Simba Day kuvunja rekodi msimu huu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:27 AM Jun 29 2024
news
Picha: Mtandao
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally.

UONGOZI wa klabu ya Simba umetangaza rasmi siku ya kilele cha tamasha lake la kila mwaka maarufu 'Simba Day' ambapo msimu huu limepangwa kufanyika Agosti 3 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa huku wakipanga kuvunja rekodi za matamasha yaliyopita.

Klabu hiyo itatumia tamasha hilo kuwapa 'suprise' mashabiki wao kwenye utambulisho wa wachezaji wao wapya watakaounda kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema kilele hicho kitafuatiwa na wiki nzima ya wanachama na mashabiki kufanya kazi za kijamii maeneo mbalimbali nchini kabla ya wote kujumuika Uwanja wa Mkapa kwenye siku ya kilele, ingawa hakutaja timu ambayo itacheza na kikosi hicho.

Tamasha hilo la kila mwaka linawakutanisha wanachama na mashabiki wa Simba ambao pamoja na mambo mengine ya burudani ya muziki na ngoma kutoka kwa wasanii mbalimbali pia kutakuwa na mechi za timu za vijana na za wanawake. Pia kutumia tamasha hilo kutangaza kikosi kipya kwa ajili ya mashindano mbalimbali na baadae kumaliza tamasha hilo kwa mchezo wa kimataifa wa kirafiki kati ya kikosi cha Simba na timu alikwa.

"Tungependa kutoa taarifa kwa Wanasimba wote kuwa tarehe rasmi ya tukio letu kubwa la Simba Day  itakuwa  Agosti 3 mwaka huu, Uwanja wa Benjamin Mkapa hapa hapa  Dar es Salaam.

"Tumeamua kutangaza mapema ili watu wanaokuja kutoka mataifa mbalimbali ya nje waanze kukata tiketi mapema, unajua Simba Day huwa inaleta watu kutoka maeneo mengi duniani, ikumbukwe msimu uliopita tiketi ziliisha siku mbili kabla ya kilele chake, haijawahi kutokea, sasa safari hii tunataka rekodi ivunjwe," alisema Ahmed.

Alisema mashabiki wa timu hiyo watapata 'suprise' mbalimbali katika usajili wa timu hiyo msimu huu huku pia wakipanga kuwa na burudani za aina yake zitakazowafurahisha mashabiki wao.

Tamasha hilo litakuwa la 25 kwa klabu hiyo kubwa  tangu walipobuni na kulifanya kwa mara ya kwanza mwaka 2009 chini ya Mwenyekiti wa Klabu hiyo wakati huo, Hassan Dalali, ambapo sasa imekuwa ni utamaduni wao kufanya tamasha hilo.

Miaka michache baada ya kuanzisha tamasha hilo, klabu nyingine nazo zilianza kufanya matamasha yao.

Katika tamasha la kwanza mwaka 2009, Simba ilicheza mechi kirafiki na klabu ya SC Villa ya Uganda kwenye Uwanja wa Uhuru na  ikashinda bao 1-0 lililofungwa na Hilary Echessa, kiungo wa Kenya aliyekuwa amesajliwa msimu huo, timu ikiwa chini ya kocha Mzambia, Patrick Phiri.

Ni msimu huo Simba ilikuwa imewasajili kwa mara ya kwanza wachezaji wawili raia wa Uganda, Emmanuel Okwi na Joseph Owino.

Tamasha la msimu uliopita lilifanyika Agosti  6, Uwanja wa Benjamin Mkapa Simba ikicheza dhidi ya Power Dynamos ya Zambia na kupata ushindi wa mabao 2-0 yaliyowekwa wavuni na Willy Onana na Fabrice Ngoma ambao nao walikuwa wachezaji wapya katika kikosi hicho.