JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani limewakamata watu watatu wakiwa na mtoto wa miezi saba, Merysiana Melkzedeck, wanaodaiwa kumwiba kwa wazazi wake katika tukio la uvamizi lililotokea Januari 15, mwaka huu.
Tukio hilo lililotokea saa moja asubuhi Galagaza, Kata ya Msagani, wilayani Kibaha, mkoani Pwani. Watu wanne wakiwa na mapanga na nondo walimvamia nyumbani kwake na kumjeruhi mfanyabiashara Melkizedeck Sostenes (28).
Watu hao pia, walimfunga kamba na kumtumbukiza kwenye shimo la maji taka kisha kumchukua mke wake, Johana Gabriel na mtoto huyo na kuondoka nao kusikojulikana.
Vilevile, watu hao waliiba gari dogo aina ya IST lenye namba za usajili T.331 DLZ, runinga aina ya Haier nchi 42, kompyuta mpakato tatu na simu tano za aina mbalimbali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi (ACP) Salim Morcase, alisema baada ya msako waliwakamata watuhumiwa hao jana saa 9:00 alfajiri wakiwa wamejificha katika msitu ulioko kati ya eneo la Kimara Misale na Serengeti "B" Kata ya Dutumi.
Alisema mtoto aliyepatikana alipelekwa Hospitali ya Rufani Tumbi kwa uchunguzi zaidi.
“Jeshi la Polisi tulifanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu ambao walihusika katika tukio hili wakiwa na mtoto wa kike mwenye umri wa miezi saba akiwa hai waliomchukua katika tukio la uvamizi la 15/01/2025,” alisema.
Pia alisema Jeshi la Polisi lilifanikiwa kukamata gari lililoibwa katika uvamizi huo, pete ya ndoa ya mke wa Melchizedek, simu aina ya Redmi na kompyuta mpakato moja.
Alisema baada ya kupokea taarifa ya uvamizi huo, Kamanda Morcase aliambatana na wataalamu wa kuchunguza matukio makubwa ambapo walifika eneo la tukio na baada ya kupata taarifa msako ulifanyika na kukamatwa kwa wahalifu na kupatikana mama na mtoto waliochukuliwa.
“Mke wa Melchizedek alipatikana saa 10:00 jioni akiwa ametumbukizwa katika shimo la nyumba ya jirani umbali wa mita 300, ambalo halikuwa limeanza kutumika,” alisema.
Morcase alisema upelelezi unaendelea ikiwamo kusakwa kwa mtuhumiwa mmoja, huku Jeshi la Polisi likitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu haraka kwa viongozi walioko maeneo yao ili hatua za haraka zichukuliwe.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED