Nderiananga ataka suala la maafa kuwa ajenda kwenye vikao

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 02:37 PM Jul 25 2024
NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga.
Picha: Mpigapicha Wetu
NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga.

NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga amesema ni muhimu masuala ya usimamizi wa maafa kujumuishwa katika mipango ya maendeleo ya wilaya katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku sambamba na jambo la maafa kuwa ajenda kwenye vikao vya ushauri vya wilaya.

Nderiananga aliyasema hayo  alipokuwa akizindua nyaraka za usimamizi wa maafa kwa Wilaya ya Kibiti ambapo pamoja na mambo mengine alisema uandaaji wa nyaraka hizo za usimamizi wa maafa ni hatua moja wapo katika kuelekea ujenzi wa jamii iliyostahimilivu dhidi ya majanga katika wilaya hiyo.

Alisema ni vema Wakuu wa Wilaya katika vikao vyao vya ushauri wakawa na ajenda ya maafa badala ya kusubiri majanga na kwa kufanya hivyo itasaidia kuepuka atthari zinazoweza kutokea na pia kujipanga namna ya kukabiliana nazo.

Akizungumzia kuhusiana na nyaraka hizo za usimamizi Naibu Waziri huyo alisema nyaraka hizo zilizoandaliwa zinatakiwa kuwa chachu ya kuongeza ushirikishwaji wa jamii na wadau sambamba na kujenga uelewa kuhusiana na masuala ya usimamizi wa maafa na kuimarisha mfumo wa utoaji tahadhari ya awali katika kukabiliana na maafa.

Pia alisema Ofisi ya Waziri mkuu ambayo ndio yenye jukumu la kuratibu na kusimamia maafa itaendelea kutafuta rasilimali kwa ajili ya kuimarisha na kujenga uwezo wa kamati za usimamizi wa maafa ngazi ya mkoa na Wilaya ambapo pia alisisitiza ngazi ya wilaya kufanya jitihada kama hizo ngazi ya kata na Vijiji.

Kadhalika alisema kazi ya uandaaji wa mpango wa kujiandaa na kukabiliana na maafa na mkakati wa kupunguza vihatarishi vya Maafa kwa Wilaya ya Kibiti ni muendelezo wa utekelezaji wa jukumu la msingi la Ofisi ya Waziri Mkuu ambalo limelenga kuimarisha usimamizi na uratibu wa Maafa katika ngazi za Mikoa na Wilaya.

Mwakilishi wa UNDP Abbas Kitogo.
Awali Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Brigedia Jenerali Hosea Ndagala alisema Ofisi yake  kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ilianza utekelezaji wa kazi hiyo kwa Kutoa mafunzo ya kujengea uwezo kamati elekezi na Kamati ya wataalamu ya Usimamizi wa Maafa kwa Wilaya ya Rufiji na Kibiti.

Alisema mafunzo hayo yalilenga kuimarisha zaidi kamati za usimamizi wa maafa kwa kufahamu majukumu yao kisheria, mfumo wa usimamizi wa maafa nchini pamoja na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maafa kwa vipindi tofauti ikiwa ni kabla, wakati na baada ya maafa kutokea kwa kufuata mpango wa usimamizi wa maafa.

“Uandaaji wa nyaraka hizi umezingatia ushirikishwaji wa jamii, wataalamu wa Halmashauri na Taasisi za kiserikali katika utaratibu wa ukusanyaji wa taarifa za msingi na ushirikiano ulikuwa mzuri na mchakato wa uandaaji ulianza Juni 24,2024 hadi leo unapoenda kuzindua rasmi nyaraka hizi.”alsema Brigedia Jenerali Ndagala

Hata hivyo Brigedia  Jenerali amewashukuru  wadau wa maendeleo UNDP kwa ufadhili ambao umechangia jitihada za Serikali katika kutekeleza kazi hii pamoja na uongozi Wilaya ya Kibiti kamati elekezi ya usimamizi wa maafa.

Mwakilishi wa UNDP Abbas Kitogo ambaye pia ni mtaalamu wa miradi amesema amesema wataendelea kushirikiana na Serikali katika masuala mbalimbali kuondoa vikwazo vya maendeleo na kuhakikisha elimu ya maafa inaifikia jamii kupitia kamati husika ili waweze kueouka majanga yanayoweza kuwakumba.

Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanal Joseph Kolombo ameishukuru Ofisi ya Wazairi Mkuu kwa kufika katika Wilaya hiyo na kutoa elimu ya maafa na kwamba muongozo wa nyaraka za usimamizi ambao umezinduliwa utakwenda kusaidia kuchukua tahadhari ya mafuriko na namna ya kukabiliana nayo.

1