Watoto na Vijana kunufaika na Mradi wa USAID Kizazi hodari

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 12:57 PM Jun 28 2024
Mkurugenzi Mshiriki anayesimamia matokeo ya Asasi zinazotekeleza Mradi wa USAID kizazi Hodari akizungumza kwenye kikao hicho.
Picha: Marco Maduhu
Mkurugenzi Mshiriki anayesimamia matokeo ya Asasi zinazotekeleza Mradi wa USAID kizazi Hodari akizungumza kwenye kikao hicho.

WATOTO na vijana chini ya umri wa Miaka 17 kuendelea kunufaika na Mradi wa “USAID Kizazi Hodari” unaotekelezwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) katika Mikoa tisa (9) Nchini, kwa ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya kimataifa (USAID).

Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi Mshiriki anayesimamia Matokeo na Asasi zinazotekeleza Mradi wa “USAID Kizazi Hodari” Kanda ya Kaskazini mashariki Aminiel Mongi kwenye kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Mradi huo Mkoani Shinyanga.

Amesema Mradi huo pamoja na mambo mengine umelenga kuboresha Afya, ustawi na ulinzi wa watoto walio katika mazingira hatarishi na vijana chini ya Miaka 18 ili kutokomeza maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI.

“Mradi huu unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani USAID ambao ndio wafadhili wakuu, na Mradi unatekelezwa na Makao Makuu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)katika Mikoa tisa (9) ikiwa na jumla ya Halmashauri 41 Mikoa hiyo ni Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Singida, Dodoma, Mwanza, Geita pamoja na Mara”.

“Lengo kuu la Mradi huu ni kuboresha Afya, ustawi na ulinzi wa watoto waliokatika mazingira hatarishi na vijana kuanzia umri wa Miaka 0 hadi 17 ili kufikia malengo ya kidunia ya kupambana na virusi vya UKIMWI,”Amesema Mongi

"kwa maana wale wenye maambukizi waweze kujua hali zao za maambukizi lakini pia wale ambao wamefahamu hali zao za maambukizi waweze kuunganishwa na vituo vya tiba na mafunzo kwa ajili ya kuanzishiwa dawa lakini pia wale ambao wameanzishiwa dawa kufika kwenye vituo ili kufubaza maambukizi ya virusi vya UKIMWI”. Ameongeza.

Aidha, amesema, Makundi yanayofikiwa wakati wa utekelezaji wa Mradi huo ni pamoja na watoto walioathirika na virusi vya UKIMWI, watoto wa wanawake walioko katika mazingira hatarishi, pamoja na watoto walioathirika na matukio ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia, ambapo amesema kupitia Mradi huo watoto wanapata huduma mbalimbali zikiwemo za kiafya.

Ameeleza zaidi kuwa zipo afua mbalimbali ambazo zinalenga kuwaimarisha kiuchumi walezi wa watoto pamoja na mabinti au wanawake walio katika umri mdogo kwenye ngazi ya Kaya, huku akitaja shughuli zingine zinazofanyika ambazo zinagusa sekta mbalimbali ikiwemo Afya na Elimu.

Amesisitiza kwamba  kuna maeneo ambayo wanayalenga katika utoaji wa huduma ikiwemo suala la Afya kwa kuhakikisha walengwa wanakuwa na Afya bora na pia watawapatia bima za Afya ili waweze kupata matibabu kwa urahisi, lakini pia kuna huduma ya elimu tunahakikisha wanafunzi wanahudhuria shule.

Mchumi Mkuu idara ya Afya, lishe na ustawi wa jamii kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Rashid Kitambulio, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa la KKKT katika kufikia Malengo yaliyokusudiwa huku akishukuru kwa Mradi huo wa USAID kizazi hodari ambao unaendelea kuwanufaisha wahanga hasa wa Maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Zabron Masatu, amesema Mradi wa USAID kizazi hodari umekuwa na manufaa makubwa hasa katika Sekta ya Afya ambapo pamoja na mambo mengine baadhi ya familia wamepatiwa ufadhili wa kadi za bima ya Afya, na kwamba Kandi hizo zimekuwa zikiwasaidia katika kupata matibabu ya watoto na familia kwa ujumla.

Naye Mratibu wa Mikoa na Halmashauri kutoka tume ya kuthibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) amepongeza kwa Mradi huo kuendelea kuwatambua na kuwawezesha kupata huduma zinazostahili waathirika wa Virusi vya UKIMWI ambapo ameshauri Mradi wa ‘USAID Kizazi Hodari’ uwe endelevu ili kuzuia Maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi.