"KUOA tunaona lakini tukumbuke yaliyotendeka kwa George Mukabi, George alipooa bibi akakimbia, kwa kumfuata akauawa bure. Wazazi wa Mukabi walipata hasara, kupoteza mali na mtoto wao, wale ambao hatujaoa kweli ndugu zangu, tukifikiri hilo hatutaoa tena."
Haya ni mashairi ya wimbo uitwao 'Kifo cha Mukabi', ambao ulitungwa na kuimbwa na mwanamuziki John Mwale kutoka nchini Kenya.
Alitunga wimbo huo ulio kwenye mtindo wa 'twist' mwanzoni tu mwa mwaka 1960, kufuatia kifo cha kiunyama cha mwanamuziki mwenzake, George Mukabi.
Mukabi alikuwa mwanamuziki maarufu, siyo nchini Kenya tu alikozaliwa, hata nchini Tanzania ambapo alikuwa na mashabiki lukuki kutokana na nyimbo zake kali kugusa watu wengi wakati huo.
Kifo chake sio tu kwamba kilileta pigo kwa mashabiki wa muziki Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, lakini kilileta taharuki kubwa kutokana na mazingira yenyewe.
Utakumbuka kuwa wakati huo teknolojia haikuwa kubwa sana miaka ya 1950 hadi 1970, na nyimbo hizo zilipatikana kwenye santuri au sahani ambazo zilijulikana kama GV.
Ni miaka ambayo nyimbo za wanamuziki hao zilipigwa kwa magitaa baridi, yaani yasiyotumia umeme, maarufu kama 'magalatoni' zikihamishwa mapigo ya chupa, ngoma, au manyanga, mbao, au bati ili kunogesha muziki. Hakukuwa na nyombo vingi.
Pamoja na hayo wanamuziki wa enzi hizo walikuwa mahiri sana, kwani pamoja na uduni kwa vyombo, waliweza kurekodi nyimbo mbalimbali zilizokuwa kwenye santuri ambazo zilivuma na kupendwa sana Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Congo ya Kibelgiji, sasa Jamhuri ya Kidemokrasi cha Congo, kulikuwa na wanamuziki waliopendwa mno nchini wao na nyimbo zao kama Jean-Bosco Mwenda wa Bayeke, Edward Masengo, Losta Abelo, Uganda mwanamuziki aliyekuwa maarufu Bongo ni Charles Sonko na dada yake Frida Sonko, nchini Zambia kulikuwa na Nashil Pitchen na Peter Tsosi, huku Kenya kulikuwa na kina Daudi Kabaka, John Zenze, John Mwale, Fadhili William, akiwemo pia Mukabi.
Mkenya huyo alizaliwa 1930 na kuuawa mwaka 1963 akiwa bado kijana tu wa miaka 33 na tayari alikuwa ameshaanza kupata mafanikio kwenye karia yake ya muziki.
Ulivuka mipaka ya Kenya na kuwa na mashabiki wengi nchini Tanzania, huku nyimbo zake maarufu ambazo zimeendelea kupendwa hadi leo hii ni 'Sengula Nakupenda', 'Kweli Ndugu' na 'Mtoto Si Nguo'.
Kabla ya kuelezea kisa kizima kilichosababisha kukatishwa nyota, hebu tuangalie mashairi ya nyimbo zake tatu ambazo ndizo zilizokuwa ziki
"Sengula ninakupenda, si nikuwa napenda, Sengula we kweli Sengula wangu, si nilikuwa nakupenda?
Ni vizuri tupendane, nyumba ikawa na heshima, Sengula we kweli Sengula wangu si nilikuwa nakupenda.
Ninachoka na mambo yako, Sengula we kweli Sengula wangu si nilikuwa nakupenda."
Huu ndiyo wimbo bora zaidi na ulikuwa ukimtambulisha mwanamuziki huyo na kumpatia sifa na aliuza nakala nyingi mno.
"Mtoto si nguo utaomba mtu, ukikosa mtu baba, ukikosa wako utalia sana baba. George mwamba sina wangu mie, nakosa wangu ee ninalia sana baba." Nao ulipendwa sana nchini Tanzania na kufuatia ule wa 'Kweli Ndugu"
"Kweli wangu sikilizeni niwambieni, kwa kuoa nilikooa bibi mmoja mrembo, sasa kaleta hasara kuvunjavunja vikombe, kuvunja vunja sahani.
Na wandugu wangu wote walikataa, walisema afunge aende, hatutaki hasara, avunjavunja vikombe, avunjavunja sahani."
Alitunga na kuimba nyimbo nyingi sana kwa muda mfupi tu wa maisha yake, lakinbi hizo tatu zilitia fora sana hasa nchini Tanzania.
Kifo chake kilikuwa na uvumi mwingi, ikiwemo kuwa alioa mke, baada ya siku chache mke akakimbia akarudi kwao, akaamua kumfuata na huko akauawa na hawara wa mkewe.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi nchini Kenya baada ya kufanya uchunguzi wake liligundua kuwa kisa cha kifo chake hiki.
Baada ya kupiga muziki wake kwenye Jiji la Nairobi alirejea kwao Kakamega na kufikia nyumbani kwa mke mdogo. Akaweka gita lake na kumwambia anakwenda kulala kwa mke mkubwa. Mke mdogo wivu ukamshika, pia akadhani kuwa pesa zote alizopata kwenye muziki atakwenda kupewa mke mkubwa.
Wakati yupo nje anaondoka, mke mdogo kwa hasira akaamua kuchukua gitaa la mumewe na kulivunja. Ikumbukwe lilikuwa ni gitaa jipya kabisa la kisasa wakati huo ambalo alipewa na rafiki yake raia wa Uingereza.
Aliposikia kama kuna sauti za kuvunja kitu, akarejea na kukuta gita lake linevunjwa. Mke akaamua kukimbilia kwao . Mukabi kwa hasira na yeye akamfuata. Mke alipofika kwao akakimbilia moja kwa moja chumbani kwa baba yake. Mukabi akaingia humo humo. Baba mkwe alikuwa nje na aliona timbwili lile. Bila kufikiria akaanza kupiga yowe kuita majirani wamsaidie. Wanakijiji wao walipofika hawakuuliza, wakaanza kumpiga Mubaki kwa mapanga, mawe, rungu shoka na kila aina ya silaha za jadi. Binfasi nina wasiwasi labda aliita kelele za mwizi. Ilikuwa ni usiku.
Kwa kujaribu kujiokoa akakimbia na kuvuka mto Yala, lakini hakuweza kufika mbali, aliishiwa nguvu akaanguka na kuzimia.
Bado wanakijiji wao wa Bososo waliendelea kumkimbiza na walipomkuta wakamalizia kwa mawe, kabla kumkatakata vipande kama nyama. Sehemu ya mwili wake wakaipakia kwenye mkokoteni na kuipeleka kwenye hospitali ya Kakamega.
Lilikuwa ni tukio la kusikitisha sana. Mwanamuziki mmoja wa Kenya naye alitunga wimbo wa kuwashutumu wanajiji hao akaimba. "Watu wa Busoso walimkata George kama mti."
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED