Wanufaika TASAF wapanda mikoko 200,000 kunusuru mazingira baharini

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 12:44 PM Jun 28 2024
Wanufaika TASAF wapanda mikoko  200,000 kunusuru mazingira baharini.
Picha: Julieth Mkireri
Wanufaika TASAF wapanda mikoko 200,000 kunusuru mazingira baharini.

WANUFAIKA 29 kati ya 31 wa mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), katika Kijiji cha Kondo Wilaya ya Bagamoyo, wamepanda mikoko zaidi ya 200,000 kwenye maeneo ya baharini yaliyoathiriwa na shughuli za kibinadamu.

Mtaalamu msimamizi wa kikundi cha wanufaika wa mpango ambacho asilimia 75 ni wanawake, Juma Amani amesema mikoko hiyo imepandwa kwenye eneo la ekari 12.

Alisema katika eneo hilo mazingira yameharibiwa na kusababisha samaki kutoweka wakiwamo dagaa na kamba hali iliyokuwa inawapa wakati mgumu kwa watumishi wa rasilimali za baharini.

Kutokana na walichokifanya anasema maeneo mengine wameanza kuiga na kupanda mikoko kwenye maeneo kama hayo ambayo mazingira yake yanaharibiwa na shughuli za binadamu.

Mratibu wa TASAF Mkoa wa Pwani, Roseline Kimaro, amesema kabla ya mradi huo wananchi walikuwa wanakata miti na kusababisha samaki kutoweka na baada ya upandaji mikoko unaoendelea hali imeanza kubadilika na samaki wameanza kuonekana.

Mkurugenzi wa Uratibu kutoka TASAF, Haika Shayo, amewapongeza wanufaika hao kwa kutekeleza shughuli za mpango huo kwa kupanda mikoko ambayo inakwenda kuzuia mmomonyoko na kupoteza rasilimali za baharini.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Jafary Athuman, alisema wananchi walichukua hatua hiyo baada ya kuona athari za uharibifu wa mazingira ambao umeanza kukikumba kijiji hicho ikiwamo mazalia ya samaki kutoweka na kuongezeka kwa kina cha maji.

Mmoja wa wanufaika, Mwanaheri Maulid, ameshukuru TASAF ilivyomsaidia kujikwamua na hali ya umaskini kutokana na ruzuku wanayopatiwa kusaidia kusomesha watoto na kuanzisha miradi ya kuwaingizia kipato.

Wataalamu kutoka mfuko huo wakiambatana na wadau wa maendeleo wamefanya ziara kwa wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini kufuatilia utekelezaji wa mpango kwa wanaoendelea na mpango na ambao tayari wametoka baada ya hali zao kuimarika katika Wilaya ya Bagamoyo.