DUNIA ya sasa kila jambo linafanyika kielektroniki likipewa nguvu na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Teknolojia hiyo inahusisha zana na nyenzo za kiufundi zinazotumiwa kuunda, kuhifadhi, kushiriki (share) na kusambaza taarifa ambazo hutegemea kompyuta, mitandao, programu, intaneti, simu za mkononi na mikutano ya video
Zama hizi TEHAMA ni kila kitu anatumiwa karibu kwenye kila eneo, shuleni hadi vyuoni viwe vya kati hadi vikuu. Tiba, usafiri, kilimo, viwandani na utoaji wa huduma.
Pia TEHAMA inarahisisha shughuli za masomo ikiwamo kufundisha na kujifunza. Kutokana na umuhimu wa teknolojia hiyo, Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) kilichoko Mara kiko mbioni kujenga Shule Kuu ya TEHAMA katika kampasi zake.
Shule hizo za TEHAMA zinatarajiwa kujengwa kampasi kuu ya Butiama na Tabora ikiwa ni sehemu ya mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya MJNUAT.
Katika ziara ya kutembelea na kukagua ujenzi wa mindombinu ya MJNUAT, Makamu Mkuu wa chuo, Profesa Lesakit Mellau, hivi karibuni anaueleza ujumbe wa baraza la chuo, unaozuru chuo kikuu kuwa wameingia mkataba wa ujenzi wa shule hizo.
Anawafafanulia wajumbe wanaoongozwa na Profesa Roberta Malee wa Benki ya Dunia(WB), aliyeambatana na wadau wengine wa elimu wakiwamo wengine kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
“Chuo kimepata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mchanganyiko katika kampasi kuu Butiama na kusaini mkataba wa miezi 10 na kampuni ya China kukamilisha kazi hiyo, " Profesa Mellau anasema.
Anaongeza kuwa mkataba huo wenye thamani ya Sh. bilioni tisa ulifanyika katika kampasi kuu Butiama na kushuhudiwa na watu mbalimbali akiwamo Mkuu wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi na mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu Philemon Luhanjo.
Anafafanua kuwa mkataba huo utahusisha ujenzi wa barabara za ndani ya chuo, mifumo ya majitaka na ya kusambaza maji safi, lango kuu la chuo, sehemu ya kuweka taka na tanuru la kuzichoma na miundombinu ya michezo.
Vilevile, wiki iliyopita chuo kiliingia mkataba wa ujenzi wa Shule Kuu ya TEHAMA na biashara katika kampasi za Tabora na Butiama chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) , mkopo kutoka Benki ya Dunia kwenda serikalini.
Aidha, anasema chuo kimeanza kupokea wanafunzi wa mwaka wa kwanza tangu mwezi uliopita ( kuanzia Oktoba 30).
Profesa Mellau anasema ujenzi wa chuo utakapokamilika, kitadahili wanafunzi hadi 4,500 kwa kampasi kuu, 600 katika kampasi ya Oswald Mang’ombe na wanafunzi 1,500 kwa kampasi ya Tabora na kinatarajiwa kuwa na watumishi 700.
"Tunashirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia, Benki ya Dunia na taasisi nyingine za elimu ya juu kuusimamia mradi huu ili ukamilike kwa wakati,” anasema.
Anaongeza kuwa chuo hicho ni miongoni mwa taasisi 23 zinazonufaika na Mradi HEET ambao ni mkopo kutoka WB kwa serikali.
MAADILI MEMA
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha MJNUAT, Philemon Luhanjo, anawataka watumishi wa chuo hicho kuzingatia maadili mema.
Anasema hayo wakati akizungumza na wanataaluma wa chuo hicho, katika kampasi ya Oswald Mang’ombe, Butiama kwenye ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu MJNUAT.
Luhanjo anasema kilianzishwa ili kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na kwamba maadili ni jambo la muhimu kwa watumishi na wanafunzi wa chuo hicho.
“Ni lazima tuonyeshe taswira inayofanana na Mwalimu Nyerere. Chuo hiki ni maalumu na kimekuja kuwekwa katika kijiji chake. Muitunze heshima ya Mwalumu Nyerere,” anasema Luhanjo.
Katibu Mkuu kiongozi mstaafu anasema ni muhimu kulinda taswira ya chuo hicho na kuepusha mazingira yatakayowafanya watu wakiseme vibaya.
"Sisi tujitahidi kukijenga na kukiimarisha ili tuweze kutengeneza taswira ile inayotakiwa au zaidi. Kwa hiyo suala la maadili, kwa maana pana – ninyi wenyewe (watumishi), wanafunzi kwa wanafunzi, walimu kwa wanafunzi, walimu na wanafunzi na jamii inayowazunguka, muwe na mahusiano mazuri," anasema.
FURSA KEDEKEDE
Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi anasema uwepo wa chuo hicho Butiama, umeleta fursa nyingi za uwekezaji na kuwataka wakazi wa mkoa huo na maeneo mengine kuchangamikia fursa hiyo.
“Niwaombe wananchi wa mkoa wa Mara na Watanzania kuchangamkia fursa ya kuanzishwa kwa chuo hiki kuwekeza katika biashara mbalimbali zitakazokuwa zinahitajika kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi na watumishi," anasema Kanali Mtambi.
Kanali Mtambi anafafanua kuwa wawekezaji wanaweza kufungua maduka kulingana na mahitaji ya wanafunzi, watumishi wa chuo na watu wengine wanaoishi maeneo ya jirani na chuo.
Aidha, uamuzi wa serikali kukifanya chuo hicho kibebe sehemu ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wake ili kuleta mapinduzi makubwa ya kijamii na kiuchumi katika mkoa huo.
"Chuo hiki kinasadifu shabaha halisi ya kumuenzi Baba wa Taifa, mkoa wetu tunaishukuru serikali kwa maamuzi haya ya ya kujenga chuo hiki mkoani Mara ukiwa mmoja kati ya miradi mikubwa kitaifa," anasema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED