Walimu, Wanafunzi kortini tuhuma wizi wa mitihani

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 04:12 PM Jul 25 2024
Waalimu, Wanafunzi kortini tuhuma wizi wa mitihani.
Picha: Shaban Njia
Waalimu, Wanafunzi kortini tuhuma wizi wa mitihani.

WALIMU pamoja na wanafunzi wa shule ya Sekondari Lunguya iliyopo Halamshauri ya Msalala mkoani Shinyanga, akiwemo Muunguzi wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kahama kwa kuhusika katika wizi wa mitihani ya kidato cha nne iliyofanyika Novemba 2023.

Washtakiwa hao ni pamoja na Muuguzi, Lucy Justin Maganda (39) mwanafunzi aliyekuwa akirudia mitihani, Ovan Leopold Katunzi (54) mwalimu, Jacob Costantino Daniel (36) Mwalimu, Ramson Musa Kanyenyemo (35) Mwalimu pamoja na Paschal Cyprian Buchanagandi (21) mwanafunzi aliyekuwa akirudia mitihani katika Shule ya Sekondari Lunguya.

Mwendesha mashtaka wa serikali, Jukael Jairo alidai washtakiwa hao walitenda kosa la jina namba 20975/2024 kinyume cha sheria ya baraza la mitihani sura namba 107 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019 kwa kuvujisha mitihani ya kidato cha nne iliyofanyika Novemba 15 mwaka jana.

Amesema, kosa la kwanza linawahusu wanafunzi wawili waliokuwa wakirudia mitihani ya kidato cha nne kwa kukutwa na nyaraka zisizohitajika katika chumba cha mitihani kinyume na kifungu cha sheria namba 20(2) na kifungu cha 24(1)(2) cha sheria ya baraza la mitihani sura namba 107 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

Kosa la pili linawahusu walimu watatu wa sekondari ya Lungu iliyopo Halmashauri ya Msalala kwa kuvujisha mitihani wa somo la Jogorafia kwa wanafunzi wakati mitihani ikiendelea kinyume na sheria ya baraza la mitihani sura namba 107 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

1

Huku kosa la tatu linamhusu mshtakiwa namba mbili ambaye ni Ovan Katunzi mwalimu kwa kushindwa kutunza au kulinda karatasi za majibu ya mtihani wa Jogorafia na upelelezi wa shauri hilo umekamilika na kuomba kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa kwa shauri hilo.

Hakimu mkazi wa Wilaya ya Kahama Christina Chovenye alitoa masharti ya dhamana kwa washitakiwa wote ambayo ni kuwa na wadhamini wawili, mmoja akiwa mtumishi wa umma, wakiwa na bondi ya thamani ya Sh. Milioni tano pamoja na kitambulisho cha Taifa (NIDA).

Hata hivyo washtakiwa wote watano walikana mashtaka yao na kushindwa kukidhi masharti ya dhamana na kurejeshwa mahahabu hadi Agosti 7 mwaka huu ili kuendelea kusikilizwa kwa shauri hilo.