Rais apongeza mashirika kupunguza hasara

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 11:25 AM Mar 29 2024
Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza baada ya kupokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2022/2023 pamoja na taarifa ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa mwaka 2022/2023.

Rais Samia Suluhu Hassan amesema mwenendo wa mashirika ya umma unatia moyo kutokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuonesha kuwa baadhi ya mashirika yamefanikiwa kupunguza hasara.

Akizungumza Ikulu jijini Dodoma baada ya kupokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2022/2023 pamoja na taarifa ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa mwaka 2022/2023 leo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo Machi, 28, 2024.

Rais Samia amesema hatua zinazochukuliwa itafika wakati mashirika hayo hayatopata hasara tena. "Mashirika mbalimbali pamoja na kwamba yanafanya hasara lakini yanakwenda mbele; hasara ya mwaka jana sio hasara ya mwaka huu, hasara ya mwaka juzi sio hasara ya mwaka unaofuata.Tutafika pahali watakuwa kwenye faida," amesema Rais Samia.

Baadhi ya mashirika ya umma yaliyofanikiwa punguza hasara ni pamoja na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kutoka shilingi bilioni 19.2 hadi milioni 894, Shirika la Reli Tanzania (TRC) kutoka shilingi bilioni 190 hadi shilingi bilioni 100 pamoja na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutoka shilingi bilioni 205.9 hadi shilingi bilioni 156.7

Aidha, amesema ripoti hizo zinaimarisha utendaji ndani ya Serikali na mashirika ya umma na kusaidia kupunguza hasara na kwamba dosari zilizotolewa zitafanyiwa kazi na anaamini mwakani hazitojirudia.

Ameongeza kuwa uwekezaji unaofanywa kwenye ofisi za CAG na TAKUKURU pamoja na taasisi nyingine unazifanya ziaminike kwa wananchi kwa kutoa ripoti nzuri pamoja na kuaminiwa kimataifa.