EWURA yapiga marufuku uuzaji mafuta kwenye vidumu

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 07:04 AM Jun 29 2024
Uuzaji mafuta kwenye vidumu.
Picha: BBC Swahili
Uuzaji mafuta kwenye vidumu.

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Kati umewataka watu wanaouza mafuta kwenye vidumu kuacha mara moja ili kunusuru maisha yao.

Meneja wa EWURA wa Kanda hiyo,  Hawa Lweno alibanisha hayo jana jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kikao cha wadau wa sekta ya nishati na maji.

 Lweno, alisema tabia ya watu kuuza mafuta kiholela kwenye vidumu ni hatari kwa maisha yao kwa kuwa maeneo wanayoyatumia siyo salama.

“Uuzaji wa mafuta kwenye vidumu na maeneo yasiyo rasmi unaweza kusababisha majanga ambayo yatagharimu maisha ya watu wengi, hivyo nitoe wito kwa Watanzania wenzangu kuacha tabia hii ni hatari sana kwetu na kwa wale wanaotuzunguka,”alisema

Meneja Mawasiliano na Uhusiano EWURA, Titus Kaguo, alisema lengo la kikao hicho na wadau hao ni kutoa elimu kuhusu huduma wanazozitoa.

Kaguo, alisema moja kati ya changamoto iliyopo ni ukosefu wa elimu kwa jamii kuhusu huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo.

“Changamoto ambayo imejitokeza zaidi katika kikao hiki ni pamoja na usomaji mita za maji na upatikanaji wa mkataba wa huduma kwa wateja,” alisema. 

Alisema katika changamoto ya usomaji mita, watu wengi hawajui gharama halisi za uniti za maji hali ambayo imekuwa ikiibua malalamiko ya kubambikiziwa ankara za malipo.

“Pia watu bado hawajui umuhimu wa mkataba wa huduma kwa wateja ambao wanaweza kupata katika mamlaka husika na kuwasaidia kujua haki zao kwa huduma wanazozistahili,” alisema Kaguo.

Alitaja moja ya majukumu ya mamlaka hiyo ni kulinda mitaji ya wawekezaji na walaji kwa kudhibiti ubora wa bidhaa wanazozizalisha.

“Jukumu mojawapo la EWURA ni kulinda mitaji ya wawekezaji kama mwekezaji atashindwa kupata faida na kufunga uwekezaji basi itakuwa imeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kusaidia kulinda mtaji wa mwekezaji,”alisema

Alilitaja jukumu jingine kuwa ni kuchochea uchumi na maendeleo kwa kuhakikisha bidhaa zinazohakikiwa na mamlaka hiyo zinakuwa na ubora.

“Kama tukipima mafuta basi ubora ule hata mtu akitoka nje ya nchi akiweka mafuta yake kwenye gari liwake, lakini hata maji tunayazalisha hapa yawe kwenye ubora uleule na mataifa mengine yaliyoendelea,” alisema.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wajasiriamali Tanzania, Issa Njoka, alisema moja kati ya changamoto wanazukutana nazo katika uzalishaji wa bidhaa zao ni ukosefu wa umeme wa uhakika.

Njoka, alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha kuzalisha bidhaa zisokuwa na ubora kutokana na kukosekana kwa umeme wa uhakika.