Serikali yasema neno kikokotoo mafao

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:51 AM Nov 16 2024
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete.
Picha: Mtandao
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete.

SERIKALI imesema uwiano wa kikokotoo kwa sekta ya umma na binafsi ni suala linalozungumzika na tayari imeelekeza Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuliangalia suala hilo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, aliyasema hayo jana alipokuwa akifungua mkutano mkuu wanane wa kazi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) uliofanyika mjini hapa.

Ridhiwani alisema amesikia hoja ya kuhusu kutokuwapo kwa uwiano muafaka wa kikokotoo kwa sekta zote mbili.

Alisema maboresho yaliyofanyika kwa mujibu wa hoja yao, yameleta tofauti kubwa ya viwango kwa sekta ya umma kulipwa mkupuo wa asilimia 40 huku sekta binafsi ikibakia na asilimia 35.

Ridhiwani alisema serikali imeshatoa maelekezo hayo kwa taasisi hizo mbili na kwamba watakapokuwa tayari watatoa taarifa kwa shirikisho hilo kuhusu kima kilichofikiwa na msawazo ambao utakuwa umeangaliwa.

 “Kwa sasa suala hili linazungumzika hivyo ni
 jukumu lenu kujiandaa na litakapoletwa katika ushirikishwaji muwe tayari kueleza hisia zenu,” alisema.

Ridhiwani alisema katika bajeti ya 2024/25, serikali ilielekeza kufanyika mapitio viwango vya mafao kwa wastaafu na kuanzia mwezi Juni, mwaka huu, ilianza kulipa mafao ya mkupuo kwa wastaafu kutoka asilimia 33 hadi 40.

Alisema serikali imefanya ongezeko la asilimia mbili kwa pensheni kuanzia mwezi Januari, 2025.

 Kuhusu kuboresha mishahara, Kikwete alisema serikali itaendelea kuiboresha na maslahi mengine kadri uchumi wa nchi utakapohimilika.

 “Niwahakikishie lengo la serikali ni
 kuendelea kuboresha mishahara ya wafanyakazi na maslahi mengine kadri uchumi wa nchi yetu utakavyohimili vipaumbele vya Taifa.

“Ninapenda pia kuwafahamisha kuwa serikali katika kupunguza makali ya maisha imeridhia taasisi za umma kuandaa Mpango Motisha (Incentive Package) kulingana na tija na uwezo wa taasisi husika,” alisema.

Waziri alisema serikali inahimiza suala la
 matumizi ya vyombo vya mashauriano hususani, LESCO, bodi za mishahara na mabaraza ya wafanyakazi na haitavumilia ulegevu katika kuitishwa kwa vikao hivyo kwa vile imeandaa rasilimali za kutosha kwa ajili ya vikao hivyo.

 SERA YA AJIRA KUPITIWA

 Kikwete alisema Wizara tayari  imeanza mchakato wa kurejea sera ya ajira ambayo imesheeni mikakati ya kukuza ajira na mkazo mkubwa umewekwa katika mazingira wezeshi kwa ajili ya vijana kujiajiri na kuwajengea uwezo wa kuajirika.

“Hapa tunazungumzia sera ya kazi ya kujitolea, sera za ajira za muda mfupi na mrefu na sera inayotambua uwapo wa wenzetu aliosomeshwa vizuri, lakini bado wanazurura hawana kazi,”alisema.

 Alikemea baadhi ya vyama ambavyo vimeendekeza migogoro ya uongozi ndani ya  chama na baina ya chama na chama.

“Ninazo taarifa pia kwa baadhi ya vyama kugombea au kunyang’anyana wanachama. Hali hii haina afya katika umoja na mshikamano wenu, serikali inahitaji vyama imara vinavyoweza kushiriki kikamilifu na kwa weledi katika meza ya majadiliano,” alisema.

 Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya alisema uongozi wake umerejesha rasilimali za shirikisho ikiwamo majengo yalikuwapo Dodoma na Arusha ambayo yatasaidia kujiimarisha kwenye mapato.

 Akisoma risala ya TUCTA, Katibu Mkuu, Hery Mkunda, alisema tofauti iliyopo katika uwiano wa kikokotoo inaleta hisia za upendeleo na shirikisho linashauri milango ya mashauriano ifunguliwe ili jambo hilo
 lijadiliwe na muafaka upatikane.

 Kuhusu ukosefu wa ajira, alisema TUCTA inapendekeza kuanzishwa kwa miradi mingi ya serikali kadri iwezekanavyo ili iajiri sehemu kubwa ya vijana
 wanaozunguka kutafuta wapate ajira kupitia miradi hiyo.

 “Tunashauri serikali itupie macho utekelezaji wa sera ya ajira ya wageni, kwani kuna dalili za wazi za
 ukiukwaji wa sera hiyo.

“Ukosefu wa ajira unawaweka Watanzania katika hatari ya kutumikishwa kwa ujira mdogo na kazi zisizo za staha,” alisema.

 Alishauri serikali irejeshe chombo cha kusimamia na kudhibiti mifuko ya hifadhi ya jamii (SSRA) kwa kuwa wanaamini chombo hicho kina umuhimu mkubwa wa kusimamia mifuko ya hifadhi ya jamii.