UN Women: Mabalozi wanawake bado wachache

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 03:00 PM Jun 26 2024
Balozi Getrude Mongella, akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake katika Diplomasia.
Picha:Mtandao
Balozi Getrude Mongella, akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake katika Diplomasia.

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wanawake (UN Women), limesema bado kiwango cha wanawake mabalozi na wawakilishi wa kudumu ni kidogo duniani ikiwa ni asilimia 21 kati ya nchi 193.

Naibu Mwakilishi Mkazi wa UN Women Nchini, Katherine Gifford, alisema hayo katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake katika Diplomasia, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mabalozi kadhaa wanaoziwakilisha nchi zao nchini.

Alisema wakati Tanzania angalau imefikia usawa kwenye uongozi, bado uwiano wa uongozi ni mdogo duniani na itachukua takribani miaka 40 kufikia hatua hiyo.

“Wakati maendeleo yamepatikana Tanzania na mengine mengi, uwiano wa kimataifa wa wanawake katika ofisi za kisiasa uko chini katika usawa, kwa kasi ya sasa ya maendeleo inakadiriwa bado uwakilishi bungeni hautapatikana hadi 2062.

“Katika diplomasia hadi mwaka 2023, wanawake ni asilimia 21 tu ya mabalozi na wawakilishi wa kudumu duniani kote. Hii inadhihirisha kwamba, bado tuko mbali na usawa katika nyadhifa za juu za kidiplomasia. Marais wanawake ni 34 tu duniani katika nchi wanachama 193.

“Kati ya nchi 193 wanachama wa UN, ni wanawake 34 pekee wanaohudumu kama wakuu wa nchi au serikali waliochaguliwa,” alisema Katherine.

Alisema matumaini ni kwamba, mkutano huo utajikita kujadili changamoto za kipekee wanawake wanazokabiliana nazo na kujenga mazingira jumuishi, ili kusaidia kupanda kwenye nafasi za uongozi.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Riziki Pembe Juma, alisema mafanikio yapo nchini ikiwamo kuhakikisha elimu kwa wote, bila kumuacha msichana nyuma.

“Tumeimarisha huduma ya afya mama na mtoto, kuwezesha wanawake kiuchumi. Tanzania ndio ushahidi wa kwanza kwamba, tunasimamia usawa wa kijinsia na kufikia malengo la kidunia katika kuweka wanawake kwenye uongozi kuhakikisha sauti za wanawake zinawakilishwa,” alisema.

Alisema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan pia, inatekelezwa mradi ya kupikia nishati safi, ikiwekeza Sh. bilioni 2.2 ili kuinua jamii hususan wanawake ambao ndio wahusika wakuu wa kupika.