Kuenguliwa wapinzani kunavyoibua hofu matukio ya 2020 kujirudia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:22 AM Nov 13 2024

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Magdalena Sakaya.
Picha:Mtandao
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Magdalena Sakaya.

MCHAKATO wa kuchukua na kurejesha fomu za kuomba uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa, umemalizika ukiwa umeacha maswali kwa vyama vya upinzani na wananchi.

Ni kutokana na kile kinachoelezwa kuwa wagombea wa upinzani wanaenguliwa katika mazingira na sababu ambazo wanadai zinawashangaza.
 
 Wakati waliopitishwa wakielekea kwenye kampeni za uchaguzi huo zinazotarajia kuanza Jumatano ijayo Novemba 20 hadi 26, vyama hivyo vinasema wagombea wao wengi wameenguliwa, majina yao yakiwa hayaonekani. 

Kwa sasa vyama hivyo vinaendelea na mchakato wa kukata rufani ili kuhakikisha wanachama wao walioenguliwa kinyemela yanarejeshwa, watumie haki yao ya kikatiba ya kuchaguliwa.

 Vyama vinavyolalamika kufanyiwa figisu kwenye kujaza fomu hizo ni CUF, CHADEMA na ACT-Wazalendo ambapo kila kimoja kinafanya juhudi za kurudisha wagombea wao kwenye kinyang'anyiro.
 Kutokana na sintofahamu hiyo inayoendelea, baadhi ya wachambuzi na wadau wa siasa wanazungumza na Nipashe kuhusu mchakato huo.

  HUJUMA R4

 Abdulkarim Atiki ni mchambuzi wa siasa ambaye anasema mchezo wa kuengua wagombea wa upinzani ni kama mkakati wa hujuma kwa Rais Samia Suluhu Hassan ili kuyumbusha utekelezaji wa R4.
 
 "Hizo ni hujuma dhidi ya R4 za Rais Samia zinazolenga kuleta umoja wa Watanzania bila kujali itikadi za vyama. Inakuwaje wasimamizi wanakiuka kanuni? Watafakari kwa kina jambo hili," anasema Atiki.
 Anakumbusha kuwa Rais anahimiza kuunganisha Watanzania ili kuepuka mazingira yaliyotokea katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019, lakini dalili zinaonekana yatajirudia katika uchaguzi wa mwaka huu.


 "Demokrasi inatakiwa kuanzia ngazi ya chini, yaani wananchi katika kijiji wawe huru kuchagua kiongozi ambaye wanamtaka si wawekewe mgombea wasiyemtaka ndicho kinaendelea sasa, hiyo ni dhambi," anasema.
 
 Mchambuzi huyo anasema kasoro ndogo zisipewe uzito hadi kuengua mgombea ambaye wananchi wanamtaka, na kwamba aachwe agombee matokeo yaamuliwe na sanduku la kura.
 
 Atiki anasema Waziri wa TAMISEMI ambaye anasimamia uchaguzi huo aangalie uwezekano wa kusimamia haki kuepuka kutenda kosa hilo ili aruhusu wananchi wapate wagombea wanaowataka.
 
 "Mimi ni muumini wa demokrasia, ninatamani sana ushindi unaotokana na kujenga hoja majukwaani na si ushindi wa mezani ambao tayari umeanza kuonekana. Inatisha shaka kuamini kama kweli wapinzani hawajui kujaza fomu, au fomu wanazopewa wagombea wa CCM ni nyingine na wapinzani nao wanapewa tofauti  zinazowashinda kujaza? 

AIBU YA TAIFA

 Mwanaharakati ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji mstaafu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, anasema kinachoendelea katika mchakato huo ni aibu kwa taifa.
 
 Anasema ni vyema viongozi wajitokeze hadharani na kukomea vitendo vinavyoashiria kuvuruga uchaguzi wa serikali za mitaa ikiwamo kuengua wagombea wengi wa upinzani ili CCM ishinde kirahisi.
 
 "Waziri kutoka hadharani na kuwaambia walioenguliwa kuwa wakate rufani inaonyesha anajua kila kitu kinachoendelea. Kwa nini asilaani vitendo hivyo na kutoa maelekezo?” Anahoji Dk. Hellen.
 
 Dk. Hellen anasema kuwapo maeneo ambayo wasimamizi wasaidizi walifunga ofisi na kuwanyima nafasi wagombea wapinzani na wengine kukataa kupokea fomu zao bila kuchukuliwa hatua, kunaacha maswali.
 
 "Nimeona video moja wazee wakisema kuwa wanashangaa kusikia kuwa majina yao yameandikwa wakitambulishwa kuwa ni chama fulani wakati si kweli. Nani aliandika majina yao katika chama kingine?” anauliza.
 
 Mwanaharakati huyo anasema mchakato huo una kasoro nyingi ambazo anaona ni bora uwanja ungekuwa sawa kwani inaelekea bado wengine hawako tayari kuona upinzani ukiongoza.
 
 "Ifike wakati CCM iwaachie wananchi wachague viongozi wanaowataka. Mimi siamini kama kweli ndani ya upande mmoja ndiko kuna viongozi bora wasiokosea kujaza fomu au wanaojua kuongoza kuliko wengine," anasema.
 
 NI MAELEKEZO
 
 Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Magdalena Sakaya, anasema wapo baadhi ya watendaji ambao ‘rafu’ hizo zinawauma wanaamua kusema ukweli kuwa wanachofanya ni kutekeleza maelekezo bila kutaja kuwa ni ya nani.
 
 Anasema wagombea wa CCM hawana hoja badala yake wanategemea kubebwa na maelekezo ambayo yametekelezwa karibu kila kona ya nchi na kusababisha wapinzani wengi kuenguliwa.
 
 "Katika mchakato huu wametafuta sababu wamekosa wakaamua kubadili majina ya watu. Mfano kuna mgombea wetu anaitwa Mohamed Salum, aliteuliwa, lakini baada ya siku chake akapigiwa simu kuwa ameenguliwa kwa sababu amekosea kuandika jina.

Anaambiwa kuwa badala ya Salum ameandika Saluma. Yaani kule mwisho waliongeza herufi ‘a’," anasema Magdalena.
 
 Anakumbusha kuwa chama chao kilianza kupiga kelele tangu mchakato wa kuandikisha wapigakura, kuchukua fomu na kurejesha, na kwamba hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.
 
 "Kwa kuwa kauli za TAMISEMI zimekuwa ni za kawaida, mimi niwaombe viongozi wakuu wa nchi wajitokeze hadharani na kukemea vitendo hivi ambavyo vinatibua R4 za Rais," anasema.
 
 Aidha, Magdalena anaitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa isiendelee kukaa kimya badala yake iingilie kati kama mlezi wa vyama hivyo ili upinzani usiendelee kulalamika katika mchakato huo.
 
 Wakati kukiwa na sintofahamu, Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, ameshatoa maelekezo ya kuwataka wagombea walioenguliwa wakate rufani na kwamba zitasikilizwa kwa haki.