Azam yakana Kipre kutaka kuondoka

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 07:43 AM Jun 29 2024
Kipre Junior.
Picha: Azam FC
Kipre Junior.

LICHA ya kuibuka tetesi za mchezaji wake Kipre Junior kuhusishwa kutakiwa na klabu ya USM Alger ya Algeria, uongozi wa Azam FC umesema haujapokea ofa yoyote inayomuhusisha mchezaji huyo.

Aidha, wameenda mbali na kudai wapo katika kuboresha kikosi chao kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na hawataruhusu wachezaji wao tegemezi kuondoka.

"Hiki ni kipindi cha usajili, tetesi nyingi zitasikika, kuhusu Kipre huyu bado ni mchezaji wetu na tupo kwenye malengo yetu msimu ujao," alisema Zaka Zacharia, Ofisa habari wa klabu hiyo alipoulizwa juu ya tetesi hizo.

Hata hivyo alisema soka ni biashara kama kuna timu inamtaka mchezaji huyo au mchezaji mwingine yeyote basi wawasilishe ofa zao kwa uongozi.

"Kama kuna timu inamtaka Kipre basi wanatakiwa kuwasiliana na Azam FC, mpaka sasa tunapoongea hakuna ofa yoyote ya ndani au nje ya nchi inayomtaka mchezaji huyu, hizo ni tetesi tu," alisema Zaka.

Aidha, alisema Azam hawatakuwa tayari kuruhusu wachezaji wake tegemeo waondoke kiragiisi kwa kuwa malengo yao ni kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao.

Msimu ujao Azam FC itaungana na Yanga kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kumaliza ligi kwenye nafasi ya pili.