TMDA yanasa dawa ‘feki’ za kuongeza nguvu za kiume

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:57 PM Mar 28 2024
Dawa za kuongeza kuvu za kiume.
PICHA: Mtesco enterprises
Dawa za kuongeza kuvu za kiume.

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) Kanda ya Magharibi imekamata shehena ya dawa zenye thamani ya Sh. milioni 3.97 zinazodaiwa kuongeza nguvu za kiume.

Pia imekamata vifaa tiba vinavyodaiwa kuibiwa na watumishi wa serikali na kuviuza katika hospitali binafsi kinyume cha sheria.

Akizungumza na Nipashe kuhusu kukamatwa kwa vitu hivyo, Meneja wa TMDA Kanda, Dk.Christopher Migoha alisema dawa hizo zimo pia zinazotumiwa zaidi katika jamii, zikitajwa kuwa hatari kwa afya ya binadamu.

Dk.Migoha alisema katika operesheni waliyoifanya walikamata sigara dawa 8,642 zenye thamani ya zaidi ya Sh.milioni 2.1 ambako kati ya hizo sigara 2,140 zinatoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) pamoja na aina ya clabu 1,038 zinazotoka India.

Alisema dawa hizo zina madhara makubwa kwa afya ya binadamu, zinasabibisha ongezeko la msukumo wa damu mwilini hali inayoathiri mfumo wa upumuaji na ubongo, wakati mwingini kusababisha matatizo ya kisaikolojia.

Alisema dawa nyingine zilizobainika zinatokea katika nchi za India, Burundi na Congo ambapo idadi kubwa ya dawa hizo zimemalizika muda wake wa matumizi lakini jamii imekuwa ikizinunua na kuzitumia.

Kadhalika alisema kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Machi 2024 walikagua mifumo 30 ya mionzi ‘x-ray’, m-ray na’ utra sound’ ambapo walibaini mifumo mitano haifanyikazi na 25 peke ndiyo inayofanya kazi.