HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, leo, imeanzisha Kitengo cha Kuhifadhi na Kuratibu Maziwa ya Mama (Lactational Management Unit), kuhakikisha watoto njiti wanapata maziwa ya mama zao kwa wakati.
Aidha, wataalam wa afya nchini wamesisitizwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kupigania maisha ya watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda, ili kupunguza vifo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi, amesema hayo leo, wakati akifungua maadhimisho ya kuelekea siku ya mtoto aliyezaliwa kabla ya muda (njiti) yaliyofanyika katika MNH–Mloganzila.
Alisema lengo ni kufikia mkakati uliowekwa ifikapo mwaka 2030, vifo vya watoto wachanga kuwa chini ya vifo 12 katika kila vizazi hai 1,000 .
Prof. Janabi ameeleza hay oleo, Dar es Salaam, akisema kwamba kwa kila watoto 1000, kuna watoto wachanga wapatao 24 wanaofariki ndani ya siku 28 za kwanza na kwamba mikakati ya kupunguza vifo hivyo haiwezi kuwa endelevu, bila kushirikiana wadau katika sekta ya afya na kuboresha ujuzi wa kuhudumia watoto hao.
Amefafanua kuwa serikali kupitia Wizara ya Afya, imekuwa ikiratibu progamu mbalimbali ambazo lengo lake ni kupunguza vifo vya watoto wachanga na walio chini ya miaka mitano, program hizo ni kama kumsaidia mtoto kupumua baada ya kuzaliwa, kupanua huduma za watoto wachanga kwa kujenga wodi za watoto wachanga hospitali za mikoa na wilaya na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ya namna ya kuhudumia watoto wachanga.
Bingwa Bobezi wa Watoto Wachanga MNH, Dk. Martha Mkony, amesema katika Afrika takribani mtoto mmoja kati ya 10, huzaliwa kabla ya wakati na watoto hao hukabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile matatizo ya kupumua, maambukizi na hatari za ukuaji kwa muda mrefu.
“Hata hivyo pamoja na kuwapo kwa changmoto hizo, lakini bado kuna matumaini kupitia juhudi za serikali, kwani kuna maboresho ya kutia moyo katika utunzaji wa watoto wachanga nchini kwa kuboresha vituo vya afya na hospitali za kuhudumia watoto wachanga na kujengwa pamoja na kusomesha wataalam wa afya,” ameeleza Dk. Mkony.
Maadhimisho hayo yameenda sambamba na uzinduzi wa Kitengo cha Kuhifadhi na Kuratibu Maziwa ya Mama (Lactational Management Unit), kwa kuhakikisha watoto hao wanapata maziwa ya mama zao kwa wakati kwa kuWa watoto wanaozaliwa kabla ya muda wanakuwa na uzito mdogo unaosababisha kuhitaji kiasi kidogo cha maziwa.
“Mama ana uwezo wa kutoa maziwa mengi kiasi kinachobaki kinahifadhiwa, hivyo ni rahisi mama akiruhuisiwa kurejea nyumbani anakwenda na maziwa yake. Hii inasaidia mpango wa kuhakikisha watoto wachanga wanayonyeshwa miezi sita bila kupewa chochote.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED