Polisi watia fora maandamano CHADEMA

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 09:20 AM Apr 23 2024
Baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa na mkoa wa Kagera wakiongozwa na askari polisi katika maandamano ya amani katika Kata ya Kashai, Hamgembe, Bilele Rwamishenye, Manispaa ya Bukoba.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa na mkoa wa Kagera wakiongozwa na askari polisi katika maandamano ya amani katika Kata ya Kashai, Hamgembe, Bilele Rwamishenye, Manispaa ya Bukoba.

ASKARI Polisi walitia fora katika maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kuwa mstari wa mbele ikiwa ishara ya kuimarisha ulinzi hali iliyofanya jambo hilo kufanyika kwa amani.

Katika baadhi ya picha zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii, askari hao, wakiwamo wa usalama barabarani, walionekana wakiwatangulia wanachama na wafuasi hao wakati wakiandamana. 

Hali hiyo inazidi kuonyesha tofauti kubwa kwa sasa na nyakati zilizopita ambapo kulikuwa na mivutano baina ya viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama vya upinzani upande mmoja na askari polisi upande mwingine. 

Hata katika maandamano yaliyotangulia ya CHADEMA, yakiwamo yaliyofanyika Dar es Salaam, kulikuwa na hali ya utulivu mkubwa na amani huku polisi wakiwasindikiza na kulinda usalama.     

KAULI YA MBOWE

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mashujaa, mjini Bukoba, baada ya maandamano aliyoyaongoza kuanzia Mafumbo Centre, Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ameeleza kukerwa na tabia ya  baadhi ya viongozi wa serikali na watumishi wa umma, kumsifia Rais Samia Suluhu Hassan, kwenye kila jambo wanaloliezea kwa wananchi huku akitaja kitendo hicho kuwa ni ‘uchawa’.

Mbowe amesema kitendo hicho kinampunguzia sifa Rais Samia na kwamba miongoni mwa maneno aliyowahi kumwambia Rais alipokutana naye na kufanya mazungumzo, ni kuachana na sifa anazopewa na viongozi hao, akiwataja kuwa ni ‘chawa’ watakaomgharimu baadaye.

“Unakuta kila anayeongea anasema fedha hii ya ujenzi ametoa ‘mama’. Niliwahi kumwambia hii tabia ya kukusifia kila jambo, eti fedha umetoa wewe, itakugharimu. hao ni chawa.

“Nchi ina hali ngumu na hali hiyo inatokana na serikali kutosikiliza maoni ya wananchi. Gharama  kubwa za maisha zinatokana na tozo na kodi kubwa inayotozwa na serikali huku chawa kazi yao ni kusifia tu wakati hali ya maisha ngumu,” amesema.

Mbowe amesema hatua ya chama hicho kufanya maandamano ni kupaza sauti za wananchi wasio na pa kusemea ili kufikisha ujumbe kwa serikali kufanya mabadiliko na maboresho ya maeneo kadhaa ikiwamo kushusha gharama za maisha.

“Mimi ninaendelea na maandamano. Kesho (leo) naenda Kahama, kila mmoja anaenda eneo lake. Lissu anaanza Arusha, Babati, Singida, Dodoma, Dar es Salaam tutakutana kupeana taarifa, sasa hivi ni ‘bampa to bampa’. Tunafanya  kwa makini kuleta mabadiliko ya nchi yetu.”

“Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeshindwa kulinda mali, rasilimali, nyingi zinapewa wageni. Kwa kipindi cha miaka 60 ujenzi wa barabara kumpa mgeni kandarasi ujenzi ni aibu, CHADEMA hatutafanya hivyo.

“Makampuni yote ya Kitanzania yaliyojenga barabara kuanzia mwaka 2014 yamefanya kandarasi za zaidi ya Sh. bilioni 633 nchi nzima. Tanzania shamba la bibi, wanapewa wageni ambao wamelipwa Sh. trilioni 11 kwa sababu zinalipwa kama fedha ya kigeni,” amesema.

Mbowe amesema amebaini kampuni 10 za kigeni zimepewa kazi ya kujenga barabara na hujenga kwa viwango duni, jambo linalosababisha kuharibika ndani ya muda mfupi. Alisema kampuni hizo zinapaswa kufanya kazi kwa ubia na wazawa.

“Hebu fikiria habari ya kikokotoo kwa watumishi, wabunge wanakaa Dodoma kuzungumzia na kuibua mafao ya wake wa wastaafu wa viongozi. Kagera tupate majimbo sita tulete mabadiliko,” amesema.

Mbowe amesema kitendo hicho kinatokana na bunge kuwa na idadi kubwa ya  wabunge wa chama kimoja ambao hupitisha jambo lenye maslahi mapana ya nchi kwa manufaa ya wachache.