwango cha ufaulu ni zaidi ya  91/100.

Zipo familia zinanunua vyeti au kutumia vyeti vya ndugu zao kwa kubadilisha majina au kufanya chochote kinachowezekana kuwasaidia watoto wao kupata maisha hasa ajira.

USHIRIKIANA

Watanzania wamezidi kumwangusha Baba wa Taifa, aliyetamani wawe na maarifa mfano ni aibu kuamini kuwa utajiri au madaraka yanapatikana kwa kuua albino, kunajisi watoto na kutumia tunguri.

Hata watoto wadogo  wanaaminishwa kuwa njia ya mafanikio ni kupitia ushirikina na wapo mahiri wa kuvaa hirizi na kubeba dawa wanazopewa na wazazi au walezi ili wafaulu mitihani na kufanikiwa kimaisha.

Vijana wanaishi vijiweni na kusaka utajiri kwa waganga ambao wanabandika mabango kuwa wanaweza kuongeza utajiri, kutakatisha nyota na kupatia mteja fedha za majini.

Leo ni kama taifa limejaa watu waliojisahau badala ya kujiongezea maarifa katika fani na shughuli unazofanya kama kilimo, ualimu uandishi wa habari, daktari, uashi, umakenika, uvuvi au  mamalishe wanategemea ndumba.

Hakuna mwenye hamasa ya kununua vitabu, kugharamia mafunzo kama  semina badala yake tunataka kulipwa tunapopewa elimu au mafunzo.
 Kurejea nyuma kwenye imani kuwa mafanikio yanatokana na ushirikina ni aibu na kumwangusha Mwalimu Nyerere ambaye alitamani kila mmoja awe na maarifa na ayatumie kubadilisha maisha yake na kuleta maendeleo ya taifa.

Watanzania wanapoukumbuka mchango wa Mwalimu kwenye maendeleo ya taifa, hebu watafakari njia zao, hasa kwenye elimu kwa kutafuta maarifa badala ya ushirikina, kufoji vyeti na kuacha kujielimisha kwa manufaa binafsi na taifa.