VILIO na simanzi jana vilitawala katika Kijiji cha Shigatini, Tarafa ya Ugweno, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, baada ya mwili wa askari wa daraja la kwanza wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na wanawe watatu wa kike miili yao kuwasili nyumbani kwao Lomboni kwa maziko.
Askari huyo na wanawe, Mariam Zuberi (9), Salma Zuberi (7) na Bisma Zuberi (3), walipoteza maisha baada ya makazi yao kuteketea kwa moto wakiwa wamelala Juni 22, Olmatejoo jijini Arusha.
Miili yao iliwasili jana saa 6:00 mchana kwa magari maalum ya TANAPA na kuzikwa saa 10:00 jioni katika makaburi ya familia ya Msemo, yaliyoko kitongoji cha Lomboni.
Askari huyo wa uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, alirejea Arusha ilipokuwa familia yake kwa ajili ya kumpa hongera mkewe aliyekuwa amejifungua wiki moja iliyopita.
Watoto wake watatu walipoteza maisha papo hapo wakati moto ukiendelea kuteketeza nyumba yao na baba mzazi wa watoto hao, Zuberi alifariki dunia Juni 23, wakati akipatiwa matibabu Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.
Waombolezaji na ndugu wa marehemu, akiwamo Twahia Msuya, wameeleza kuwa vifo vya pamoja vya ndugu zao vimeacha pengo kubwa.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Abdallah Mwaipaya, aliwaongoza mamia ya waombolezaji katika maziko ya familia hiyo.
Akizungumzia tukio hilo juzi, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani humo, Jeradi Nonkwe, alisema chanzo cha moto huo ni kompyuta mpakato (laptop) iliyokuwa imechomekwa kwenye soketi ya umeme kushika moto na kuunguza kochi.
Watu wengine saba walionusurika akiwamo mtoto mchanga wa siku nne, walikimbizwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Arusha ya Mount.
Majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu ni mama wa watoto hao, Jasmine Khatibu (33), Mariam Mussa (60) ambaye ni mama mzazi wa Zuberi na Mwanaidi Aldina (50).
Wengine ni Mussa Msemo (34), AbdulKarim Ramadhan (9) na mfanyakazi wa ndani aliyefahamika kwa jina moja la Ester (20).
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED