Watetezi Haki za Binadamu wajifungia kuja na tamko utekaji watoto

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 05:15 PM Jul 25 2024
Mratibu wa Mtandao huo Taifa, Onesmo Ole Ngurumwa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mratibu wa Mtandao huo Taifa, Onesmo Ole Ngurumwa.

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), wameanza Mkutano Mkuu wa Wawakilishi wa Kanda za Ziwa Magharibi na Mashari lengo likiwa ni kujadili na kubaini hali ya utekelezaji wa shughuli za utetezi wa haki za binadamu sambamba na changamoto wanazokumbana nazo.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano huo mapema leo, Mratibu wa Mtandao huo Taifa, Onesmo Ole Ngurumwa amesema wanatarajia kubaini na kufikia muafaka juu ya namna sahihi ya  kushughulikia matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini.

Amesema pamoja na mambo mengine Waratibu pamoja na Wajumbe wa Kanda hizo wanatarajia kujadili na kuja na tamko la pamoja kuhusu hali ya ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na tishio la kutekwa kwa watoto linaloendelea nchini.

“Tutapata kujua yale wanayopitia katika utekelezaji wa kazi zao sambamba na wao kama watetezi wa haki za binadamu wataeleza juu ya tatizo la utekaji wa watoto na wajibu wa jamii pamoja na vyombo vya usalama katika kukabiliana na tatizo hili,”amesema Ngurumwa.

1

Mratibu wa Kanda ya Ziwa Mashariki Sophia Donald, amesema tatizo la utekaji wa watoto halipo tu kwa Mkoa wa Dar es Salaam bali hata katika mikoa ya kanda ya ziwa yamekuwa yakitokea kila uchwao lakini hayaripotiwi na hatua hazichukuliwi.

“Mfano kwa Mkoa wa Geita watoto wanatekwa na kuuawa kwa wingi wakihusisha masuala hayo pamoja na shughuli za uchimbaji madini hivyo upo umuhimu wa kuja na mikakati ya kudhibiti kabisa vitendo hivi,”amesema Sophia.

Naye Mratibu wa Kanda ya Ziwa Magharibi, Madaga Joseph amesema kupitia mkutano huo wanatarajia kuja na mbinu muhimu ya kudhibiti vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa uwakilishi katika maeneo ambayo hayajafikiwa.