ELON MUSK: Ni bilionea anayelipa wapigakura Marekani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:38 AM Oct 23 2024

Elon Musk akizungumza jijini Pennsylvania.
PICHA: REUTERS
Elon Musk akizungumza jijini Pennsylvania.

BILIONEA namba moja duniani Elon Musk, anamwaga dola kama njugu kwa wanaojiandikisha kupiga kura, akitoa Dola 1,000,000 kila siku kwa anayeshinda kupitia bahati nasibu.

Maswali yanaibuka kuhusu uhalali wa pesa za bilionea huyo wa teknolojia kwa wapigakura wa majimbo mbalimbali wanaotia saini ombi lake  la America PAC, kabla ya uchaguzi wa Marekani unaofanyika Jumanne  Novemba 5, 2024.

Ni ombi la kampeni la Musk la America PAC,  lilianzishwa  kumuunga mkono Donald Trump katika kinyang'anyiro cha urais.

Lakini, wataalamu wa sheria wanasema huenda hilo linavunja sheria ya Marekani kutoa pesa kwa mtu aliyesajiliwa kama mpigakura.

PAC inawahimiza wapigakura wa majimbo  ya  Georgia, Nevada, Arizona, Michigan, Wisconsin na North Carolina kusaini kuunga mkono uhuru wa kujieleza na haki ya kubeba silaha.

Aidha, wale wanaoleta mpigakura atakayesaini hupokea Dola  milioni  47. Kiasi cha juu ni dola milioni 100 kwa kusaini au kumleta mtu wa kusaini hutolewa huko Pennsylvania, jimbo ambalo ni uwanja wa vita kati ya Trump na Harris na kura zao huko zinaaminiwa zinaweza kuamua mshindi wa mwisho.

Amerika PAC inasema wale wanaotia saini ombi hilo wanaashiria kuunga mkono kifungu cha kwanza na cha pili cha katiba ya Marekani.

Kila siku hadi Novemba 5, zawadi ya dola milioni 1 itatolewa katika mfumo wa bahati nasibu kwa yeyote aliyetia saini mojawapo ya majimbo saba. 

"Naamini pesa ya Musk inaweza kuwa ni kinyume cha sheria," anasema Paul Schiff Berman, profesa wa sheria wa Chuo Kikuu cha George Washington.

Kanuni za Marekani kuhusu sheria ya uchaguzi, inasema mtu yeyote "anayelipa au kujitolea kulipa au kukubali malipo - kwa ajili ya kujiandikisha kupiga kura au kupiga kura" anaweza kutozwa faini ya dola 10,000 au kifungo cha miaka mitano jela.

"Pesa zake ziko kwa ajili ya wapigakura waliojiandikisha tu, kwa hivyo nadhani anakwenda kinyume na sheria hii," anasema Berman.

Idara ya Sheria ya Marekani ilikataa kutoa maoni. 

 “Hoja ya kuvunja kanuni inaweza kuwa dhaifu, kwa sababu hakuna anayelipwa moja kwa moja ili kujiandikisha au kupiga kura,” anasema mwenyekiti wa zamani wa Tume ya Shirikisho ya Uchaguzi (FEC), Brad Smith.

"Hawalipi watu kujiandikisha kupiga kura. Anawalipa ili kutia saini ombi lake, anataka waliojiandikisha tu kupiga kura, kutia saini ombi hilo. Kwa hiyo nadhani yuko sawa hapa,” anasema.

Lakini profesa wa sheria za uchaguzi katika Chuo Kikuu cha Northwestern aliiambia BBC lengo la pesa hiyo kutolewa ni muhimu.

"Naelewa kwa baadhi ya wachambuzi kuwa sio kinyume cha sheria, lakini lengo moja liko wazi, kushawishi watu kujiandikisha kupiga kura kwa njia ambayo ina shida kisheria," anasema Michael Kang.

Adav Noti kutoka kituo cha Campaign Legal Center, anasema mpango wa Musk "unakiuka sheria ya shirikisho na uko chini ya kosa la kiraia au jinai kwa mujibu wa Idara ya Haki." 

"Ni kinyume cha sheria kutoa pesa kwa masharti kwamba wapokeaji wawe wamejisajili kama wapiga kura," anasema Noti.

Profesa wa sheria za katiba Jeremy Paul, kutoka Chuo Kikuu cha Northeastern anasema katika barua pepe kwa BBC kwamba Musk anatumia mwanya wa kisheria.

Ingawa kuna hoja kwamba pesa hizo zinaweza kuwa kinyume cha sheria, “lakini zinatolewa kwa mtindo wa kuizunguka sheria" na anaamini kesi hiyo itakuwa ngumu mahakamani.

Musk, bilionea mfuasi kindaki ndaki wa rais wa zamani Donald Trump, alitangaza Jumamosi iliyopita kuwa atatoa dola milioni moja kila siku hadi uchaguzi ufanyike kwa mpiga kura wa jimbo moja ambaye bahati nasibu ikichezeshwa itamwangukia .Utoaji wa fedha hizo kutoka kwa mtu tajiri zaidi duniani ni jambo ambalo halijawahi kutokea kwa miaka mingi nchini humo.

Musk alitangaza tuzo za kila siku ya dola milioni katika mkutano wa hadhara wa Trump huko Harrisburg na  Pennsylvania, Jumamosi iliyopita na siku hiyo  mshindi wa kwanza akatangazwa kuwa ni  John Dreher.

Wapigakura wanaweza kufanikiwa kupata zawadi kwa kusaini ombi la kuunga mkono uhuru wa kujieleza au wa maoni na haki ya kumiliki na kubeba silaha inayoendeshwa na Musk's America PAC. Ni kampeni inayotumia mamilioni kumuunga mkono Trump  ikiwa ni pamoja na kugharamia ziara za nyumba kwa nyumba katika majimbo ambayo yanaonekana kuwa yeyote kati ya Donald Trump wa Republican na Kamala Haris wa Democrat anaweza kushinda . Marekani wakiyaita ‘swing states’. Wapigakura katika majimbo ya Pennsylvania wangepokea  dola milioni Jumapili na Jumatatu, na katika siku 15 zijazo watu waliotia saini PAC ambayo inasisitiza uhuru wa maoni na kumiliki silaha wa majimbo ya Pennsylvania, Georgia, Nevada, Arizona, Michigan, Wisconsin na North Carolina watafuata kupokea chao. Wakili wa masuala ya uchaguzi Rick Hasen,  anasema katika  blogu yake kuwa mpango wa hivi  sasa wa Musk ni kinyume cha sheria, akisema kuwa unakiuka sheria ya shirikisho inayopiga marufuku "kulipa au kutoa,  ama kulipa au kukubali malipo kwa kusajili kupiga kura. Tena ni kinyume cha sheria. Gavana wa Democrat wa Jimbo la Pennsylvania, Josh Shapiro, anamkosoa Musk na zawadi hiyo, akisema bilionea huyo ana haki ya kutoa maoni yake, "lakini anapoanza kuingiza aina hii ya kugawa pesa katika siasa, ni jambo linalozua maswali mazito ambayo watu lazima waangalie.

Mwekezaji bilionea Mark Cuban, ambaye amefanya kampeni katika wiki za hivi karibuni kwa Kamala Harris, anasema:

"Ikiwa mpango huo utafanya kazi au la ni jambo jingine. Na mpango huo unaweza hata kukupa matokeo tofauti na uyatakayo," aliiambia CNBC.

Musk amejibu ukosoaji huo, akisema Democratic na wafadhili wao wamefadhili mipango kama hiyo hapo awali.

Kwenye mtandao wa X au twiter, aliweka chapisho linalosema bosi wa Meta, Mark Zuckerburg" alifanya vivyo hivyo mwaka 2020."

Zuckerburg alichangia dola milioni 400 katika uchaguzi wa 2020 lakini pesa hiyo ilitolewa kwa mashirika mawili yasiyoegemea upande wowote ili kusaidia vifaa vya upigaji kura kwa njia ya posta. Haikutolewa moja kwa moja kwa wapigakura.

Huko nyuma Democratic, kiliwahi kuwekeza katika mipango ya kuongeza wafuasi, kwa kampeni ya usajili wa wapigakura ya dola milioni 25 katika uchaguzi wa katikati ya muhula wa Marekani wa 2022.

Lakini pesa hizo hazikutolewa moja kwa moja kwa wapiga kura. Zilikuwa ni za mipango ya kuwahimiza wapigakura kujiandikisha na zilitolewa kwa  walioajiriwa kwenye kampeni za  nyumba kwa nyumba, na kwa matangazo ya televisheni na mtandaoni.

"Ni halali kuwalipa watu kwenda kusajili wapiga kura, lakini huwezi kuwalipa watu moja kwa moja kujiandikisha," anasema Prof. Kang.

 

BBC SWAHILI, FORBES