Yanga kuuma na Safari Champion

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 07:48 AM Jun 29 2024
Kikosi cha Safari Champion.
Picha: Mtandao
Kikosi cha Safari Champion.

KIKOSI cha mabingwa wa soka nchini, Yanga leo kitashuka kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kupimana ubavu na kikosi cha Safari Champion katika mchezo maalum kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mchezo huo unaosubiriwa na mashabiki mbalimbali umepangwa kuchezwa kuanzia saa 2:15 usiku.

Kikosi kinachokutana na Yanga ni kile ambacho kilipatikana kupitia programu maalum iliyoendeshwa na TBL ambayo ilitafuta vijana  wenye vipaji  kutoka mikoa mbali mbali na kufanikiwa kuunda timu  yenye wachezaji 25.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kocha Mkuu wa timu ya Vijana ya Yanga, Soud Slim anayesimamia kikosi cha Yanga, alisema wamejiandaa vema kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo ambao utakuwa na upinzani mkubwa kutokana na uwezo wachezaji wanaounda kikosi cha Safari Champion. 

"Timu ya Safari  Champion ni timu yenye ushindani  kutokana na aina ya wachezaji waliopo ndani ya kikosi hicho, baadhi nimeona wana uwezo mkubwa sana na wataweza kutoa upinzani kwa kwetu, alisema Slim. 

Aidha aliwataka watanzania wajitokeze kwa wingi uwanjani hapo kushuhudia mchezo huo. 

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa timu ya Safari Champion, Sekilojo Chambua, alisema amewajenga kisaikolojia wachezaji wake ili waweze kuonyesha viwango vyao katika mchezo huo. 

"Nimewajenga kisaikolojia wachezaji wangu kuhakikisha wanafanya vizuri licha ya kuwa hawajawahi  kucheza michezo ya usiku," alisema Chambua. 

Alisema maandalizi ya siku 26 aliyoyafanya anaamini yatawasaidia kwa kiasi kikubwa kuonyesha vipaji vyao kupitia mchezo huo.