Ugonjwa Marburg waua mtu mmoja

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 08:51 AM Jan 25 2025
Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya, Dk. Ntuli Kapologwe.
Picha: Wizara ya Afya
Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya, Dk. Ntuli Kapologwe.

WIZARA ya Afya, imesema mtu mmoja amefariki dunia kwa ugonjwa wa Marburg mkoani Kagera, wakati akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo.

Mtu huyo alikuwa  kati ya wawili waliobainika awali kuwa na ugonjwa huo na kulazwa hospitalini hapo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani humo, Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya, Dk. Ntuli Kapologwe, alisema kifo hicho kilitokea Januari 21, mwaka huu, na mmoja anaendelea na matibabu na afya yake inaendelea vizuri.

Dk. Kapologwe alisema wanaendelea kuwafuatilia kwa siku 21 watu 281 ambao walichangamana na  watu waliothibitika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo ili kuona kama wataonesha dalili zozote.

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Magembe, alisema idadi ya wahisiwa inabadilika kulingana na watu wanaokwenda kutoa taarifa wanapohisi kuwa na dalili na hadi jana, wahisiwa walifika 15.

Dk. Magembe alisema wahisiwa hao walifanyiwa kipimo kimoja ambacho hakikuonesha kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo na watarudia baada ya saa 72.

Alisema dalili za ugonjwa huo zinafanana na za magonjwa mengine kama vile malaria, maambukizi kwa njia ya mkojo (UTI) na magonjwa ya tumbo. 

Alisema kutokana na hali hiyo, watu wakienda hospitalini kwa magonjwa mengine wanawapima na ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Dk. Magembe, idadi ya wahisiwa inabadilika kila siku kutokana na idadi ya watu watakaojitokeza kupima wakijihisi kuwa na dalili za ugonjwa huo.

Alisema licha ya kuthibitika kuwapo kwa ugonjwa huo katika kata mbili za wilaya ya Biharamulo, hatua zote stahiki za kujikinga na ugonjwa huo zimechukuliwa na watu wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.

“Hii inatuonesha kwamba tunaweza kuendelea na shughuli wakati tukizingatia kanuni zote za afya ambazo zinatusaidia tusieneze haya maambukizi,” alisema.

Januari 20, mwaka huu, Shirika la Afya Duniani (WHO) liliipatia Tanzania Sh. bilioni 7.55 ili kudhibiti na kukabiliana na ugonjwa huo.

Januri 21, mwaka huu, akizungumza na waandishi wa habari Ikulu ya Chamwino, Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan, aliwahakikishia Watanzania na jumuiya ya kimataifa kuwa Tanzania ni eneo salama licha ya kubainika kisa kimoja cha mtu mmoja kupata maambukizi hao.

Alisema hatua zilizochukuliwa kudhibiti virusi hivyo vilipobainika nchini mwaka 2023 zimeiwezesha Tanzania kuwa na uzoefu wa kutosha kudhibiti maambukizi.